Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu akiteta
jambo na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Bwana Bernard Konga katika
mkutano wa hadhara Halmashauri ya Wilaya ya Nanyamba Mkoani Mtwara wakati wa
uhamasishaji wa wananchi kujiunga na NHIF, kupitia Mpango wa Ushirika Afya.
Na Grace Michael
Wananchi Mkoani Mtwara wametakiwa kufanya uwekezaji kwenye afya zao
kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ili wawe na uhakika wa kupata
huduma za matibabu wakati wowote. Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto, Ummy Mwalimu wakati akizungumza na wananchi katika
Halmashauri ya Mji wa Nanyamba mkoani Mtwara.
Amesema kuwa ili kila mwananchi aweze kuwa na uhakika wa kufanya
shughuli zingine za maendeleo na uwekezaji mwingine lazima awe na
uhakika na afya yake kwa kuwa na uhakika wa kupata matibabu.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu akikagua
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara.
“Nawaomba sana wananchi wa Mtwara wekezeni kwenye eneo la afya
zenu na uwekezaji mzuri ni kuwa na Bima ya Afya kupitia NHIF ili
iwawezeshe kupata huduma zote za matibabu kwa ngazi mbalimbali za
vituo vya kutolea huduma kuanzia ngazi ya Zahanati hadi Hospitali ya
Taifa,” alisema Mhe. Ummy.
Alisema kuwa Serikali imeweka utaratibu mzuri wenye gharama nafuu wa
kupata huduma za matibabu kupitia NHIF, utaratibu ambao unamtaka
mwananchi kujiunga kabla ya kuugua ili aweze kunufaika na huduma za
matibabu wakati wowote anapopatwa na maradhi.
“Wengi wetu hapa mmeuza mazao yenu na mnalipwa fedha nyingi, kati ya
fedha mnazopata hakikisheni mnatenga shilingi 76,800 tu kwa ajili ya
kukata kadi ya bima ya afya ambayo itakusaidia kupata huduma mahali
popote ndani ya nchi kwenye zaidi ya vituo 7000 vilivyosajiliwa na NHIF,”
alisema Mhe. Ummy wakati akizungumza na wananchi wa Nanyamba
Mkoani Mtwara.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu
akimhamasisha mmoja wa akina mama kumwandikisha mtoto wake na mpango wa Toto Afya
Kadi ili awe na uhakika wa kupata matibabu.
Aliwahakikishia wananchi upatikanaji wa huduma za matibabu katika
hospitali zote nchini kutokana na maboresho makubwa yaliyofanyika chini
ya Serikali ya Awamu ya Tano ambayo imeongeza kwa kiasi kikubwa bajeti
ya afya hususan bajeti ya dawa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...