Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (katikati mbele) pamoja na msafara wake wakiendelea na ziara katika machimbo ya dhahabu ya Msege yaliyopo wilayani Tarime mkoani Mara.

Na Greyson Mwase, Tarime

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko ametatua mgogoro kwenye machimbo ya madini ya dhahabu ya Msege yaliyopo wilayani Tarime mkoani Mara kwa kuitaka kampuni inayojishughulisha na uchimbaji wa madini hayo ya Everson Limited kuhakikisha inasaini mikataba kati yake na wachimbaji wadogo wa madini wanaoendesha shughuli za uchimbaji madini na kushirikiana kwa karibu zaidi. Naibu Waziri Biteko ametoa agizo hilo mara baada ya kutembelea machimbo hayo leo tarehe 19 Septemba, 2018 na kusikiliza kero za wachimbai wadogo wa madini ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika mikoa ya Mara na Geita yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini, kusikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wachimbaji wa madini.

Katika hatua nyingine, Biteko alimtaka mmiliki wa kampuni ya Everson Limited, Mwita Wambura kuhakikisha anasimamia makubaliano aliyojiwekea kati ya wachimbaji wadogo wa madini na kampuni yake huku akihakikisha sheria na kanuni za uchimbaji wa madini zinafuatwa.

Alisema kuwa mara baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote mbili yaani kampuni na wachimbaji hao alibaini kuwa kampuni husika ilikataa kusaini mikataba kati yake na wachimbaji wadogo wa madini kinyume na makubaliano hali iliyopelekea mgogoro kutokuisha.
Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko akiangalia sehemu ya nyaraka mbalimbali za uchimbaji madini katika machimbo ya dhahabu ya Msege yaliyopo wilayani Tarime mkoani Mara.

“Haiwezekani kama kampuni mnakaa katika vikao kwa kushirikisha viongozi wa serikali na kukubaliana kuandaa mikataba ili kusaini halafu baadaye mnashindwa kutekeleza makubaliano, kama Serikali tunataka kuhakikisha kila upande unanufaika, huku Serikali ikipata mapato yanayostahili,” alisisitiza Biteko.

Aliendelea kusema kuwa, Serikali ina haki ya kuchukua leseni ya kampuni yoyote pale inapoonekana makubaliano kati yake na wachimbaji wadogo hayafuatwi hali inayosimamisha kukwama kwa shughuli za uchimbaji madini na kukosa mapato yake.

Wakati huo huo wananchi kutoka sehemu mbalimbali katika Wilaya ya Tarime walimpongeza Naibu Waziri Biteko kwa kuhakikisha kuwa mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu pasipo kupatikana suluhu unatatuliwa ndani ya kipindi kifupi na kusisitiza kuwa wataendelea kutoa ushirikiano kwa Wizara ya Madini kwa kuhakikisha wanafuata sheria na kanuni za madini huku wakilipa kodi zote serikalini.
Mmoja wa wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu katika machimbo ya dhahabu ya Msege yaliyopo wilayani Tarime mkoani Mara akiwasilisha kero yake mbele ya Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo pichani).

Akizungumza kwa niaba ya wachimbaji wa madini, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji wa Madini Mkoa wa Mara, Stephan Msseti alimpongeza Biteko kwa kuhakikisha amefika kwenye machimbo hayo na kutatua mgogoro na kufafanua kuwa sasa wachimbaji wadogo wataanza kuchimba katika mazingira ya amani na kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi.

Msseti alimtaka mmiliki wa kampuni ya uchimbaji wa madini ya dhahabu ya Everson Limited, Mwita Wambura kuhakikisha anaheshimu mamlaka za serikali kwa kuhakikisha anatekeleza makubaliano yote wanayojiwekea.

Awali akizungumzia mgogoro huo, mmiliki wa kampuni ya uchimbaji wa madini ya dhahabu ya Everson Limited, Mwita Wambura alisema kuwa mara baada ya kufanya utafiti na kuanza uchimbaji wa madini ya dhahabu katika eneo hilo, wananchi walianza kuvamia eneo hilo hali iliyopelekea mgororo.

Alisema kuwa aliwaruhusu wachimbaji wadogo kuchimba madini katika mashimo matano lakini wachimbaji hao wamekuwa wakidhuru wafanyakazi wa kampuni hiyo kwa kuwapiga kwa kuwa si wakazi wa kijiji husika kauli ambayo ilipingwa na Diwani wa Kata wa Nyarukoba kupitia CHADEMA, Matiko Marwa.
Sehemu ya wananchi wa kijiji cha Msege kilichopo wilayani Tarime mkoani Mara wakisikiliza ufafanuzi uliokuwa unatolewa na Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo pichani).

Marwa mbali na kupongeza kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Wizara ya Madini alimtaka mwekezaji huyo kutii makubaliano kwa kusaini mikataba ili kumaliza mgogoro. Kabla ya kufanya ziara katika machimbo hayo, Naibu Waziri Biteko alikutana na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Glorious Luoga na kuelezwa changamoto mbalimbali zinazoikabili Wilaya hiyo hususan kwenye uchimbaji wa madini.

Luoga alieleza changamoto hizo kuwa ni pamoja na ukusanyaji wa maduhuli kuwa mdogo kutokana na wachimbaji wadogo wengi kuchimba madini pasipo kutambulika, baadhi ya wachimbaji wadogo kuwepo kwenye leseni zenye uwekezaji, utoroshwaji wa mawe yenye dhahabu na migogoro katika baadhi ya maeneo yenye shughuli za uchimbaji madini.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...