Mh. ABDULRABI ALLY YUSUPH(71), ambaye alizaliwa siku ya IJUMAA, alikuwa ni mbunge wa Songea mjini baada ya kushinda ubunge kwenye uchaguzi mkuu wa  mwezi Octoba 1985. 

Haikuwa ajabu kwake kujikita katika ulingo wa siasa kwani alikulia katika mazingira ya siasa ambapo baba yake, marehemu ABDULRABI YUSUPH, alikuwa Katibu wa kwanza wa TANU akifanya kazi kwa karibu kabisa na Mwalimu JK NYERERE. Kwavile, kwa mujibu wa Katiba yetu  mbunge hukaa kipindi cha miaka mitano, Mh. ABDULRABI alitarajia kuhudumu kwenye wadhifa huo wa ubunge hadi mwaka 1990, na ingewapendeza wapiga kura wake angeendelea kwa kipindi kingine.

Hata hivyo, hilo halikutimia kwani alikamatwa siku ya IJUMAA akiwa na nyara za tembo 105 ndani ya gari lake la ubunge aina ya Land rover. Kwa vile Katiba yetu haitoi kinga "immunity"  kwa mbunge atuhumiwapo kwa kosa la jinai,  baada ya upelelezi wa kina, Mh. ABDULRABI akashtakiwa na kufikishwa Mahakamani Kuu, Songea, kwa mara ya kwanza, siku ya IJUMAA.

Kesi yake ilivuta hisia kubwa si tu Songea bali nchi nzima. Wananchi toka maeneo mbalimbali ya Songea walikuwa wakifurika mahakamani kujua kinachojiri kwani kwanza haikuwa kawaida kwa kiongozi mkubwa kama yeye kushtakiwa na pili ilijengeka dhana kuwa majangili wa nyara za tembo ni Wasomali na wananchi wa hali ya chini.

Baada ya upande wa mashtaka na upande wa utetezi kumaliza kutoa ushahidi, Mh. ABDULRABI alitiwa hatiani na Mahakama Kuu tarehe 15 April 1988, siku ya IJUMAA, baada ya mahakama hiyo kuridhika na ushahidi usio na mawaa wa upande wa mashtaka na ikampiga "mvua" 9. Hiki kilikuwa kitu cha ajabu sana kwani wananchi wengi hawakutegemea mbunge kufungwa!. 

Baada ya kutolewa adhabu hiyo na Mahakama Kuu, Mh. ABDULRABI hakuridhika hivyo alikata rufaa kwenye Mahakama ya Rufaa nchini ambayo aliiwasilisha siku ya IJUMAA ambapo aliorodhesha sababu sita. Sababu yake kubwa ilikuwa kwamba- "Hizo nyara sio zake ila yeye alibambwa na nyara hizo  kwavile siku hiyo  "alikuwa ameamua kwenda-front mwenyewe kuwakamata majangili wa nyara za tembo". 

Mahakama ya Rufaa, baada ya kuisikiliza kwa makini rufaa hiyo, ilitoa hukumu tarehe 24 Machi 1989, siku ya IJUMAA. Katika hukumu hiyo, Mahakama hiyo ya juu 'ilimchinjia baharini" Mh. ABDULRABI, huku Mh. ROBERT KISANGA, mmoja wa majaji bora kabisa kuwahi kutokea nchini, akizikejeri sababu hizo 6 za rufaa, kwa niaba ya majaji wenzake, kwa kusema:
"We only wish to say that one needed very unusual courage to swallow such a fantastic story. The six grounds, raised by the appellant in his memorandum to the court, were totally devoid of substance". 

Mahakama hiyo ikaamua kuonesha mfano kwa mahakama zote nchini ambapo si tu haikukubaliana na hoja za Mh. ABDULRABI bali pia iliamua kumuongezea "mvua" toka miaka 9 hadi 12.!!! Mh. ABDULRABI, familia yake, ndugu na marafiki zake hawakuamini maskio yao na kubakia kububujikwa na machozi! Kwa hakika, ilikuwa ni siku ya uchungu mno kwao. 

Mh. ABDULRABI alianza kutumikia kifungo chake cha jela kwenye gereza la Songea. Baadae alihamishiwa gereza la Lilungu, Mtwara, siku ya IJUMAA na baadaye akahamishiwa Ukonga Dar Es Salaam na kisha gereza la Maweni, Tanga.

Kutokana na kipaji chake cha kuzaliwa cha uongozi, Mh. ABDULRABI alikuwa Mnyapala mkuu katika kila gereza alikohamishiwa na pia alikuwa ni Imamu wa kuswalisha waislam wote waliofungwa. Kwa hakika alikuwa ni mtu maarufu sana magereza yote aliyopitia.

Mh. ABDULRABI, akiwa anatumikia kifungo chake hicho, alipatwa na mikasa mingi. Mkasa wa kwanza ulikuwa ni wa kuachwa na mkewe miezi mitano tu baada ya kuanza kutumikia kifungo chake. 

Siku moja akiwa gereza la Lulindi, Mtwara, kiongozi mmoja Mlokole alimfuata na kumwambia amemsilimisha mkewe na kuwa Mlokole na mbaya zaidi akamuoa kabisa! Mh ABDULRABI alihuzunika na kupata uchungu sana kwani  alikuwa amezaa watoto 6 na mke wake huyo wa kwanza, ambapo baadhi ya watoto hao pia wakawa walokole wakati yeye ni "Swala 5"!.

Mkasa mwingine uliomkumba akiwa "lupango" ulitokea siku moja ya IJUMAA alipomsikia kiongozi mmoja wa zamani wa Bunge  la Jamhuri  ya Muungano alipolitangazia Bunge na Taifa kwamba: "aliyekuwa Mbunge wa Songea mjini(CCM) Bw. YUSUPH ALLY ANDULRABI aliyekuwa amefungwa, amefariki". Jambo hili lilimtia simanzi na uchungu usio na mfano na hadi leo haelewi ni kwanini  kiongozi huyo alitangaza hivyo!.

Mkasa mwingine ni pale akiwa "lupango", watoto wake walipotimuliwa shule kwa kukosa mtu wa kuwasomesha. Siku moja, Rais wa awamu ya pili, Mh ALLY HASSAN MWINYI alifanya ziara ya kitaifa huko Songea na akahutubia kwenye uwanja wa Majimaji.  

Huku Rais MWINYI akiendelea kuhutubia, dada yake Mh. ABDULRABI aliamua "kujitoa fahamu" na kwenda karibu kabisa na alipokuwa Mh. Rais MWINYI na akamwangukia miguuni huku akilia kwa uchungu! Kitendo hicho kiliwaudhi mno wanausalama ambao, kufumba na kufumbua, wakawa wamemkwida na kumbeba mzobemzobe hadi nje. 

Hata hivyo, baadae "Mzee Rukhsa", akiwa Ikulu ndogo, aliagiza mwanamke huyo apelekwe ili akatoe dukuduku lake. Alipofika Ikulu ndogo, dada huyo wa Mh. ABDULRABI alimweza "Mzee Rukhsa" kuwa anaishi na watoto 2 wa Mh. ABDULRABI na kwamba yeye ni fukara chokambaya asiye na nyuma wala mbele na kipindi chote alichokaa na watoto hao 2, "hakuna rangi aliyoacha kuiona" hivyo akaomba kusaidiwa. "Mzee Rukhsa", papo hapo, akaagiza CCM iwasomeshe watoto hao waliokuwa wadogo na kweli ikawasomesha hadi kidato cha nne.

Jambo lingine lililomkumba Mh ABDULRABI ni kukimbiwa na viongozi na marafiki zake karibu wote ambao zamani walikuwa wanakunywa wote na kufurahi kwa pamoja. Hili linamsononesha sana. Hii ndio mikasa aliyokumbana nayo.

Mh. ABDULRABI, akiwa anatumikia kifungo chake, alishuhudia na kushiriki kwenye mambo mengi mengine yakiwa si ya kawaida. Mfano mmoja mkubwa ni pale aliposhuhudia, kwa macho yake, kunyongwa kwa wafungwa 11 baada ya Rais MWINYI kutia saini hati zao za kuidhinisha wanyongwe baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya mauaji ya kukusudia na Mahakama Kuu na rufaa zao kutupwa na Mahakama ya Rufaa  . 

Baadhi ya watu wamekuwa wakitoa takwimu potofu kuhusu idadi halisi ya watu walionyongwa nchini toka tupate uhuru. Taarifa rasmi na sahihi ilitolewa bungeni tarehe 30/1/2008 na Mh. MATHIAS MEINRAD CHIKAWE, Naibu Waziri wa Sheria na Katiba wa awamu ya nne kama ifuatavyo:
"Mh Spika, jumla ya watu 82 wamenyongwa kuanzia awamu ya kwanza hadi awamu hii ya nne. Kati ya watu hao, 10 walinyongwa wakati wa awamu ya kwanza na 72 walinyongwa wakati wa awamu ya pili. Hakuna ambaye alinyongwa wakati wa awamu ya tatu na awamu ya nne..."

Mh. ABDULRABI si tu alishuhudia kunyongwa kwa watu hao 11 bali pia yeye alikuwa mmoja wa waliopewa kazi ya kusafisha vitanzi hivyo baada ya adhabu hiyo kutekelezwa.

Mh. Rais MWINYI alimsamehe Mh. ABDULRABI, muda mfupi kabla ya kuacha urais, akitumia mamlaka yake  kwa mujibu wa ibara ya 45 (1)(a) ya Katiba yetu isemayo:
"Rais anaweza kutoa msamaha kwa yeyote aliyepatikana na hatia mbele ya mahakama kwa kosa lolote.."

Mh. ABDULRABI aliachiwa ikiwa imebaki miezi 4 amalize kutumikia kifungo chake. Mh. ABDULRABI hakutumikia miaka yote 12 gerezani kwani kwa mujibu wa Kifungu cha cha 49(1),(2),(3) cha Sheria ya Magereza Sura ya 58 'RE (2002) mfungwa yeyote( isipokuwa aliyehukumiwa kunyongwa au kifungo cha maisha) hupata msamaha wa 1/3 ya kifungo chake. Mh. ABDULRABI alifungwa Aprili 1988 kwa kupatikana na nyara za serikali hivyo ukiondoa 1/3 ya miaka 12 unabaki na miaka 8. Hivyo, angetoka April 1996 kama asingepata msamaha huo wa Mh. Rais MWINYI.   

Mh. ABDULRABI akaachiwa siku ya IJUMAA na kwenda kuishi eneo lijulikanalo kama Mfaranyaki ambako alikuja kuwa Mwenyekiti wa CCM wa Kata hiyo. 

Mh. ABDULRABI, kwa kupata msamaha huo wa Rais, amekuwa mmoja wa wafungwa viongozi/watu maarufu waliopata msamaha wa Rais kwa mujibu wa Katiba. Baadhi ya wengine ni ISMAEL ADEN RAGE (Rais Kikwete), NGUZA VIKING@BABU SEYA na mwanae JOHNSON NGUZA@ PAPII KOCHA (Rais Magufuli), AGNES DORIS LIUNDI (Rais Nyerere) na ASHA MKWIZU (Rais Mwinyi).  

Kama ionekanavyo maeneo mengi ya makala hii hapo juu, siku ya IJUMAA ni ya kipekee sana kwa maisha ya Mh. ABDULRABI na mama yake mzazi aliyefariki mwaka 2011 aliwahi kumsihi amshukuru Mungu kila siku ya Ijumaa kwani ina historia ndefu kwa maisha yake. Cha ajabu hata leo hii makala hii ya kumhusu Mh. ABDULRABI  imeandikwa IJUMAA!!!.  

Mh. ABDULRABI kwa sasa "amefulia" akiishi kwenye nyumba chakavu ya urithi pamoja na wake wawili ambao ni mama ntilie, na watoto kadhaa. Kwavile umri umekimbia,  kwasasa anawategemea mama ntilie hao kwa kila kitu. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...