Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
WAZIRI wa TAMISEMI, Selemani Jafo ameziagiza halmashauri zote zilizopatiwa fedha za kujenga hospitali ya wilaya mpya, kuhakikisha wanasimamia majengo hayo yanakamilika ifikapo June 30 mwaka huu. 

Aidha ameelekeza watalaamu wa halmashauri hizo wasimamie ubora wa majengo yanayoboreshwa na kupanua vituo vya afya ili yaweze kudumu kwa kipindi kirefu kijacho .
 Pamoja na hayo Jafo ameridhishwa na utekelezaji wa agizo alilolitoa kwa halmashauri ya Kibaha Vijijini, mkoani Pwani miezi michache iliyopita kuhusu kukarabati chumba cha kuhifadhia maiti katika kituo cha afya cha Mlandizi. 

Akitembelea ujenzi wa upanuzi wa kituo cha afya Mlandizi na hospitali ya wilaya inayojengwa Kibaha Vijijini, Jafo alitaka hospital hizo zikamilike kwa muda huo na kwa kiwango chenye ubora kulingana na thamani iliyotolewa. 

Alisema serikali imetoa kiasi cha sh. milioni 400-500 kwa vituo vya afya 97 nchini ili kuboresha huduma za afya kwa wananchi. 

Jafo pia aliyaasa mashirika yasiyo ya kiserikali ikiwemo TACAIDS kukabidhi fedha za miradi wanayotaka kuyajenga ikiwemo maabara katika kituo cha afya Mlandizi kwa halmashauri ya Kibaha Vijijini badala ya kusimamia wenyewe ili kuondoa mkanganyiko. 

"Kwanini mkandarasi wamlete wao, nyie wenyewe mmeweza kujenga kwa umakini na kutumia fedha vizuri kuboresha kituo hiki cha afya, kwanini wao wasitoe hizo milioni 600 kwenu mkasimamia miradi hiyo "

"Msije kuingizwa mkenge simamie na wanapaswa kupitisha fedha hizo kwenu "alifafanua Jafo. 
 Kuhusu chumba cha kuhifadhia maiti amepongeza halmashauri hiyo kwa kutekeleza agizo lake kwa asilimia 100. Nae mbunge wa jimbo hilo, Hamoud Jumaa alimuomba waziri huyo kuwaongezea fedha kwa ajili ya kuboresha zahanati ya Dutumi na Kwala. 

Jafo alisema serikali itaangalia uwezekano wa jambo hilo ukizingatia Kwala kunajengwa bandari kavu hivyo ni bora huduma za kijamii zikaangaliwa. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...