Na Karama Kenyunko, Glogu ya jamii 
MKURUGENZI wa Fairme NGO, Rene Staheli (62) ambaye pia ni raia wa Uswis leo Oktoba 23, 2018 amehukumiwa kulipa faini ya Sh Sh. Milioni 34 ama kutumikia kifungo cha miaka 20 gerezani baada ya kukiri kosa la kukutwa na vipande vitatu vya meno ya Kiboko. 

 Hukumu hiyo imesomwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Rwizile wa mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Rwizile amesema mahakama imemtia hatiani mshtakiwa kufuatia yeye mwenyewe kukiri kosa lake. 

" Kufuatia kukiri kutenda kosa linalokukabiri na kukubali vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapa, mahakama inakutia hatiani na inakuhukumu kulipa faini ya Sh 34,036,188 na iwapo utashindwa basi utatumikia kifungo cha miaka 20 gerezani", amesema Hakimu Rwizile. 

Kabla ya hukumu hiyo kutolewa, wakili wa serikali Mwandamizi, Patrick Mwita aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa huyo kwa kukutwa na maliasili yetu ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo.
Katika utetezi wake, ameiomba mahakama impe adhabu ndogo kwa kuwa hili ni kosa lake la kwanza, na haijaisumbua mahakama ndio maana amekiri kosa lake na pia ana familia kubwa inayomtegemea huko kwao Uswisi. 

 Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi, mshtakiwa huyo anadaiwa kuwa Oktoba 16, mwaka huu katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Staheli alikamatwa akiwa na nyaraka za Serikali ambazo ni vipande vitatu vya meno ya Kiboko vyenye uzito wa kilogramu tano na thamani ya USD 1,500 ambazo ni sawa na Sh 3, 403, 618.80 mali ya serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania bila ya kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa wanyama pori.
Mkurugenzi wa Fairme NGO, Rene Staheli (62) ambaye pia ni raia wa Uswis leo Oktoba 23.2018 akitoka katika Mhakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kuhukumiwa kulipa faini ya Sh Sh. Milioni 34 ama kutumikia kifungo cha miaka 20 gerezani baada ya kukiri kosa la kukutwa na vipande vitatu vya meno ya Kiboko. 
Hadi MICHUZI BLOG inaondoka katika mahakama ya Kisutu mshtakiwa alikuwa ameshindwa kulipa faini hivyo amepelekwa gerezani kuanza kutumikia kifungo chake.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...