Na Lydia Churi- Mahakama, Mwanza 

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka watumishi wa Mahakama katika wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza hususan Mahakimu kutimiza wajibu wao kikamilifu kwa kuhakikisha wanamaliza kesi ili wananchi waweze kupata haki kwa wakati. 

Akizungumza na Watumishi wa Mahakama ya wilaya ya Nansio-Ukerewe pamoja na Mahakama za Mwanzo za Ilangala na Nansio mjini, Jaji Mkuu pia amewakumbusha Mahakimu kuhakikisha hukumu zinatolewa ndani ya siku 90 baada ya shauri kusikilizwa na endapo siku zitazidi basi zisizidi siku ishirini na moja. 

Alisema Mahakama ya Tanzania inafanya kila jitihada ili kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati huku akitolea mfano wa nakala za hukumu kutolewa bure. Alisema Mahakama imeingia mkataba na shirika la Posta ili kusambaza nakala za hukumu pamoja na nyaraka nyingine za mahakama. 

“Suala la hakimu kuchelewesha hukumu bila sababu za msingi halikubaliki na ni utovu wa nidhamu, jiwekeni kwenye nafasi ya wanaocheleweshewa hukumu ndipo mtaona ni kwa namna gani wanaumizwa na suala hili”, alisema Jaji Mkuu. Awali akizungumza na Kaimu Mkuu wa wilaya ya Ukererwe Bwana Focus Majumbi, Jaji Mkuu alitoa wito kwa viongozi wa serikali kusaidia kuwaelimisha wananchi taratibu za Mahakama ili wapate haki kwa wakati kwa kuwa haki ni kwa mujibu wa Sheria. 

Alisema wananchi wengi hawafahamu taratibu za Mahakama ambapo badala ya kudai haki zao Mahakamani huenda kwa watu wasiohusika na kusababisha haki zao kuchelewa. Naye Kaimu Mkuu wa wilaya ya Ukerewe aliiomba Mahakama ya Tanzania kuanza kuitumia Mahakama ya Mwanzo ya Irugwa ambayo hivi sasa haijaanza kutumika kutokana na ukosefu watumishi. Mkuu huyo wa wilaya pia aliiomba Mahakama kusaidia ili wilaya yake isaidiwe kupata Mwenyekiti wa kudumu wa mabaraza ya kata. 

Jaji Mkuu wa Tanzania anaendelea na ziara yake ya siku nne mkoani Mwanza ambapo atakagua utekelezaji wa shughuli za Mahakama.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwasili katika kisiwa cha Ukerewe kuanza ziara yake ya kukagua shughuli za Mahakama katika Mkoa wa Mwanza. Leo Jaji Mkuu alitembelea Mahakama ya wilaya ya Nansio- Ukerewe, Mahakama za Mwanzo za Nansio mjini na Ilangala pamoja na Ofisi ya Mkuu wa wilaya. Katikati ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza Mhe. Mary Moyo. 

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akielezea kuhusu Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama baada ya kumkabidhi kitabu cha Mpango huo Kaimu Mkuu wa wilaya ya Ukerewe ambaye ni Katibu Tawala wa wilaya (DAS) Bwana Focus Majumbi. 
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Ilangala mara baada ya kuzungumza nao.wakati Jaji Mkuu alipotembelea ofisi ya Mkuu wa wilaya 
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa katika picha ya pamoja na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Pius Msekwa na Mkewe mama Anna Abdalah alipowatembelea nyumbani kwao Nansio Ukerewe. Wa kwanza kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza Mhe. Sam Rumanyika pamoja na watumishi wengine wa Mahakama ya Tanzania. 
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa katika picha ya pamoja na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Pius Msekwa na Mkewe mama Anna Abdalah alipowatembelea nyumbani kwao Nansio Ukerewe 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...