*Yaelezwa kuna madereva wamekimbia na funguo za mabasi kusikojulikana

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

BADALA ya raha sasa karaha!Ndivyo unavyoweza kuuzungumzia usafiri wa mabasi ya mwendo kasi katika Jiji la Dar es Salaam ambapo wananchi wa Jiji hilo wamelalamikia unyanyasaji unaofanywa na watoa huduma wa usafiri huo.

Wakati watumiaji wa usafiri huo wakioneshwa kuchoshwa na usafir inavyoendesha, kwa upande wa uongozi wa DART umedai mradi huo unahujumiwa na baadhi ya watu wasiokuwa na nia njema kwao.

Hata hivyo kutokana na changamoto za usafiri huo leo asubuhi wananchi wa Kimara waliamua kuonesha hisia zao kwa kufunga barabara huku wakidai wamechoshwa na namna ambavyo huduma hiyo inatolewa.Wameiomba Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam kuingilia kati kumaliza changamoto na adha ya usafiri wanayoipata huku wengine wakesema usafiri huo ni mateso kwao.

Wameiambia Michuzi Blog kuwa mabasi hayo yamekuwa yakiwapita watu vituoni na hakuna sababu za msingi za kufanya hivyo na matokeo yake kusababisha watu kujazana na hiyo ni hatari kwani inaweza kusababisha maafa.

WATENDAJI UDART WAJITETEA 

Kwa upande wa Watendaji wanaosimamia Usafiri wa Mabasi ya Mwendo wa haraka(UDART) kupitia Meneja Mawasiliano wao Deus Bugaiywa amesema kinachotokea kwenye mradi huo 
wanahisi kuna hujuma zinazonywa kwa lengo la kukwamisha huduma ya usafiri kwa wananchi.

Amesema kutokana na hali hiyo kwa sasa kuna uchunguzi maalumu unafanywa kwa lengo la kubaini ukweli.Kuhusu kilichotokea leo asubuhi na kusababisha adha kubwa ya usafiri kwa wakazi wa Dar es Salaam na hasa wa Kimara amesema imetokana na kitendo cha madereva wawili kuchukua funguo za mabasi mawili ya mita 18 na kukimbia kusikojulikana."Kawaida mabasi huanza kutolewa saa 10 alfajiri ili kwa ajili ya kuanza kutoa huduma ya kusafirisha wananchi.Lakini leo asubuhi muda huo ulipofika walikuja madereva wawili na kisha kuchukua mabasi mawili na kisha kwenda kuziba njia.
"Baada ya hapo wakakimbia kusikojulikana na wakati wanachukua funguo hizo walikuwa wamevaa makoti marefu na kufunika sura zao.Hivyo bado wanaendelea kufuatiliwa ili kuwabaini na ndio maana tunahisi kuna hujuma zinaendelea,"amesema Bugaiywa.Ameongeza hata madai ya kuwa wamegoma kwasababu ya kutolipwa mshahara nalo halina ukweli kwani wamekuwa wakilipwa mshahara kama kawaida.

MAKONDA KUTINGA KITUO CHA KIMARA 
Wakati huohuo Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda amewaagiza watendaji wote wanaosimamia Usafiri wa Mabasi ya Mwendo wa haraka (UDART) kukutana nae kesho saa 12:30  asubuhi eneo la kituo cha Mabasi (Kimara Bus Terminal) .Makonda amesema lengo anataka kufahamu kwanini hakuna hatua madhubuti walizochukuwa kumaliza kero za wananchi na  hafurahishwi hata kidogo na namna mradi wa mabasi ya mwendo wa haraka unavyoendeshwa.

Amesema hata matarajio ya Rais Dk. John Magufuli yalikuwa ni kuona changamoto ya muda mrefu ya usafiri inageuzwa kuwa historia kupitia mradi huo lakini imekuwa tofauti na matarajio hayo."Hatuwezi kuvumilia kuona wananchi wanateseka wakati Serikali yao ipo kwaajili yao, kesho lazima hili liishe ili wananchi wasafiri pasipo usumbufu kama Serikali yao inavyotaka". amesema Makonda

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...