Meneja Mradi Legal Services Facility, Ramadhan Masele, akiongea na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba (hawapo pichani) jijini Dodoma.

Na Mwandishi Wetu

Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wameombwa kuunga mkono kazi za wasaidizi wa kisheria na watoa huduma za msaada wa kisheria nchini baada ya huduma zao kuonekana zikiwasaidia mamilioni ya Watanzania kuondokana na vitendo vya kikatili na udhalimu.

“Ni kweli kwamba wasaidizi wa kisheria na watoa huduma za msaada wa kisheria wengine wamekuwa msaada mkubwa kwa makundi mbalimbali ya watu wanaoishi kwenye mazingira magumu na wanaoweza kudhurika, lakini hawawezi kutoa huduma bila ya kusaidiwa kama ambavyo wabunge nao hawawezi kufanya kazi kwa ufanisi bila msaada wa watu wengine,” alisema Ramadhan Masele, ambaye ni meneja wa mpango wa Taasisi ya Msaada wa Kisheria (LSF) wakati wa ufunguzi wa semina ya mafunzo ya siku mbili kwa wabunge juu ya wasaidizi wa kisheria na watoa huduma za kisheria nchini. LSF, ambayo ni shirika lisilo la kiserikali na lisilofanya kazi kwa kupata faida, ilianzishwa mwaka 2011. Shirika hili linafadhiliwa na Wakala wa Kimataifa wa Maendeleo ya Watu wa Denmark (DANIDA) na Idara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Uingereza (DfID) kwa kutoa misaada ya fedha kupitia LSF kwa ajili ya kufadhili mashirika yasiyo ya kiserikali yanayotoa msaada wa kisheria na huduma za wasaidizi wa kisheria Tanzania Bara na Zanzibar.

Meneja Mradi Legal Services Facility, Ramadhan Masele, akiongea na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba jijini Dodoma, LSF imefanya kikao na wabunge wa kamati hiyo ili kujadili namna watakavyoendelea kushirikiana katika kuboresha haki na upatikanaji wa huduma za msaada wa sheria kwa wananchi.

LSF ina lengo la kuwafanya wabunge kujua masuala mbalimbali, ikiwemo namna wasaidizi wa kisheria wanavyotoa huduma, idadi ya wilaya wanamotoa huduma na aina ya kesi wanazozishughulikia, msaada wa kisheria na huduma za wasaidizi wa kisheria, kazi za LSF na ushiriki wake katika kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) 17 ya Umoja wa Mataifa na “ndoto ya muda mrefu ya taifa" ya kupata haki kwa wote Tanzania, nchi ambayo inajenga uchumi wa kati na wa viwanda ifikapo.

Semina hii ya mafunzo inakuja wakati kuna ongezeko la matukio yaliyokwisha ripotiwa ya uvunjaji wa haki za binadamu nchini, kama vile watu kuteswa, ukatili wa kijinsia, udhalilishaji wa kijinsia, kuwashambuliwa wanawake kwa kuwapiga, unyang'anyaji wa ardhi na matukio mengine yanayofanana na hayo.

Kwa kupata ufadhili kutoka LSF, wasaidizi wa kisheria na watoa msaada wa kisheria wamekuwa msitari wa mbele katika kuwasaidia wanawake, wanaume na wasichana maskini na makundi ya watu wengine wanaoishi kwenye mazingira magumu wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali zinazotokana na uvunjwaji wa haki za binadamu—upatikanaji wa haki kwa gharama nafuu au bila gharama yoyote na huduma bora za msaada wa kisheria na hivyo kupata haki zao, kwa mujibu wa meneja mpango wa LSF.
Baadhi ya wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya huduma na maendeleo ya jamii pamoja na wafanyakazi wa Legal Services Facility (LSF) wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumaliza mkutano wenye lengo la kujadili jinsi ya kushirikiana katika kuboresha upatikanaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi.

“Lakini wasaidizi wa kisheria na watoa msaada wa kisheria wengine wangeweza kutoa huduma kwa kuwafikia na kuwasaidia watu wengi zaidi, ambao haki zao zimevunjwa kama wakiungwa mkono na wabunge,” aliongeza Masele, huku akisema kwamba “wanawake na wanaume wanaoteswa, dhalilishwa au kufanyiwa ukatili wa kijinsia, ambao haki zao za ardhi na mirathi zimevunjwa, ni wananchi na wapigakura wa majimbo yanayoongozwa na wabunge wenyewe.”

"Pamoja na mambo mengine, alisema semina ya mafunzo itawasaidia wabunge kufahamu masuala ambayo wasaidizi wa kisheria na watoa huduma za kisheria wengine wanayoshughulika nayo kama vile yale yanayohusu haki za binadamu na elimu ya sheria, huduma za wasaidizi wa kisheria (ikiwemo jinsi wanavyotoa huduma zao), na namna wasaidizi wa kisheria wanavyoweza kushirikiana na wabunge kupanua wigo wa huduma za msaada wa kisheria. Lengo ni kuwasaidia watu wengi wanaohitaji msaada wa kisheria na kuwafanya kuwa katika hali nzuri zaidi kupeleka elimu ya haki za binadamu na sheria kwa wananchi walio katika majimbo yanayoongozwa na wabunge," alisisitiza Masele.

Kwa mujibu wa maelezo ya LSF, semina hii itawawezesha wabunge kufahamu huduma mbalimbali zitolewazo na wasaidizi wa kisheria, ambao kwa sasa wanafanya kazi katika wilaya 170 nchini, kuwasiliana nao, namna ya kupata huduma zao na kueneza taarifa za huduma zao majimboni kwao.

“Taarifa muhimu kama hizi zitasaidia kazi za wabunge na wasaidizi wa kisheria hasa kwa upande wa kutatua migogoro ya ardhi, ndoa na mimba za utotoni, mirathi, wanaume kuacha familia zao nk,” inasema sehemu ya taarifa ya LSF. Mada za kimkakati zilitolewa na wataalamu wa LSF kwenye semina iliyohudhuriwa na wabunge kutoka Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...