*Polepole afafanua kwa kina ubora na umuhimu wa sheria mpya,agusia wanaosema Msajili kapewa madaraka makubwa

*Mwenyekiti UVCCM ataka vijana kutoa maoni kuhusu muswada huo, wengine wazungumzia vikosi vya ulinzi

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

WANACHAMA,makada na wapenzi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) akiwamo Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama hicho Humphrey Polepole ameuchambua na kutoa maoni yake kuhusu mchakato wa muswada wa sheria mpya ya vyama vya siasa.

Kwa upande wake Polepole amesema sheria mpya iwapo itapitishwa baada ya watanzania wakiwamo wadau wa vyama viasa kuujadili ni wazi itakuwa na tija kwani kwa sasa kuna mambo mengi ambayo hayaendi sawa na Msajili wa Vyama vya Siasa anakosa nguvu ya kisheria kuchukua hatua.

Akizungumza leo Januari 16 jijini Dar es Salaam Polepole amesema kuna faida nyingi ambazo zitapatikana kwenye sheria mpya ya vyama vya siasa na kwamba sheria mpya itavifanya vyama vya siasa kutekeleza majukumu yake kwa ajili ya watu na sio kukifanya chama cha siasa kuwa mali ya mtu binafsi.

"Tunataka vyama vya siasa ambavyo vitakuwa taasisi kwa ajili ya watu na si kuwa na vyama kwa ajili ya watu.Umma wa watanzania jicho lao katika kuvitazama vyama vya siasa ni Msajili wa Vyama vya Siasa kwani ndio mlezi wao na hivyo sheria mpya itampa uhalali wa kisheria kusimamia vyama hivyo.

" Kwetu CCM tunaunga mkono kipengele hicho kwani lazima Msajili wa Vyama vya Siasa ambayo ni taasisi lakini vyama vingine havitaki na wanatoa upotoshaji mkubwa eti oooo msajili sasa atakuwa kama Mungu mtu iwapo muswada huo utapita na kuwa sheria,"amesema Polepole.

Amefafanua katika sheria ya sasa kuna mambo ambayo yapo lakini hayampi nafasi Msajili wa vyama vya siasa kuchukua hatua.Kwa mfano Msajili kwa sasa anayo nafasi tu ya kukifuta chama cha siasa lakini hana nafasi nyingine,wakati kuna uwezekano angeweza kuwa na uwezo wa kuangalia kosa na kutoa adhabu inayofaa.

"Hivyo wameona ni vema kukatengenezwa sheria ambayo itafanya vyama kuwa bora zaidi na hiyo italeta manufaa kwa umma.Tunataka kuona Msajili anakuwa na nguvu ya kisheria pale chama.kinapokosea hata kwenye matumizi ya fedha za ruzuku awe na uwezo wa kuchukua hatua.

" Kwa CCM inajitajidi kusimamia mambo yake, na ndani ya Chama chetu ukienda kinyume na utaratibu utachukuliwa hatua.Hata kwenye za ruzuku na fedha za Chama tuko sahihi na ukila fedha za CCM utapata tabu sana,"amesema Polepole.

Amefafanua katika baadhi ya vyama vingine hakuna utaratibu mzuri wa kutunza fedha zake,hivyo inahitajika sheria ambayo itakuwa na jicho la upole lakini wakati huo huo kuwe na kali kwa mambo ya hovyo.

Amesema sheria hiyo ni nzuri na sio mbaya kama wanavyosema baadhi ya watu na kwba ametaka ifahamike kuwa ofisi ya msajili wa vyama vya siasa ni taasisi na si mtu."Sheria ya sasa inatamka Msajili wa vyama vya siasa atasimamia vyama vya siasa bila kusema anasimamia mambo gani na ndio maana kwetu tunaona umuhimu wa kisheria ambao yale ambayo anayasimamia yawepo kisheria kwa kuandikwa,"

Kuhusu baadhi ya majukumu ambayo Msajili atatakiwa kuzisimamia ni Msajili atahusika kusajili vyama, atasimamia shughuli za uchaguzi ndani ya vyama na hilo ni jambo nzuri kwani kuna vyama ambayo havizingatii uchaguzi.

Polepole amesema kuna vyama Mwenyekiti wa Chama ndio mwenye kuamua nani awe Viti Maalum na asipoongea vizuri na Mwenyekiti basi viti maalum atasikia kwenye bomba."Kwa CCM tunajitahidi kusimamia chaguzi za ndani kwa kufuata utaratibu.Hivyo kipengele cha Msajili kuwa na nguvu kisheria kufuatilia chaguzi za ndani ni jambo nzuri na tunaunga mkono.
Pia kupitia sheria mpya Msajili anatakiwa kuhakiki fedha za vyama ambazo zinatolewa na Serikali, lakini wengine wanasema huko ni kuingilia haki za chama," amesema.

Ameongeza kuwa kna vyama ambavyo Mwenyekiti anadai amekopesha chama na huu ni mwaka wa 17 anadai tu, watu wanaogopa kuhoji kwani wakihoji wanachukuliwa hatua lakini sasa Msajili ataweza kuhoji matumizi ya fedha za ruzuku ambavyo zinatumika kwa vyama vyote na hilo ni jambo nzuri kwani fedha hizo ni za umma.

Pia amezungumzia kipengele ambacho kinazungumzia utolewaji wa elimu ya uraia kwa vyama vya siasa,na msajili atakuwa msimamizi wa elimu hiyo inayotolewa."Msajili atakuwa na nafasi ya kujua hiyo elimu ambayo inatolewa ni kweli ni ya uraia maana kuna vyama vinahubiri mambo ambayo ukiyaangalia kwa kina hayana nia njema,"

Kuhusu Msajili wa vyama vya siasa kupewa madaraka makubwa katika sheria mpya na anakuwa kama Mungu mtu ,ambapo amejibu sio kweli kwani sheria mpya yote ambayo yatasimamiwa na Msajili yatakuwa kwa mujibu wa sheria.Amefafanua sheria ya sasa ilikuwa inampa nafasi Msajili kufuta vyama vya siasa lakini mchakato wa kumuwezesha kufuta ndio ilikuwa haijafikiwa.

"Kwa sasa Msajili wa Vyama vya Siasa kwenye sheria mpya atakuwa na uwezo wa kutoa onyo,kuelekeza na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria inavyotaka kama ambavyo imeandikwa." Vyama vinakosea lakini Msajili sio kosa basi ni kufuta chama atakuwa na nafasi ya kuonya kwanza na kuchukua hatua mbalimbali kabla ya kuchukua hatua,"amefafanua.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Hery James amesema muswada huo wa sheria ya vyama vya siasa umekuja wakati sahihi na kuomba vijana kutoa maoni yao kwani sheria inayotumika sasa ilipitishwa miaka 10 iliyopita.

Amewataka vijana kutumia akili zao kutoa maoni yao kuhusu muswada na kwamba kwa namna ambavyo yeye ameuchambua kuna faida nyingi lakini kwa kuwa muswada huo umeandikwa na binadamu na ndio maana unajadiliwa ili kuuboresha na baada ya kuwa sheria iwe na tija.

Ametumia nafasi hiyo kuonesha mashaka na kipengele ambacho kinazungumzia kuwa mtu anapotaka kuanzisha Chama cha siasa bas wazazi wake wafuatiliwe uraia wao kama ni wa Tanzania au laa ambapo anaona eneo hilo libaki tu anayetaka kuanzisha chama ndio anayetakiwa kuangaliwa uraia wake.

Wakati huo huo wana-CCM wengine wameupongeza muswada huo kwani umekidhi mahitaji hasa kuhakikisha vyama vya siasa nchini kufanya kazi zake za siasa kwa misingi iliyopo.Hata hivyo kuna baadhi ya maeneo ambayo wametoa maoni yao ambapo baadhi yao wamesema katika eneo la kuondoa kikosi cha usalama cha aina yoyote ni vema kikaangaliwa upya.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...