Wanatasnia wa filamu na michezo ya kuigiza nchini wameaswa kujua
thamani yao na kazi zao katika kulinda maadili na utamaduni wa kitanzania ili
kujijengea heshima mbele ya jamii na wapenzi wa kazi zao.
Rai hiyo imetolewa leo na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu nchini Bibi. Joyce
Fissoo alipokuwa akizungumza na viongozi wa Kamati ya Matukio, Maadili na
Mikataba wa Chama cha Waigizaji Mkoa wa Kinondoni (Tanzania Drama Film
Actors Association - Kinondoni) walipotembelea na kufanya kikao katika Ofisi za
Bodi ya Filamu Mtaa wa Samora Jijini Dar es salaam.
Bibi. Fissoo alisema baadhi ya wanatasnia ya filamu wanaonyesha mwenendo
unaokinzana na maisha na maadili ya kitanzania huku miongoni mwao wakifanya
vitendo vinavyodhalilisha utu na heshima hivyo kuitia doa tasnia nzima ya filamu
na michezo ya kuigiza.
“Nawapongeza Chama cha Waigizaji kwa kushirikiana na serikali katika kukemea
wale wanachama wachache wanao chafua taswira ya tasnia. Ni muhimu kuendelea
kuongeza nguvu katika nidhamu, matumizi ya lugha zenye staha, mavazi
yanayoonyesha taswira chanya ya taifa letu; hivyo endeleeni kuiunga mkono
Serikali katika hatua inazozichukua” alisema Fissoo.
Kwa upande wake Msemaji wa Chama hicho Bw. Masoud Kaftany alisema lengo
la kukutana na Bodi ya Filamu Tanzania ni kuwatambulisha viongozi na kamati ya
matukio, maadili na mikataba kutoka kwenye chama cha Waigizaji Kinondoni kwa
uongozi wa Bodi ya Filamu kama njia mojawapo ya kuendeleza ushirikiano katika
tasnia hiyo.
“Kamati yetu inaundwa na wawakilishi 13 wakiongozwa na Mwenyekiti bwana
Ahmad Hussein, Katibu bwana Khalifan Ahmed na Msemaji bwana Masoud
Kaftany na leo tumekuja Bodi ya Filamu kujitambulisha na kujifunza Sheria,
Kanuni na Taratibu zinazotakiwa kufuatwa ili zitusaidie katika utendaji wa kila
siku wa kazi zetu” alisema Kaftany.
Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati ya Chama hicho Bi. Vanitha Omari
ameiomba Bodi ya Filamu kutochoka kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wadau
wa sekta ya filamu ili waweze kupata uelewa stahiki katika tasnia kwa ujumla.
Chama cha waigizaji wa filamu Mkoa wa Kinondoni ni miongoni mwa vyama
vinavyounda vyama vya waigizaji wa filamu taifa na ni chama ambacho kimekuwa
mfano katika kutetea maslahi na haki za wanachama wake.
Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Tanzania Bibi. Joyce Fissoo (katikati)
akiongoza kikao na viongozi wa Kamati ya Matukio, Maadili na Mikataba wa
Chama cha Waigizaji Mkoa wa Kinondoni (Tanzania Drama Film Actors
Association-Kinondoni) walipotembelea ofisi za Bodi ya Filamu kuwatambulisha
viongozi wa chama hicho kwa uongozi wa Bodi ya Filamu hivi karibuni katika
Ofisi za Bodi ya Filamu Mtaa wa Samora jijini Dar es salaam.
Baadhi ya wanachama na viongozi wa Kamati ya Matukio, Maadili na
Mikataba wa Chama cha Waigizaji Mkoa wa Kinondoni (Tanzania Drama Film
Actors Association-Kinondoni) wakifuatilia taarifa iliyokua ikitolewa wakati wa
kikao na Bodi ya Filamu kuwatambulisha viongozi hao hivi karibuni katika Ofisi
za Bodi ya Filamu Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Tanzania Bibi. Joyce Fissoo (wanne kulia)
katika picha ya pamoja na Wanachama na Wajumbe wa Kamati ya Matukio,
Maadili na Mikataba wa Chama cha Waigizaji Mkoa wa Kinondoni (Tanzania
Drama Film Actors Association-Kinondoni) baada ya kikao na wajumbe hao
walitembelea ofisi za Bodi ya Filamu kuwatambulisha viongozi wa chama hicho
kwa uongozi wa Bodi ya Filamu hivi karibuni katika Ofisi za Bodi ya Filamu Jijini
Dar es salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...