Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kusitisha mpango wake wa kurasimisha bandari bubu zilizopo mkoa wa Dar es Salaam

Hayo yameelezwa na Nditiye wakati wa ziara yake Wilayani Bagamoyo ya kukagua bandari bubu zilizopo ambapo amebaini uwepo wa bandari bubu zaidi ya kumi na tisa zinazosafirisha bidhaa kwenye eneo la mwambao wa bahari lililopo wilayani Bagamoyo. 

Amesema kuwa uwepo wa bandari bubu hizo ni kipenyo cha baadhi ya wafanyabiashara kukwepa kulipa kodi kwa kutumia bandari rasmi na hivyo kupunguza mapato ya Serikali na kuihujumu nchi kwa kufifisha jitihada za Serikali za kufikia uchumi wa kati na azma yake ya ujenzi wa viwanda, utoaji wa huduma za afya, elimu, maji, umeme na ujenzi wa miudombinu ya sehemu mbali mbali nchini

Nditiye ameielekeza TPA iache mara moja mpango huo wa kurasimisha bandari bubu zilizopo Mbweni na Temeke kwa kuwa Dar es Salaam ipo bandari na itumike hiyo kwa shughuli za usafirishaji wa bidhaa na abiria. “TPA wafute mara moja mpango wao wa kurasimisha bandari bubu za Mbweni, Temeke kuwa bandari rasmi wakati kuna bandari ya Dar es Salaam,” amesema Nditiye. Pia, ameongeza kuwa fedha zilizotengwa na TPA kwa ajili ya mpango huo lipewe jeshi la bandari ili waweze kununua vifaa kwa ajili ya kufanya doria ya kuimarisha ulinzi kwenye mwambao wa bandari

Amefafanua kuwa yapo majahazi yanayofanya shughuli za usafirishaji ufukweni mwa bahari ya Hindi kwenye mwambao upatao kilomita 300 kwenye eneo la Bagamoyo ambapo majahazi yanashusha mizigo kinyemela. “Nimeshuhudia taratibu za nchi zikikiukwa na kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Bagamoyo inapata changamoto ila inawadhibiti kwa namna moja au nyingine japo yapo majahazi yanayoshusha bidhaa na kuficha kwenye misitu iliyopo ndani ya bahari,” amesema Nditiye.

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa pili kulia) akipata maelezo kuhusu bandari bubu kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Zainabu Kawawa (mwenye koti nyekundu) wakati wa ziara yake ya kukagua bandari bubu hizo wilayani humo. Anayesikiliza ni Msimamizi wa Bandari ya Bagamoyo, Witharo J. Witharo 
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (katikati) akitoa maelekezo kwa Msimamizi wa Bandari ya Bagamoyo, Witharo J. Witharo (wa kwanza kulia) kuhusu kudhibiti bandari bubu zilizopo wilayani Bagamoyo wakati wa ziara yake kwenye bandari hizo 
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akitoa maelekezo kwa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Bagamoyo kuhusu kudhibiti bandari bubu zilizopo wilayani humo wakati wa ziara yake ya kukagua bandari hizo 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...