*Asema kuna gari wanaishikilia inayodhaniwa kuhusika katika kutekwa kwake
*Watu nane waendelea kushikiliwa, azungumzia umuhimu wa CCTV Kamera

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

JESHI la Polisi nchini limesema wakati uchunguzi ukiendelea kuhusu kutekwa kwa Mfanyabiashara, Mohamed Dewji 'MO' wamefanikiwa  kuitambua gari inayodhaniwa kuhusika kwenye tukio hilo.

Pia limesema watu nane wanashikiliwa kutokana na tukio hilo ambapo wanaendelea kuhojiwa. Awali Jeshi hilo lilikuwa linawashikilia watu 27 lakini baada ya upelelezi limebaki na hao nane.Akizungumza leo na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro amesema Polisi wanaendelea na upepelezi wa tukio la kutekwa kwa Mfanyabiashara huyo.

Kuhusu gari ambayo inasadikiwa kutumika kwenye tukio hilo IGP Sirro amesema kamera za CCTV zimewasaidia  kutambua gari iliyotumika kumteka Mo Dewji.Ametaja namba za usajili wa  gari hiyo ni AGX 404 MC ambapo amewaeleza waandishi wa habari limetoka nchi jirani na tayari wameshapata taarifa za mtu mwenye umiliki wa gari hilo.

Pia IGP Sirro ametoa rai kwa Watanzania wenye uwezo wa kuwa na silaha na wenye uwezo wa kifedha ni vizuri wakawa na silaha zao kwa ajili ya kujilinda na ni vema hata wasaidizi wao nao wakawa na silaha.

Alipoulizwa kuhusu Mo kuwa hai au laa, IGP amejibu kwamba hana jibu la swali hilo kwa sasa na kuhusu malengo ya watekaji amefafanua watakapopatikana waliohusika wataeleza lengo lao. Ameonya watu wanaotaka kuchafua taswira ya nchi  kwa kufanya tukio hilo na wakipatikana watakiona cha moto.

Kuhusu Jeshi la Polisi kuendelea kuaminika IGP Sirro amewaomba watanzania kuendelea kuwaamini kwani linafanya kazi kubwa na wamefanikiwa kuifanya nchi kuendelea kuwa salama huku akifafanua huko nyuma kulikuwa na matukio mengi lakini Polisi wamedhibiti matukio ya hayo.

"Jeshi la Polisi limefanikiwa kudhibiti matukio mengi ya uhalifu nchini kwetu bila kuomba msaada kutoka nchi nyingine. Kwanini hilo tukio la kutekwa Mo tuombe msaada wa mataifa mengine. Tunao uwezo mkubwa na tumesomea hivyo hatuna mashaka na kazi tunayoifanya na hatuna sababu ya kuomba msaada," amesema IGP Sirro.Amefafanua sababu za kumtaka mtu kuja kusaidia Tanzania kwa ajili ya uchunguzi ni kwa ajili ya nini wakati Jeshi la Polisi liko imara na wamesomea mambo ya upelezi na wanaoweledi wa kutosha.

Kuhusu familia ya Mohammed Dewji amesema kwamba wamekuwa wakiwasiliana na familia hiyo ambayo inalishukuru Jeshi la Polisi kutokana na jitihada zinazofanyika kuhakikisha Mo anapatikana."Ni siku ya tisa leo Jeshi la Polisi halilali kwa ajili ya kumtafuta MO. Kama familia ya MO itakuwa haina imani na Polisi hilo litabaki kuwa la kwao lakini ukweli wanatushukuru sana kwa kazi tunayoifanya," amesema.

Hata hivyo amesema kwa sasa kuna tatizo kwamba kila mtu anataka kuwa mpelelezi na kama kazi hiyo waliipenda wangeanda chuo cha polisi kusomea.
Amesema Jeshi la Polisi linapokea mawazo mazuri yenye kufanikisha kupatikana kwa MO lakini si mawazo yenye mlengo wa kupotosha ambayo kwao hawana nafasi .

Wakati huo huo amesema kumekuwa na kasumba siku hizi hata Mtoto akipotea Kanisani utasikia wanasema ametekwa au  mtu kapotea nyumbani kwake utasikia katekwa lakini ukweli  kuna mazingira ya aina yake.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...