Beki hodari wa zamani wa YANGA na TAIFA STARS, HASSAN "WA MORROCO" GOBBOS amefariki dunia. Moja ya mechi yake aliyong'ara vilivyo ni ile ya mwaka 1972. Katika picha hii, Rais wa Sudan, JAFFAR MOHAMED AL- NIMEIRY anaonekana akisalimiana na wachezaji wa Taifa stars mwaka huo 1972.

Mh. NIMEIRY anaonekana akiongozwa na ABRAHAMAN JUMA, Kapteni wa Dar Es Salaam YOUNG AFRICANS na Timu ya Taifa huku pembeni akiwa ni Mwanamume wa shoka KITWANA MANARA "POPAT" aliyeweka rekodi kwa kuchezea Timu ya Taifa toka 1960 hadi 1976 na wa kwanza ni Chinga-Boy, MOHAMED CHUMA, beki Tatu Bora kuwahi kutokea Bongo! Anaeonekana kwa mbali ni ABDALLAH KIBADEN "KING" wa Simba.

Kipute hicho kilipigwa tarehe 4.7.1972 Shamba la bibi shamrashamra za sikukuu ya Sabasaba.

Jenerali NIMEIRY alimtania Mwalimu- "Ndugu yangu, umefilisika kiasi kwamba hata jezi hamna?. Mwalimu aliumia ila "aliua soo" kwa kusema We subiri, tutawafungeni tu"! Mwalimu baadae alitaka maelezo ya kina ni kwanini fedheha hiyo ilitupata.

Mtanange huo ulichezeshwa na mwamuzi GRATIAN MATOVU na Tanzania ikashinda 3-1. Magoli yakiwa yamefungwa na ABDALLAH KIBADEN "KING" (79) mchezaji aliyekuwa na chenga za maudhi na mfungaji hodari wa magoli. 


Magoli mengine mawili yalifungwa na GIBSON SEMBULI, Mshambuliaji nambari 9 wa kipekee  wa YANGA NA TAIFA STARS. Tanzania haijawahi kuwa na mchezaji mwenye kupiga mashuti makali kama SEMBULI! Makipa walikuwa wakikwepa mashuti yake hasa baada ya kumvunja mikono kipa "MACHAPATI"!! Katika mechi hiyo, SEMBULI alitupia kambani dk ya 65 na 68 ambapo bao lake la pili alifumua GRUNETI toka katikati ya uwanja na mpira kujaa wavuni na kushangiliwa mno!!!



GOBBOS aliyekuwa ndiye mchezaji kipenzi wa kocha wa Timu ya Taifa, Mkorea PAK YUNG TANG kutokana na kuwa msomi na mwepesi kuelewa mafunzo na mbinu, ndiye aliyekuwa nyota wa mchezo huo kwa kuwadhibiti vilivyo washambuliaji wepesi wa Sudan wakiongozwa na DAHIESH.

Fedheha ya aina hiyo ilijirudia tena tarehe 9.10.2010 katika mechi ya Tanzania Vs Morocco "Kwa Mchina"(Sio Shamba la bibi) huku mgeni rasmi akiwa Mh. Rais KIKWETE ambapo CD ya nyimbo za taifa iligoma ikabidi ziimbwe kavukavu na wapenzi wa YANGA kubadili na kuimba MUNGU IBARIKI YANGA-FRIKA badala ya Mungu Ibariki Afrika!!!

Watanzania wengi hawajui ni kwanini Timu ya Taifa ilicheza vifua wazi mwaka 1972 na wengine wametumia fursa hiyo kutunga uongo. Sababu hasa ni hii:

"Jezi za Taifa Stars zilikuwa zimepelekwa kwa Mganga ili ishinde. Siku ya mechi tarehe 4.7.1972, Meneja wa Taifa Stars alimfuata Mganga nyumbani kwake lakini bahati mbaya hakumkuta. Kwakuwa Meneja alikwenda na basi la timu, ilibidi wachezaji watembee kwa miguu toka kambini Hostel ya Jeshi la Wokovu Kurasini. Ndio maana Timu yetu ilicheza vifua wazi siku hiyo na ikawa ni aibu kubwa kwa Taifa"
HASSAN CHABANGA DYAMWALE(Aliyekuwa Meneja wa Uwanja wa Taifa mwaka 1972) kama alivyoeleza tarehe 10.10.2016.

REST IN PEACE HASSAN "WAMOROCCO" GOBBOS !

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...