Na Veronica Simba – Mara
Wananchi wametakiwa kuondoa hofu kuwa umeme unaosambazwa vijijini kupitia Mradi wa Umeme Vijijini (REA) ni mdogo usioweza kutumika kwa shughuli kubwa za kibiashara kwani si kweli, kwakuwa umeme huo una nguvu sawa na umeme mwingine na unaweza kutumika kwa matumizi yote ikiwemo viwanda.
Hayo yamebainishwa kwa nyakati tofauti na Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, wakati akizungumza na wananchi wa maeneo mbalimbali katika Wilaya za Bunda na Serengeti mkoani Mara, pamoja na Bariadi mkoani Simiyu, Septemba 19, 2018 akiwa katika ziara ya kazi.
Waziri Kalemani alisema kuwa, baadhi ya watu wamekuwa na hofu kuwa huenda umeme huo ambao Serikali inausambaza vijijini  ni mdogo usioweza kuendesha shughuli kubwa za kibiashara zinazohitaji umeme mkubwa.
“Naomba niwahakikishie kwamba, umeme wa REA hautumiki kwa ajili ya kuwashia taa tu, bali ni umeme kama ulivyo umeme mwingine na una uwezo wa kutumika katika shughuli zote hata kuendeshea viwanda vikubwa.”
Akieleza zaidi, Waziri alifafanua kuwa, lengo la Serikali kupeleka umeme vijijini kupitia Mradi wa REA ni kuhakikisha umeme huo mbali na kutumika kwa matumizi madogomadogo ya kawaida, utumike zaidi kwa shughuli za kiuchumi ikiwemo viwanda vidogo na hata vikubwa, ili kuinua kipato cha wananchi na uchumi wa nchi kwa ujumla.
Alisema kuwa, katika kuwezesha uchumi wa viwanda, Serikali imedhamiria viwanda hivyo vianzishwe vijijini ambako ndiko kwenye rasilimali nyingi, na kwamba Serikali inatambua kuwa umeme ndiyo ‘injini’ ya uchumi wa viwanda; hivyo ni lazima upelekwe umeme unaoweza kukidhi matakwa hayo.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (katikati), akikata utepe kuashiria uwashaji rasmi wa umeme katika kijiji cha Bukama, wilayani Bunda, Septemba 19, 2018.
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani akizungumza na wananchi wa kijiji cha Bukama wilayani Bunda, wakati wa hafla ya uwashaji rasmi wa umeme katika eneo hilo iliyofanyika katika Shule ya Msingi Busore, Septemba 19, 2018.
Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mwalimu Lydia Bupilipili akizungumza wakati wa Mkutano wa Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (kushoto) na wananchi wa kijiji cha Salama ‘A’ (hawapo pichani), akiwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (wa pili-kushoto) akipokea fimbo maalum inayoashiria uongozi mahiri kutoka kwa wazee wa kijiji cha Bukama wilayani Bunda; wakati wa hafla ya uwashaji rasmi umeme katika eneo hilo iliyofanyika Septemba 19, 2018. Wa kwanza kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Bunda, Boniphace Getere na wa tatu kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mwalimu Lydia Bupilipili.
Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Nurdin Babu akizungumza, wakati Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (wa kwanza kulia), alipofika ofisini kwake kabla ya kuanza ziara ya kazi wilayani humo kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme. Ziara hiyo ilifanyika Septemba 19, 2018.

KUSOMA ZAIDI BOFYA HAPA

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...