Kwa mujibu wa mtandao wa Statista, mpaka kufikia mwaka 2021 mauzo yatakayotokana na biashara za mtandaoni yatafikia Dola za Kimarekani trilioni 4.88. Kiasi hiko kitakuwa ni maradufu ya sasa ambapo mauzo yaliyopatikana kwa mwaka 2018 ni Dola za Kimarekani trilioni 2.84. 

Hii inaasharia kukua kwa sekta hii pamoja na kutengeneza faida kubwa kwa wauzaji wa bidhaa mbalimbali kwa njia ya mtandao duniani. 

Kasi ya ukuaji wa biashara za mtandaoni inaenda sanjari na maendeleo ya sayansi na teknolojia yanayopelekea tabia za wateja kubadilika kwa kasi. Wateja wa sasa wamekuwa na tabia tofauti ukilinganisha na awali ambapo hakukuwepo na matumizi ya mifumo ya kidigitali.

Mifumo ya kidigitali imebadili kwa kiasi kikubwa tabia za wateja ambapo watoa huduma hawana budi kubadilika ili kuendana nao. Kwa mfano, sasa hivi mtu anaweza kufanya shughuli tofauti akiwa eneo moja. Malipo ya huduma mbalimbali kwa kutumia simu ya mkononi kama vile ada, umeme, visimbuzi, maji, faini, benki, leseni na mengineyo yanawezekana bila ya kwenda moja kwa moja kwenye ofisi za watoa huduma. Pia, mtu anaweza kuwa ofisini akiendelea na shughuli zake lakini akafanya huduma za manunuzi, malazi na hata kuagiza chakula pale pale alipo.

Siku za hivi karibuni biashara nyingi zimekuwa zikikumbwa na changamoto ya kupokea idadi ndogo ya wateja wanaotembelea madukani mwao. Sababu kubwa iliyopelekea hili kutokea ni kutokana na kuibuka kwa sekta ya mtandaoni ambayo huwapatia wateja uwezo wa kupata huduma na bidhaa tofauti kwa urahisi na haraka ndani ya muda mfupi. Hivyo basi, imekuwa ni vigumu kwa wafanyabiashara wasiotaka kubadilika kushindana na mahitaji ya sasa ya wateja.

Tunapouanza mwaka mpya wa 2019, Jumia inawashauri wafanyabiashara kuwa hawana budi kutumia fursa zote za kiteknolojia zinazopatikana kwa sasa ili kukuza biashara zao na kupata faida zaidi. Tanzania kwa sasa ina watumiaji wa simu za mkononi zaidi ya milioni 40, kati yao zaidi ya milioni 23 wanatumia huduma ya intaneti. 

Pongezi kubwa kuendelea kuongezeka kwa uwekezaji kwenye sekta za mitandao ya mawasiliano ya simu, makampuni ya uuzaji wa simu pamoja na watoa huduma wa intaneti kwa kuchochea kwa kiasi kikubwa watanzania wengi kuweza kutumia huduma za simu na intaneti.

Kutokana na upatikanaji wa huduma za intaneti hususani kupitia simu za mkononi miongoni mwa watanzania wengi, kumepelekea shughuli nyingi kufanyika mtandaoni. Asilimia kubwa ya wateja hivi sasa wakihitaji bidhaa au huduma yoyote ni rahisi kwa wao kuingia mtandaoni kupitia simu zao za kiganjani kupata taarifa zaidi kabla ya kufanya maamuzi ya kufanya manunuzi.

Hivyo basi, wafanyabiashara hawana budi kuwa na uwepo wa kutosha mtandaoni. Hapa inamaanisha kuwa na tovuti, kufungua akaunti katika kurasa tofauti za mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Twitter, Instagram, Youtube na hata blogu kama ikiwezekana. 

Uwepo tu mtandaoni hautoshi endapo hakutokuwa na taarifa za kutosha zinazoendana na wakati. Imekuwa ni kasumba kwa wafanyabiashara wengi kuwa na kurasa za mitandao ya kijamii au tovuti lakini taarifa nyingi si sahihi au zimepitwa na wakati. Hivyo, hakikisha kunakuwa na taarifa za kutosha, sahihi na zinazokwenda na wakati ili kujibu maswali yote ya mteja atakayokuwa nayo. 

Kingine ambacho wafanyabiashara wanatakiwa kukizingatia kwa umakini ni kutambua wateja wao wanataka nini. Wateja wengi wa sasa hivi ni werevu na wanakwenda na wakati. Takribani kila mteja anapendelea bidhaa au huduma atakayoiona mtandaoni apalekewe mpaka pale alipo, tena kwa ubora na sifa zilezile kama alivyoziona mtandaoni. Hii itapelekea kujenga imani baina ya mfanyabiashara na mteja kuendelea kununua bidhaa siku zijazo.

Yapo mengi ya kutarajia katika mwaka huu kwa upande wa biashara kwa njia ya mtandaoni, pengine kwa kufanya tathmini ya ndani utakuwa umegundua ni vitu gani zaidi vya kufanya marekebisho. Je, ni kwa upande wa bidhaa? Huduma kwa wateja? Huduma baada ya mauzo? Au pengine namna za malipo wanazopendelea wateja? Ni lazima kuyazingatia yote haya ili kuwa na mwaka wenye mafanikio zaidi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...