Na: Sylvester Raphael

Taasisi mpya ya Agri Thamani Foundation iliyoanzishwa kwa lengo kuu la kuboresha lishe Mkoani Kagera na kuongeza ushirikishwaji wa wanawake na vijana katika kuongeza Mnyororo wa thamani kwenye Sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi imetiliana saini na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera katika Mkataba wa Makubaliano ili kuanza utekelezaji wa shughuli zake ifikapo Novemba Mosi, 2018.

Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Taasisi ya Agri Thamani Foundation ambaye ni mzawa wa Mkoa wa Kagera Bi Neema Lugangira mara baada ya kutiliana saini kwenye Mkataba wa Makubaliano na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Bw. Nesphory Bwana alisema kuwa aliamua kuanzisha Taasisi hiyo kutokana na Mkoa wa Kagera kuwa na kiwango kikubwa cha watoto wenye udumavu na utapiamlo kutokana na kutopata lishe bora na stahiki.

“Nimeamua nianzishe Taasisi ambayo itausaidia Mkoa wetu wa Kagera hasa kuondoa udumavu kwa watoto kwani ukiangalia haraka utaona kuwa Mkoa wa Kagera kila zao linakubali kustawi lakini watoto hawapati lishe bora jambo ambalo linapelekea kudumaa kwao na mtoto akiwa na udamavu hawezi kuwa na kiwango kizuri cha akili hata kukua kwake kunaathirika.” Alieleza Bi Neema.

Bi Neema alieleza kuwa ili kufanikisha suala la kuondoa udumavu Kagera kwanza ni kuongeza ushiriki wa Wanawake na Vijana katika kuongeza Mnyororo wa Thamani katika Sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambapo alitolea mfano katika kwenye kilimo kuwa Kagera kuna Mazao mengi lakini huenda akina mama hawajui namna bora ya kuongeza mnyororo wa thamani kwenye mazao hayo lakini pia hawajui maana ya kufanya kilimo baishara ili kuingiza kipato na kuongeza ajira kwa vijana.

“Tutajikita katika Kilimo Biashara kwa kuongeza ushiriki wa wanawake na vijana katika kuhakikisha wanaongeza thamani ya mazao mfano mama anayelima viazi lishe afundishwe namna ya kukausha viazi hivyo na kuchanganya na mazao mengine na kutengeneza unga bora wa lishe, kwanza mama huyo watoto wake hawawezi kupata udumavu, pili atakuwa amejua namna bora ya kutunza unga wa viazi lishe badala ya kutunza viazi vyenyewe ambavyo mwisho wa siku vinaharibika.” Alifafanua Bi Neema

Bi Neema anasema kuwa Mkoa wa Kagera umebarikiwa kila zao kukubalika na wananchi wa Kagera wanalima mazao yote, masoko ya mazao hayo yapo lakini tatizo mazao hayo hayalimwi katika mfumo wa kuyaongezea Mnyororo wa Thamani yanapelekwa sokoni hivyo hivyo jambo ambalo linapelekea Mkulima kunyonywa lakini wakulima hanufaiki na mazao hayo kwani watoto wao utawakuta na udumavu kutokana na kutopata lishe bora.
 Bi Neema Rugangira Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Taasisi ya Agri Thamani Foundation na Kaimu  Katibu Tawala Mkoa Bw. Nesphory Bwana Wakipeana Mikono Baada ya Kusaini Mkataba 
 Kabla ya Kusaini Mkataba wa Makubaliano.
 Kaimu  Katibu Tawala Mkoa Bw. Nesphory Bwana  akisaini Mkataba wa Makubaliano Pamoja Bw. Isaya Tendega Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji.
Picha ya Pamoja.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...