Serikali imepiga marufuku
Watumishi wa Umma waliohamia Makao Makuu ya Nchi Dodoma kwa gharama za
Serikali kuomba uhamisho wa kurejea jijini Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa jana na Katibu Mkuu,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro
alipokuwa akifanya mahojiano maalum na Shirika la Utangazaji Tanzania
(TBC) kuhusiana na zoezi zima la uhamisho wa watumishi wa umma kutoka
Dar es Salaam kwenda Dodoma.
Dkt. Ndumbaro amesema kuwa, Ofisi
yake imekuwa ikipokea barua mbili au tatu kwa siku za watumishi
waliohamia Dodoma kuomba uhamisho wa kurejea Dar es Salaam kutokana na
sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na za kiafya wakati hospitali ya Rufaa
ya Benjamin Mkapa ina vifaa vya kisasa na uwezo mkubwa wa kutoa huduma
za matibabu kwa watumishi hao.
Dkt. Ndumbaro amefafanua kwamba,
kabla ya watumishi kuhamia Dodoma, Serikali ilitoa maelekezo kwa
waajiri kuwasilisha orodha ya watumishi wenye matatizo ya kimsingi ili
wabaki kwenye vituo vya kazi vilivyopo Dar es Salaam wakiendelea
kutekeleza majukumu yao.
Dkt. Ndumbaro ameongeza kuwa,
baadhi ya watumishi waliohamia Dodoma, wamegeuza uhamisho huo kuwa mradi
wa kuwaingizia kipato kwani mara baada ya kuripoti Dodoma, ndani ya
kipindi kifupi wanaomba uhamisho wa kurejea Dar es Salaam.
Dkt. Ndumbaro amesisitiza
kuwa, kutokana na suala hilo, Serikali imetoa Waraka wa Barua wenye
Kumb. Na. CAC 228/257/01/A/53 wa tarehe 25 Septemba, 2018 kuhusu
Uhamisho wa Watumishi Waliohamia Dodoma Kutekeleza Uamuzi wa Serikali
Kuhamishia Makao Makuu ya Nchi Dodoma ambao unazuia mtumishi
aliyehamishiwa Dodoma kwa gharama za Serikali kuomba uhamisho wa kurejea
Dar es Salaam mpaka atimize miaka mitatu katika kituo cha Dodoma.
Watumishi wa Umma kuhamia Dodoma
ni utekelezaji wa agizo la Serikali lililotolewa na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 25 Julai,
2016 wakati wa maadhimisho ya Kumbukumbu ya Siku ya Mashujaa.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akizungumza katika mahojiano maalum na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ofisini kwake jana jijini Dodoma kuhusiana na zoezi zima la uhamisho wa watumishi wa umma kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...