Na Munir Shemweta, MULEBA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameshangazwa na maafisa ardhi wa halamashauri ya wilaya ya Muleba mkoa wa Kagera kushindwa kuelewa idadi ya viwanja vilivyopimwa katika halmashauri hiyo na kumuagiza kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Shaban Manyama kufanya mabadiliko katika idara hiyo ili kupata watu sahihi watakaoisaidia idara.

Dkt Mabula alikutana na kadhia hiyo katika wilaya ya Muleba jana akiwa katika siku yake ya kwanza ya ziara yake ya kutembelea wilaya za mkoa wa Kagera kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi.

Waziri Mabula alisema haiwezekani watendaji wa sekta ya ardhi kuwa katika idara halafu wanashindwa kujua ni viwanja vingapi vimemilikishwa kwa wananchi wakati agizo lilishatolewa tangu mwaka 2017 kuwa viwanja vyote viingizwe kwenye mfumo ili kuwa na takwimu sahihi

‘’Hapa hakuna idara ya ardhi maana watendaji wake hawajitambui lazima pafanyike mabadiliko na kupata watu watakaoweza kusimamia idara hii maana sekta inadidimia kwa kukosa mtu wa kuisimamia’’. Alisema Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Aidha, Dkt Mabula ametaka afisa ardhi Mteule wa halmashauri hiyo kuwekwa chini ya uangalizi maalum wa miezi sita na kubainisha kuwa serikali haiwezi kuwa na sekta isiyofanya kazi zake kwa ufanisi.

Naibu Waziri wa ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi pia ameshtushwa na halmashauri ya wilaya ya Muleba kuwekewa lengo la kukusanya shilingi milioni mia tatu lakini ikifanikiwa kukusanya milioni 72,870,943 pekee huku ikidai bilioni 3.3 jambo alilolieleza kuwa halikubaliki kwani serikali inakosa mapato mengi.

Awali Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Muleba Shaban Manyama alimueleza Naibu Waziri Mabula kuwa halmashauri yake imeweza kukusanya shilingi milioni 72.87 kupitia kodi ya ardhi ambazo ni sawa na asilimia 24.3 na kuongeza kuwa katika kipindi cha mwezi februari mosi hadi tarehe 11 Machi jumla ya shilingi 1,802,750 zimekusanywa kama kodi ya ardhi.

Naye Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Ziwa Makwasa Biswalo alisema halmashauri ya wilaya ya Muleba inahitaji kusaidiwa kutokana na watendaji wake kutokuwa makini katika utendaji kazi na kutolea mfano tofauti ya takwimu za umilikishwaji ardhi katika halmashauri hiyo zinazoelezwa na watendaji wa sekta hiyo ni ishara kuwa idara hiyo inahitaji msaada na kuahidi kupeleka mtu kutoka ofisi ya ardhi Kanda ya Ziwa kwa ajili ya kuweka mambo sawa.
 Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akisalimiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Muleba mkoani Kagera alipowasili wilayani humo kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mhandisi Richard Ruyango.
 Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Muleba mkoani Kagera (hawapo pichani) wakati wa ziara ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi. Wa pili kushoto ni Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Ziwa Makwasa Biswalo na wa pili kulia ni Katibu Tawala wa wilaya ya Muleba Benjamin Mwakasege.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiangalia moja ya majalada ya ardhi katika Masijala ya ardhi ya halmashauri ya wilaya ya Muleba mkoa wa  Kagera akiwa katika ziara ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi. Wa pili kushoto ni Katibu Tawala wa Wilaya Benjamin Mwakasege, kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Muleba Shaban Manyama na wa pili kulia ni Afisa Ardhi Simon Mosha.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...