*Asema yeye na wenzake wameutua mzigo wa CUF na wala hawana habari tena

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

HATIMAYE Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi(CUF) Maalim Seif Sharif Hamad pamoja na viongozi wenzake wametangaza rasmi kuondoka Chama hicho na kujiunga na Chama cha ACT-Wazalendo leo Machi 18,2019.

Ametangaza uamuzi huo leo jijini Dar es Salaam ambapo amesema baada ya kutafakari kwa kina wameona wanayo nafasi ya kuendelea na mapambano ya kisiasa na hivyo wamejiunga ACT-Wazalendo kuendeleza mapambano hayo.

Uamuzi wa Maalim Seif na wenzake umekuja baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam leo asubuhi kutoa uamuzi wa kumtambua Profesa Ibrahim Lipumba kama Mwenyekiti halali wa CUF.

"Mahakama Kuu ya Tanzania imetoa uamuzi wa kesi 23 ya mwaka 2016 ambayo tuliifungua kupinga uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa kuingia maamuzi ya Chama ya kutomtambua Lipumba.

"Kwa mujibu wa Mahakama Kuu ya Tanzania ni kwamba Msajili kumtambua Profesa Lipumba kama Mwenyekiti halali wa CUF.Tunajua sababu za kutolewa kwa uamuzi huo ni kuihujumu CUF pamoja na demokrasia nchini.Mahakama ilichelewa kutoa uamuzi kwasababu ya kutoa nafasi kwa Lipumba kusajili Bodi ya Wadhamini,"amesema.

Akifafanua zaidi Maalim Seif anasema wanahamia ACT wakiamini umma wa Watanzania haujawahi kushindwa mahali popote na kusisitiza wana-CUF wote na wananchi kuwaunga mkono na sasa ni wakati wa shusha Tanga pandisha Tanga.

Ametumia nafasi hiyo kueleza kuna watu walijitolea nyumba zao kwa ajili ya Ofisi za CUF na ombi lake kwao waendelee na moyo huo huo kwa kuzifanya nyumba hizo kuwa ofisi za ACT-Wazalendo na safari inaendelea.

Pia amesema kitendo cha wao kuhama katika Chama ambacho wamepambana kukijenga inakwenda kuandika historia mpya kuelekea Tanzania mpya ambayo itasimamia haki kwa Watanzania wote na kwamba huko wanakokwenda wanakwenda wakiwa wanachama wa kawaida.

Ameongeza mzigo wa CUF kwa sasa wameutua na hawana habari tena na Chama hicho , kwani wao wameshamalizana nao na ni mwendo wa kusonga mbele na Watanzania wafahamu kabla ya kujiunga na Chama hicho wamefanya upembezi wa kutosha kwa kupitia Katiba ya chama kimoja baada ya kingine na wamejiridhisha ACT ndio sehemu sahihi ya wao kwenda.
 
"Eneo ambalo tunaamini mapambano yetu yataendelea ni ACT- Wazalendo, tunakwenda huko kupigania wananchi na si kutafuta vyeo.Hatuendi na masharti ya aina yoyote yale.Tunajua wanachama wa CUF wakiwamo wabunge wanatuunga mkono sana lakini tunaacha wachukue maamuzi wenyewe na sio sisi,"amesema Maalim Seif.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...