Idara ya Uhamiaji Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Uhamiaji la Kimataifa (IOM) limeanza kutoa mafunzo ya Ushirikishwaji wa Wananchi katika Ulinzi na Usimamizi wa Mipaka katika Kijiji cha Horohoro, mpakani mwa Tanzania na Kenya kwa siku tatu kuanzia leo tarehe 13-15 Machi, 2019.

Warsha hiyo ya Mafunzo ambayo imefunguliwa na Mkuu wa Wilaya ya Mkinga Mhe. Yona Maki, inashirikisha wananchi waishio mpakani wenye ushawishi katika jamii pamoja na viongozi wa dini, wakulima, mgambo, viongozi wa vijiji na waendesha bodaboda.

Awali akifungua warsha hii, Mkuu wa Wilaya ya Mkinga aliipongeza Idara ya Uhamiaji kwa kuamua kutoa mafunzo yenye lengo la kuwashirikisha wananchi wa kawaida katika suala zima la ulinzi na usimamizi wa mipaka.

“Kwanza niwashukuru sana Idara ya Uhamiaji pamoja na watu wa IOM kwa kuamua kutoa mafunzo kwa wananchi wa kawaida. Ninaamini baada ya mafunzo haya, washiriki kwa kuwa ni watu wenye ushawishi katika jamii ya vijiji vya kata hii, watasaidia sana kufikisha ujumbe. Naona kuna viongozi wa bodaboda, hawa bodaboda ndio wanaosafirisha watu, miongoni mwa watu hao kuna wahamiaji haramu pia, naamini wakipewa elimu basi hawa bodaboda watakuwa ni sehemu muhimu katika Ulinzi na Usimamizi wa mipaka yetu”.

Mkuu huyo wa Wilaya alieleza kuwa Baba wa Taifa aliwahi kusema kuwa jukumu la ulinzi wa Taifa ni letu sote na hasa wazalendo. Hivyo jukumu hili la ulinzi si la vyombo vya ulinzi na usalama pekee, bali ni la kila Mtanzania.

Wakati akitoa taarifa kwa Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Afisa Uhamiaji Wilaya Mkinga alisema kwamba jumla ya wahamiaji haramu 216 kutoka mataifa ya Ethiopia, Somalia na Kenya walikamatwa katika wilaya ya Mkinga katika Mwaka 2018.

Warsha hii ya siku tatu imelenga katika kuwajengea uwezo washiriki juu ya Uhalifu wa Kimataifa, Makosa ya kiuhamiaji, Biashara ya Magendo ya Binadamu, Usafirishaji Haramu wa Binadamu, Uraia wa Tanzania na mambo yanayohusiana na Uhamiaji nje ya Mfumo rasmi.
Mkuu wa wilaya ya Mkinga, Yona Maki akizungumza wakati wa mafunzo ya Ushirikishwaji wa Wananchi katika Ulinzi na Usimamizi wa Mipaka katika Kijiji cha Horohoro, mpakani mwa Tanzania na Kenya.
Msemaji wa Idara ya Uhamiaji, Ally Mtanda akitambulishwa kwa wajumbe wakati wa mafunzo ya Ushirikishwaji wa Wananchi katika Ulinzi na Usimamizi wa Mipaka katika Kijiji cha Horohoro, mpakani mwa Tanzania na Kenya

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...