1. Usuli:

Ijumaa ya tarehe 28.12.1945, Vita Kuu ya pili ya dunia ikiwa ndio inamalizika duniani, Mwalimu MATHEW DOUGLAS RAMADHAN na mkewe, Mwalimu BRIDGET ANA CONSTANCE MASOUD, wakazi wa Kisima-Majongoo, Zanzibar walibarikiwa kupata mtoto wa kiume buheri wa afya, AUGUSTINO STEPHEN LAWRANCE RAMADHANI. Mtoto huyu alikuwa ni mtoto wao wa pili kuzaliwa kati ya watoto wao nane ambapo wavulana walikuwa ni wanne na wasichana wanne pia.

Ingawa familia hii ina majina mchanganyiko ya dini ya kiislam na kikristo lakini familia hii ni ya kikristo, madhehebu ya Anglikana.

2. Kuhamia Mpwapwa:

Mwezi April mwaka 1952, Mwalimu MATHEW DOUGLAS RAMADHANI alihamishiwa Mpwapwa, Idodomia kwenda kufundisha, akiwa na familia yake huku AUGUSTINO akiwa na miaka saba.

3. Elimu:

3.1 Elimu ya Msingi:

AUGUSTINO alisoma shule ya msingi Mpwapwa kuanzia mwaka 1952 hadi 1953.

Baba yake akahamishiwa mkoa wa Tabora hivyo AUGUSTINO akasoma "Town school" darasa la tatu na la nne mwaka 1954 hadi 1956.

Mwaka 1957 hadi 1958 AUGUSTINO alisoma shule ya "Kaze Hill" (sasa Itetemia).

Mwaka 1959, Mwalimu MATHEW DOUGLAS RAMADHANI alirudishwa Mpwapwa baada ya kupandishwa cheo na kuwa "Headmaster" hivyo AUGUSTINO alimalizia elimu yake ya msingi Mpwapwa.

3.2 Elimu ya Sekondari:

Baada ya kufaulu vizuri masomo yake ya shule ya msingi, AUGUSTINO alichaguliwa kujiunga na shule maarufu iliyokuwa ikitayarisha vijana wa Tanganyika kuja kushika uongozi wa nchi, "Tabora Boyz" kuanzia mwaka 1960 hadi kumaliza kidato cha sita mwaka 1965. Akiwa shuleni hapo alijifunza mambo mengi ikiwemo kupiga piano ambapo pia alirithi kipaji cha babu yake ambaye pia alirithi jina lake, AUGUSTINO RAMADHANI. Aidha, alijifunza "basketball" aliyoimudu sana kutokana na wajihi wake kwani "amekwenda hewani".

4. Baba yake kufariki katika ajali ya treni UK:

Tarehe 1.3.1961, AUGUSTINO, akiwa kijana mdogo wa miaka 15 na mwanafunzi wa "Tabora Boyz", alipata pigo kubwa kuliko yote katika maisha yake baada ya baba yake, Mwalimu MATHEW DOUGLAS RAMADHANI, aliyezaliwa Zanzibar tarehe 11.9.1951,  akiwa masomoni nchini Uingereza kufariki katika ajali ya treni katika kituo cha Guidebridge Ashton Under-Lyne. Inadaiwa kifo chake kilichagizwa na ubaguzi wa rangi ambao ulikuwa umetamalaki vilivyo nchini Uingereza wakati huo ambapo inadaiwa alisukumwa na kukanyagwa na treni na akazikwa Southern graveyard, UK. AUGUSTINO, licha ya uchungu mkubwa wa kufiwa na mzazi wake huyo aliyekuwa wa kupigiwa mfano kwa maadili, akili na utanashati,  aliingiwa na hofu kubwa kuwa huo ndio ungekuwa mwisho wake kusoma kwa kukosa mtu wa kumlipia ada. Hata hivyo, aliweza kusoma na si tu kumaliza kidato cha sita bali pia kufaulu kwa kiwango cha juu.

5. Kujiunga na Chuo Kikuu:

AUGUSTINO alijiunga na Chuo Kikuu kusomea fani ya sheria, akiwa ni mmoja wa watanzania wa mwanzomwanzo kusomea fani hii ya kipekee.

6. "Kufyekelewa mbali" na Rais NYERERE

Mwaka 1966 kulitokea  mgomo wa kwanza mkubwa katika historia ya chuo hicho. Wanafunzi walikuwa wakipinga masharti ya kujiunga kwa lazma na JKT. Ingawa kuna baadhi ya wanafunzi hawakushiriki mgomo huo akiwemo AUGUSTINO, Rais NYERERE aligadhabishwa mno na kitendo hicho kisicho cha kizalendo hivyo "kuwafukuzilia mbali" wanafunzi wote. Wanafunzi hao, hata hivyo, walirejeshwa chuoni hapo mwezi Julai, 1967.

7. Kukata kadi ya TANU:

AUGUSTINO alikata kadi ya TANU na akawa mwanachama wa "TANU Youth League", akiwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu, mwaka 1969 katika tawi la Temeke.

8. Kumaliza Chuo Kikuu

AUGUSTINO alimaliza elimu ya Chuo Kikuu mwaka 1970 na kufaulu vizuri.

9. Kujiunga na JWTZ

Mwezi Machi 1970, baada ya kumaliza Chuo Kikuu, AUGUSTINO alijiunga na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

10. Kuoa

Licha ya kuwa mkristo, AUGUSTINO alimuoa laaziz wake, Bi. SAADA MBAROUK, ambaye ni mwislam, tarehe 1.11.1975.

11. Kuteuliwa Naibu Mwanasheria Mkuu ZNZ:

Mwaka 1978 ulikuwa ni mwaka wa mafanikio makubwa kwa AUGUSTINO.

Mwanzoni mwaka 1978, Rais wa pili wa Zanzibar, Alhaj ABDOU JUMBE MWINYI, alimteua kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, kikiwa ni moja ya vyeo vya juu kisiwani humo.

Mwaka huohuo wa 1978, AUGUSTINO alipata shahada ya uzamili ya Udsm, katika Sheria za Kimataifa.

12. Kurudishwa JWTZ

Mwezi Machi 1979, Mh. AUGUSTINO alirudishwa JWTZ na katika vita ya Kagera iliyorindima mwaka huo alipelekwa vitani ambako jukumu lake kubwa lilikuwa kuendesha mahakama za kijeshi.

13. Kuteuliwa  Jaji Mkuu ZNZ:

Mwezi Januari 1980, Mh. AUGUSTINO aliapishwa kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar, akiwa Luteni Kanali. Alihudumu cheo hicho hadi mwaka 1989.

14. Kuteuliwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa TZ

Tarehe 23.6.1989, Rais wa awamu ya pili wa Jamhuri ya Muungano wa TZ, Alhaj ALI HASSAN MWINYI "Mzee Rukhsa" alimteua Mh. AUGUSTINO kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa Tanzania.

15. Kujiondoa Uanachama wa CCM

Mh. AUGUSTINO alijiondoa uanachama wa CCM mwaka 1992 baada ya mabadiliko ya Katiba ya nchi yaliyokataza majaji na wanajeshi kuwa wanachama wa vyama vya siasa.

16. Kuteuliwa M/Mwenyekiti NEC

Mwaka 1993, Rais MWINYI alimteua Mh. AUGUSTINO kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Alihudumu kwenye cheo hicho hadi mwaka 2003.

17. Kustaafu Uanajeshi

Mwaka 1997,  Mh. AUGUSTINO alistaafu rasmi JWTZ akiwa na cheo cha Brigedia Jenerali na kuagwa kwa heshma zote za kijeshi katika hafla ya kukata na shoka.

18. Kuteuliwa Jaji wa Mahakama ya Afrika Mashariki

Mh. AUGUSTINO aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Afrika Mashariki mwezi Novemba, 2001 na kuhudumu hadi mwaka 2007.

19. Kuteuliwa M/Mwenyekiti ZEC

Mh. AUGUSTINO aliteuliwa Makamu wa Mwenyekiti Tume ya Uchaguzi, Zanzibar (ZEC) mwaka 2002 hadi 2007.

20. Kusomea Uchungaji:

Mh. AUGUSTINO alisomea uchungaji Chuo Kikuu cha London nchini Uingereza ambapo mwaka 2004 alipata shahada ya uchungaji ( a Bachelor of Divinity).

21. Kuteuliwa Jaji Mkuu wa TZ

Mh. AUGUSTINO alipata heshma ya kipekee alipoteuliwa na Rais KIKWETE kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania mwaka 2007 na akahudumu kwenye cheo hicho hadi tarehe 27.12. 2010 baada ya kufikisha miaka 65, ambao ni muda wa kustaafa kwa lazima kwa mujibu wa Katiba ya nchi.

22. Kuteuliwa Jaji wa Mahakama ya Afrika

Mwaka 2010, Mh. AUGUSTINO aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu.

23. Kurejea CCM

Mh. AUGUSTINO, baada ya kustaafu, alirejea uanachama wa CCM mwezi Septemba 2011 katika Tawi la CCM, Oysterbay.

24. Kutunukiwa Tuzo Maalum na Balozi wa Marekani

Tarehe 23.2. 2012, Mh. AUGUSTINO alitunukiwa Tuzo Maalum "Dr. Martin Luther King Award" na Balozi wa Marekani, Mh. ALFONSO LENHARDT kutonaka na utumishi wake uliotukuka na hivyo kuwa Mbongo wa 13 kupokea Tuzo hiyo mujarab.

25. Kuteuliwa M/Mwenyekiti Tume ya Katiba

Tarehe 7.4.2012, Rais KIKWETE alimteua Mh. AUGUSTINO kuwa Makamu Mwenyekiti Tume ya Katiba ambapo alitoa mchango mkubwa.

26. Kusimikwa MCHUNGAJI

Tarehe 28.12.2013, Mh. Jaji AUGUSTINO alitawazwa kuwa Mchungaji wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Zanzibar baada ya kuwa Shemasi kwa miezi sita. Mchungaji AUGUSTINO alitawazwa katika kanisa la Anglikana lililopo minara miwili, Unguja.

27 Kuteuliwa RAIS wa Mahakama ya Afrika:

Tarehe 14.9.2014, Mh. AUGUSTINO alichaguliwa Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu baada ya kuonesha uwezo mkubwa akiwa jaji wa kawaida wa mahakama hiyo ambapo katika uchaguzi alipata kura 9 na hivyo "kumtimulia vumbi" mpinzani wake aliyeambulia kura kiduchu, nne tu! Mh. AUGUSTINO alihudumu katika cheo hicho hadi alipomaliza ngwe yake jumapili ya tarehe 3.9.2016.

28. Rais JK Amtunuku Nishani

Tarehe 9.12.2014, katika maadhimisho ya miaka 53 ya uhuru wa Tanganyika, Rais wa awamu ya nne, Dr. JAKAYA MRISHO KIKWETE, alimtunuku Mh. AUGUSTINO Nishani Maalumu ya utumishi uliotukuka.

29. "Kuingia-"fronti" kinyang'anyiro cha Urais

Mh. AUGUSTINO, aliushangaza umma, tarehe 15.6.2015 pale jijini Idodomia alipochukua fomu ya kugombea urais kupitia CCM na kuwa mmoja wa wagombea 42. Hata hivyo, tarehe 11 Julai 2015 "alichinjiwa baharini" na Kamati Kuu ya CCM iliyochuja majina hayo na kuibuka na majina matano tu ya Dr. ASHA ROSE MIGIRO, Mh. JANUARI YUSUPH MAKAMBA, Mh. BERNAD KAMILIUS MEMBE, Mh. AMINA SALUM ALI na DR. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI aliyeibuka kidedea.

30. Rekodi zake Kuntu za Kipekee

30.1 Mbongo pekee kuwa Jaji Mkuu Zanzibar na Tanzania;

30.2 Mbongo wa kwanza kuwa Jaji wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu;

30.3 Mbongo pekee kuwahi kuwa Rais wa Mahamaka ya Afrika ya Haki za Binadamu;

30.4 Mbongo pekee kuwa Jaji Mkuu kisha Mchungaji;

30.5 Mbongo pekee kuwa Jaji Mkuu na Brigedia Jenerali;

30.6 Mbongo pekee aliyejaliwa talanta nyingi kwenye tasnia tofauti (Jurist, Basketballer, Pianist, Army officer & Pastor). Mchungaji AUGUSTINO aliwahi kuwa Mwenyekiti wa " Tanzania Basketball Association". 

Mwisho

Huyu ndiye Mh. Mchungaji AUGUSTINO STEPHEN LAWRENCE RAMADHANI ambaye mkewe, Bi. SAADA MBAROUK RAMADHANI ni mwislamu aliyekuwa Luteni Kanali kabla ya kustaafu. Mchungaji AUGUSTINO ana watoto wanne ambapo wawili ni wavulana(FRANCIS & MATHEW) na wawili ni wasichana (MARINA & BRIDGET). 

Kwa hakika, Mchungaji AUGUSTINO ana historia ya kuvutia na ya kipekee!







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Sifikiri kama bado tupo wengi ambao walifundishwa na hayati mwalimu Mathew Ramadhani. Nilikuwa mwanafunzi wake na alikuwa anipenda sana kwani huko Tabora alijuwa kuwa asili ya familia yangu yatokea Zanzibar.Alikuwa na style yake ya kipekee katika mahusiano yake na wanafunzi wake.He invited debate and free speech. He would ask a student to go infront of the class and *teach* while he sat on that students desk. I was very sad when I heard of his death, six years after it happened. Mungu amlaze mahali pema

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...