1. Usuli:
Mnyama SIMBA leo majira ya saa 11 jioni kwa saa za DRC au saa 1 ya usiku kwa Bongo, atashuka dimba la Stade de Martyr, jijini Kinshasa, kupambana na ASSOCIATION SPORTIVE VITA CLUB@ AS VITA CLUB "The Black Dolphins" , mabingwa wa DRC, katika mtanange ambao kocha mwenye uzoefu wa AS VITA, mzee mzima FLORENT IBENGE amesema "lije jua, ije mvua, SIMBA lazma ichezee kichapo"!.

AL AHLY ya Masri ndiyo timu inayoongoza kundi hilo kwa kuwa na pointi 4 baada ya usiku wa jana kwenda sare ya 1-1 ugenini Algeria dhidi ya JS SAOURA. Katika mechi hiyo, Al Ahly, kama kawaida yake ugenini, ilikuwa ikitafuta sare tu na ikawaikipoteza muda mara kwa mara. Js Saoura ilipata bao dk ya 59 na Al Ahly ikasawazisha dk ya 85.

2. AS VITA kama YANGA!!!:

Timu ya AS VITA inatumia rangi 3 zitumiwazo na YANGA yaani njano, kijani na nyeusi na manazi wa timu hiyo huwa na kawaida ya kula mihogo na nyama ya nyani kabla ya mechi ambayo wanaamini inawapa nguvu na huishangilia timu yao mwanzo mwenga hivyo SIMBA ijitayarishe kisaikolojia kukumbana na kelele nyingi sana uwanjani!.

3.  SIMBA Yafikia Hoteli ya DC MOTEMA PEMBE!

SIMBA imefanya figisu baada ya kuwasili Kinshasa alhamis kwa kuamua kufikia hoteli ya Venus, iliyopo nje kidogo ya Kinshasa, ambayo ndiyo hutumiwa na DC MOTEMA PEMBE, wapinzani wakubwa wa AS VITA.


Kitendo hicho kimewakasirisha wapenzi wa AS VITA ambao sasa wameipa chagizo kubwa timu yao kuiangushia kipondo SIMBA kama inavyoifanyaga DC MOTEMA PEMBE!. Jiji la Kinshasa siku ya Ijumaa maongezi yalikuwa ni mechi hii ambapo suala la  matokeo ya uchaguzi liliwekwa kando na kwa hakika leo mtoto hatumwi dukani.!.


4. SIMBA Vs AS VITA 1978:

Hii itakuwa ni mara ya pili kwa SIMBA kupambana na AS VITA katika michuano hiyo.

Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1978 timu hizo zilipopambana katika raundi ya pili ya michuano hii. Katika mechi ya kwanza iliyopigwa 'Shamba la bibi', Dsm, AS VITA ikicheza pungufu kwa takriban muda wote wa mchezo, baada ya mchezaji wao, BAKU MONDELA KAZADI, kulimwa kadi nyekundu dk 10, iliitandika SIMBA kwa bao 1-0.

Kwenye mechi ya marudiano ya kihistoria iliyopigwa jijini Kinshasa, kwenye uwanja unaopigwa mechi ya leo wa Stade de Martyr, unaoingiza mtu 70.000 wenye nyasi bandia,  Mnyama SIMBA alionesha uoga ambao hata "Mwoga-mkongwe" JOSE MOURINHO anasubiri kwani MOURINHO hupaki basi lakini SIMBA siku hiyo jijini Kinshasa ilipaki Basi, Meli na Treni kwa wakati mmoja!.

Hii ni kutokana na timu ya AS VITA kuogopewa sana barani Afrika enzi hizo kwa kuwa na sifa ya kutopoteza mchezo kwenye uwanja huo ambao huitwa Machinjioni . Katika mtanange huo, SIMBA ilielemewa mno kwani ilichezewa robo uwanja( na sio nusu uwanja) na haikuwezi kupiga hata shuti moja kwenye lango la AS VITA kwa dakika zote 90. Ni mchezaji mmoja tu aliyekuwa akijitahidi walau kufika katikati ya uwanja, GEORGE "BEST" KULAGWA. Huyu alikuwa winga hodari wa SIMBA aliyepewa jina la "BEST" kwa kufananishwa na GEORGE BEST, mmoja wa wachezaji hodari kabisa kuwahi kuichezea MAN U.

AS VITA ilikuwa na safu ya ushambuliaji matata sana ya akina LOFOMBO, LOBILO na mkali wao, JEAN ADELARDE MAKU MAYANGA. MAYANGA, aliyeitungua SIMBA mechi ya Dsm, alikuwa mshambuliaji aliyekuwa akiogopewa bara zima la Afrika kwani alikuwa ni mshambuliaji mahiri sana mwenye sifa zote. Mashambulizi "yaliyosukumiwa ndani" ya 18 za SIMBA siku hiyo na washambuliaji hao wenye uchu mkali, hayakuwa ya nchi hiyo!!!.

5. TWINS wapewa majina ya OMAR MAHADHI:

OMAR MAHADHI "BIN JABIR", kipa hodari sana wa Mnyama SIMBA" na "Tanzania One" wa wakati huo, alifanya mambo makubwa sana ya kihistoria na kuwa shujaa wa SIMBA siku.

Katika mechi hiyo, MAHADHI alithibitisha kuwa CAF haikukosea kumchagua katika TIMU YA AFRIKA mwaka 1973 baada ya kumalizika kwa michuano ya "All Africa games" nchini Nigeria. Katika michuano hiyo, MAHADHI na MAULID DILINGA "MEXICO" wa YANGA walichaguliwa baada ya kuonesha uwezo mkubwa sana. Katika michuano hiyo, Taifa Stars ilitoka sare 0-0 na Nigeria A, ikaifunga Nigeria B 2-1, ikazifunga Ghana 1-0 na Togo 1-0. Katika hatua inayofuata, iliyochezwa kwa ligi tena, Taifa stars ilitoka sare 1-1 na Nigeria A, ikatoka sare na Misri 1-1 kabla ya kufungwa na Algeria 2-1 na kuondolewa mashindanoni. DILUNGA alifunga katika karibu kila mechi na kwa hakika YANGA haijawahi kuwa na namba 10 bora kama mtaalam DILUNGA! Uwezo mkubwa wa MAHADHI katika michuano hizo ndio uliopelekea achaguliwe Timu ya Afrika.

Katika mechi dhidi ya AS VITA, beki ya SIMBA ilikuwa ikikatika mara kwa mara na kama si uhodari wa MAHADHI basi SIMBA ingeweka rekodi ya kuwa timu ya Bongo iliyofungwa magoli mengi zaidi nje ya nchi!  Kwa wale waliomuona DAVID DE GEA wa MAN U akiokoa magoli ya wazi dhidi ya TOTTENHAM katika kipindi cha pili, jumapili ya tarehe 13.1.2019, wanapaswa kutambua kuwa MAHADHI yeye alifanya kama alivyofanya DAVID DE GEA  ila MAHADHI alifanya kwa vipindi vyote viwili kwani kila wakati alijikuta yuko uso kwa uso na akina MAYANGA, LOBILO na LOFOMBO!!! Hatimaye, AS VITA wakabahatisha kagoli kamoja kalikofungwa kwa umahiri wa hali ya juu na MAYANGA ambaye baada ya kukusanya kijiji, alijifanya kama anajikuna na kuachia atomic missile iliyogonga besela na kujaa wavuni! SIMBA ikatolewa kwa jumla ya mabao 2-0. Baada tu ya refa kupuliza kipyenga kumaliza mechi hiyo, MAYANGA alimkibilia MAHADHI na kumkumbatia na kumpa hongera kwa uhodari mkubwa aliouonesha!.

SADIQUE MUSIMBWA, mpenzi wa AS VITA, aliyefurahishwa sana na uwezo wa MAHADHI, na ambaye mkewe alijifungua watoto mapacha wa kiume masaa machache baada ya mechi hiyo, aliwapa 'twins' wake majina ya kipa huyo mahiri wa SIMBA ambapo mmoja alimwita OMAR na mwingine MAHADHI.

Magazeti yote ya michezo ya kesho yake jijini Kinshasa yalitamalaki picha za MAHADHI akikumbatiana na MAYANGA na picha za 'twins" hao!

Itapendeza sana iwapo "Twins' hao, ambao sasa wana umri wa miaka 41, wataushuhudia mtanange huo na baadae kuonana  na kupiga picha na viongozi na wachezaji wa SIMBA kama kumbukizi ya mambo makubwa aliyofanya kipa wao katika mtanange huo wa mwaka 1978.

Ili SIMBA isichezee kichapo leo, AISHI MANURA itabidi afanye walau robo ya mambo aliyofanya MAHADHI mwaka 1978!.

6. Mafanikio ya AS VITA:

AS VITA ni timu iliyoshiriki michuano mbalimbali barani Afrika hivyo ina uzoefu mkubwa:

6.1 AS VITA ilikuwa Mabingwa wa Afrika mwaka 1973;

6.2 AS VITA imeingia fainali ya ubingwa wa Afrika 1982 na 2014;

6.3 AS VITA iliingia fainali ya CAF CONFEDERATIONS CUP mwaka jana Disemba 2018 (AS VITA ilifungwa 3-0 na Raja Casablanca ugenini na yenyewe ikaitandika RAJA 3-1 "machinjioni" Stade de Martyr).

7. Mfumo wa AS VITA ni kushambulia tu:

SIMBA LUWALA/LUNYASI lazma itambue kuwa leo inakutana na "Mziki mnene" kwani timu ya AS VITA huwa haina hekaya za abunuwasi wala hadithi za Esopo za kupaki basi wao ni kushambulia tu muda wote ikiwa na wachezaji wenye mbio na stamina ya hali ya juu. Sifa yao kubwa ni upigaji vichwa ambapo 60% ya magoli yao ni ya vichwa hivyo SIMBA isiruhusu kabisa mipira ya faulu, krosi au kona. 

Katika mechi yao dhidi ya AL AHLY nchini Masri, AS VITA ilicheza muda mrefu na wachezaji 10 baada ya mchezaji wao CHARLES KALONJI kutolewa dk 36. AL AHLY, licha ya kuwa na numerical advantage, ilisumbuka sana na ikafanikiwa kupata bao la kulazimisha dk ya 65 na penati ya kimazabe dk ya 79 hivyo kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.

8. Jean Mac Makusu Mundele @ MUNDENDE!!!

Mshambuliaji huyu mahiri wa AS VITA na timu ya taifa ya DRC ndiye kipenzi cha manazi wa AS VITA. Ni mchezaji mwenye umbo dogo lakini mjanja sana na mwenye uwezo mkubwa wa kucheka na nyavu. Yeye "husukumia ndani magoli ya aina zote yaani ya kichwa, mguu wa kulia, mguu wa kushoto na hupenda sana kufunga magoli ya "Tikitaka".

MAKUSU alikuwa mfungaji bora wa pili kwenye CAF Confederations Cup 2018.

9. AS VITA HAIFUNGWAGI NYUMBANI:

Moja ya sifa kubwa ya timu hii ni kutofungika katika uwanja wake wa nyumbani, Stade de Martyr. Hii imepelekea manazi wa DC MOTEMA PEMBE kuwatania AS VITA kwamba walizika nyani 100 wakati wa kujenga uwanja huo( nyani huliwa sana na wacongoman).

9.1 Katika mechi 15 za mzunguko wa kwanza wa ligi ya DRC, AS VITA haijafungwa hata mechi moja uwanja wa nyumbani.

9.2. AS VITA haikufungwa hata mechi moja katika mechi za nyumbani kwenye CAF CONFEDERATIONS CUP 2018.

9.3 AS VITA haijafungwa hata mechi moja nyumbani kwenye hii Champions league msimu huu.


JE, MNYAMA SIMBA "ATATOKA" LEO?

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...