WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametangaza tume ya
kuchunguza ajali ya kivuko cha MV Nyerere yenye wajumbe saba ambayo itaongozwa
na Jenerali mstaafu, George Waitara.
Akitangaza majina hayo kwenye kijiji cha
Bwisya katika kisiwa cha Ukara, wilayani Ukerewe, mkoani Mwanza leo (Jumatatu,
Septemba 24, 2018), Waziri Mkuu amesema wajumbe hao wanapaswa kuikamilisha
kazi hiyo ndani ya mwezi mmoja.
Amewataja wajumbe wengine kuwa ni Mbunge wa
Ukerewe, Bw. Joseph Mkundi, Mhandisi Marcelina Magesa, Wakili Julius Kalolo na
Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Bi. Queen Mlozi.
Wengine ni SACP Camillus Wambura na Mkurugenzi
wa Idara ya Maafa katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Bashiru Taratibu Hussein.Amemwagiza Mkuu wa Majeshi, Jenarali Venance
Mabeyo asimamie uundaji wa tume hiyo na kuainisha ni mahitaji gani yanatakiwa kwa
haraka na pia afuatilie utekelezaji wake.
MV Nyerere ilipinduka na kuzama Septemba 20,
mwaka huu ambapo hadi sasa jumla ya watu 41 wameokolewa na wengine 227
wamepoteza maisha baada ya miili mingine mitatu kupatikana leo asubuhi. Jana
yalifanyika mazishi ya kitaifa ambapo miili tisa ilizikwa kwenye eneo la uwanja
wa shule ya msingi Bwisya. Miili 214 ilitambuliwa na kuchukuliwa na ndugu zao.
Wakati huohuo,
Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza itangazwe zabuni ya
haraka ya kutengeneza kivuko kingine kipya chenye uwezo wa kubeba tani 50 za
mizigo na abiria zaidi ya 200.
“Hili ni agizo la Mheshimiwa Rais, na mimi
ninamuagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe
aitishe zabuni hiyo haraka sana. Kazi hiyo ifanywe mara moja ili kivuko kipya
kiweze kutengenezwa na kusaidia wananchi wa eneo hili kwa haraka,” amesema.
Amesema kivuko kipya kikikamilika, itabidi
kipangiwe ratiba za safari nyingi zaidi badala ya kwenda mara moja kwa siku ili
kuondoka kero ilikuwa ikiwakabili wananchi hao.
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU,
SEPTEMBA 24, 2018.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...