Na Siti Said
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, amemtaka mkandarasi wa kampuni CGI Contractors Limited anayekarabati barabara ya Dodoma- Morogoro sehemu ya Magubike na Gairo kuhakikisha anakamilisha kazi hiyo mapema ili kupunguza adha ya msongamano wa magari katika eneo hilo.
Agizo hilo amelitoa leo wilayani Gairo mkoani Morogoro akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miundombinu inayosimamiwa na sekta yake katika mikoa ya Dodoma na Morogoro ili kujionea maendeleo yake.

Aidha, Naibu Waziri Kwandikwa amemsisitiza mkandarasi huyo kuchukua tahadhari katika kipindi hiki cha mvua ikiwa ni pamoja na kuhakikisha ujenzi wa barabara hiyo unakuwa imara hususan katika sehemu za miinuko ili kuzuia ajali zinazoweza kutokea katika maeneo hayo. "Hakikisheni mnamaliza haraka ukarabati wa barabara hii, magari hapa yamekuwa mengi na msongamano ni mkubwa, mnachotakiwa kufanya kwa sasa ni kufuatilia taarifa za hali ya hewa ili muweze kukabiliana na mvua na huku mkipanga ratiba zenu kuhakikisha mnakamilisha kazi hii mapema", amesema Naibu Waziri Kwandikwa.

Akiwa njiani kuelekea mkoani Morogoro katika eneo la Kibaigwa (panda mbili) mjini Dodoma, Naibu Waziri Kwandikwa amekagua madaraja yanayojengwa na Wakala wa Barabara ( TANROADS), mkoani humo na kuwapongeza kwa ujenzi wa madaraja hayo ili kudhibiti maji yanayotuama hapo hususan katika kipindi cha mvua na kusababisha kero kwa watumiaji wa barabara hiyo. Ameongeza kuwa kwa mwaka huu wa fedha 2018/ 2019, Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu kuhusu ujenzi wa barabara ya Dodoma - Morogoro kutokana na mahitaji ya barabara hiyo kuonekana kuwa ni makubwa kutokana na ongezeko la watu na magari mara baada ya Serikali kuhamia Dodoma.
 Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akitizama uimara wa kingo mojawapo iliyopo katika moja ya madaraja yanayojengwa eneo la Kibaigwa mjini Dodoma. Madaraja hayo yanajengwa kwa ajili ya kuzuia maji ambayo hutuama na kusababisha mafuriko katika eneo hilo. 
 Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Leonard Chimagu, kuhusu namna ya kuboresha ujenzi wa madaraja yanayojengwa na Wakala huo eneo la Kibaigwa mjini Dodoma.
 Muonekano wa sehemu ya barabara ya Dodoma – Morogoro eneo la Gairo ambalo linakarabatiwa na Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Morogoro.
 Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akikagua moja ya jengo lililopo kwenye mzani mpya wa Dakawa Magereza mkoani Morogoro. Wa Kwanza kulia ni Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Morogoro Mhandisi Dorothy Mtenga. 

KUSOMA ZAIDI BOFYA HAPA

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...