Na Moshy Kiyungi,Dar es Salaam.

Muziki wa dansi umeshika nafasi kubwa katika burudani katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Kongo Brazzaville.

Watu wa nchi hizo wanaongea lugha moja ya Lingala pia wamepakana. Aidha sehemu ya mipaka yao imetenganishwa na mto Kongo.

Katika makala hii inaizungumzia bendi ya Extra Musica, iliyoko Kongo Brazzaville.

Bendi hiyo ilianzishwa mwaka 1993 jijini Brazzaville, ikiasisiwa na wanamuziki akina Ibabi Okambi Rogatien ‘Roga Roga’, ambaye ni mahiri kwa kulicharaza gitaa la solo. Aidha Roga Roga ndiye kiongozi wa kundi hilo hadi sasa. Muasisi mwingine ni Espe Bass, ambaye ni muungurumishaji wa gitaa la besi.

Mwaka 1995, wanamuziki wa bendi hiyo waliachia albamu yao ya kwanza ya Nouveaux Missiles, iliyowatambulisha vyema kwenye ulimwengu wa muziki.

Albamu hiyo ilipambwa na nyimbo nyingi kali hususani ule Fred Nelson. Wanamuziki walioshiriki kwenye albamu hiyo mbali na Roga Roga na Espe Bass, ni pamoja na Guy Guy Fall, Quentin Moyascko, Oxygen Mbon Slyvain, Dou Dou Copa ‘Elenga Laka Bienvenu’, Dominique, Christian na Herman Nagasaki ambao wote ni waimbaji pamoja na kunengua.

Wanamuziki wengine walikuwa akina Killa Mbongo aliyekuwa ‘rapa’, Durell Loemba, ambaye ni mcharazaji wa gitaa la rhythm, kwa upande wa uchanganyaji drums, yupo Ngolali G’Ramatoulaye na Christian Kingstall alikuwa anabofya kinanda.

Wanamziki wa bendi hii ya Extra Musica walijizolea sifa lukuki, wakapendwa na wapenzi wengi kwa jinsi walivyo wajuzi katika kulishabulia jukwaa wakinengua katika maonesho yao yote ikiwahusisha wanamuziki wenyewe kunengua, tofauti na bendi nyingine ambazo hutumia wanenguaji wa kike.

Ndiyo sababu wao walipenda kujiita wao ni ‘La Difference’ (wa tofauti).
Kwenye albamu hiyo ya kwanza, kulikuwa na wanamuziki wengine ambao hawakupata nafasi ya kurekodi wakiwemo akina Pinochet Thierry, Regis Touba, Cyrille Molanga na Arnaud Luguna.

Albamu hiyo ya Nouvoeaux Missiles, ilisababisha wanamuziki wengine nje ya bendi yao kuvutiwa nayo mmojawapo alikuwa ni Samba Brice ‘Abillissi’, aliyeamua kujiunga nao.

Albamu ya pili ya Confirmation ya mwaka 1996, ilipelekea kundi hilo kuzidi kutikisa vilizvyo hadi wakapata mialiko mingi barani Afrika na Ulaya.
Yaelezwa kuwa albamu hiyo ya Confirmation iliuza nakala nyingi mno kuzidi ile ya mwanzo.

Lakini mafanikio hayo yalisababisha kuzuka kwa mgogoro mkubwa wa kimasilahi. Hali iliyofanya baadhi ya wanamuziki wake wakiwamo akina Christian na Guy Guy Fall, kujiondoa kundini japokuwa kuondoka kwa wanamuziki hao, Extra Musica iliendelea kuwa imara.

Ilipotoka albamu ya tatu ya Ouragan mwaka 1997, wanamuziki Herman Nagassaki na Samba Brice ‘Abilliss’, waliziba vilivyo mapengo ya Guy Guy Fall na Christian .

Mgogoro wa chini kwa chini ulikuwa ukifukuta miongoni mwa wanamuziki wa bendi hiyo na uongozi.Baadhi ya wanamuziki walishindwa kuvumilia wakaihama bendi hiyo.Wanamziki hao walikuwa ni Arnaud Laguna, Quentin Mayascko, Durell Loemba, Cyrille Malonga, Regis Touba na Pinochet Thierry.

Wakaenda kuunda kundi lao jingine walilolipa majina ya Z.I. International, chini ya uongozi wa Cyrille Malonga, Regis Touba, Pinochet Thierry na Durrell Loemba.

Baada ya bendi ya Extra Musica kukimbiwa na wanamuziki hao, walikaa chini na kuamua kuwatafuta wanamuziki wengine vijana wenye vipaji vikubwa.

Walifanikiwa kuwapata vijana hao akina Gildas Pozzi, na Emery Mboma. Wakati huohuo Sonor alichukua nafasi ya ucharazaji wa gitaa la rhythm, lilokuwa likishikwa na Durell Loemba.

Mara baada ya kuwaingiza vijana hao kundini, mwaka 1998 waliachia albam yao ya nne ya Extra Major.Albamu hiyo ilivunja rekodi ya mauzo ya albamu zote za awali na kuwaletea tuzo nyingi barani Afrika, ikiwemo ya Kora kwa kuteuliwa kuwa bendi bora ya muziki kwa bara la Afrika.

Mwaka uliofuatia waliachia albamu nyingine tano zilizokuwa kali mno.
Kati ya albamu hizo ile ya Shalai ilisababisha kuwapata wanamuziki wengine wakali akina Papy Batin Maboulango na Boudouin Massipi.

Rapa wao wa kutumainiwa Killa Mbango, alijitoa kundini akaachana na muziki. Lakini baadaye alirejea tena kundini.Extra Musica ilichukuam kipindi kirefu kutoa albamu ya sita ya Trop C’Est Trop ya mwaka 2001.

Rapa mwingine alijulikana kwa jina la Arafat, nae alijiunga na bendi hiyo, akichukua nafasi iliyoachwa wazi kwa mara nyingine tena na Killa Mbongo.
Baada ya kutoka na albamu hiyo, waliamua kubadilisha kidogo majina ya bendi yao ikaitwa Extra Misica Zagul.

Mara baada ya kutoa albamu ya saba ya Obligatoire mwaka 2004, mwimbaji wao Dou Dou Copa naye akajiondoa kundini akafuatiwa na Oxygene mwaka 2005.Kuodoka kwa wanamuziki hao hakukuithiri Extra Musica Zagul, kwani waliachia albamu ya nane ya La Main Noire mwaka 2006 na nyingine ya tisa ya Sorcellirie ‘Kindoki’ ya mwaka 2011.

Pamoja na kukimbiwa na vijana wake wengi, kiongozi wao Roga Roga, bado anaendelea kuamsha muziki mkali akiwa na vijana wengine wenye vipaji vikali.Hili ndilo kundi la Etra Muzica Zagul kutoka Kongo Brazzaville, japo sasa kuna makundi mengine kadhaa yamezaliwa kutokea ndani ya bendi hiyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...