MJADALA WA WANA -CCM WASIVAE SARE ZAO  SHEREHE ZA UWASHAJI MWENGE KITAIFA WAIBUA MJADALA KATIKA KIKAO CHA KAMATI YA MWENGE MKOA WA SONGWE,

Na Mashaka Mhando, Mbozi

KIKAO cha Kamati ya Mwenge mkoani hapa, umewapiga marufuku wana-CCM watakaohudhuria sherehe za kitaifa za uwashwaji wa Mwenge Kitaifa zitakazofanyika mjini hapa Aprili 2 mwaka huu, wasivae sare zao za Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hoja hiyo iliwasilishwa na Mwenyekiti wa kikao hicho kilichofanyika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi na ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Brigedia Jenerali Mstaafu Nicodemus Mwengela ambapo amedai sherehe hizo ni za kitaifa na watu wa CCM hawapaswi kuvaa sare hizo.

Kikao hicho kilichofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, baada ya Mkuu huyo kuwasilisha hoja katika agenda ya sare zitakazovaliwa kwenye uwashaji huo, aliungwa mkono na wajumbe waliohudhuria kikao hicho isipokuwa Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mbozi Kazimbaya Makwega.

Baada ya hoja kujadiliwa kwa kina na wajumbe, Mkuu wa mkoa aliomba mwongozo kwa Mratibu wa Mwenge wa mkoa wa Songwe Saida Mponjoli alieleza kwamba watu wote wanatakiwa wavae sare za kitenge kilichoandaliwa.

Kamanda wa polisi mkoani Songwe ACP George Kyando aliuliza kimasihara kwamba na wao pia wanalazimika kuvaa sare hizo mwenyekiti akamjibu wanatakiwa pia kuvaa.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Mbozi Makwega hakukubaliana na uwamuzi huo akieleza CCM ndiyo waliounda Serikali hivyo wana kila sababu ya kuvaa sare zao.

"Hii mwenyekiti si sawa sisi wengine tuvaeni sare, lakini wana-CCM tusiwapangie, mathalani amekuja mwenyekiti wao wa Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anaweza kutuacha sisi tuliovaa sare za Mwenge akaenda kuwasalimia ndugu zake waliovalia, tuwaache wavae sare zao," alisema Makwega.

Hata hivyo, akichangia mjadala huo Ofisa Usalama wa Mkoa Paulius Nansebwa ambaye vikao vingi vya mkoa amekuwa mchangiaji mzuri, alisema sherehe hizo ni za kitaifa na watu wa CCM wasivae sare zao ili kufanya uwashaji huo wa Mwenge usionekane wa kichama.

Katibu wa CCM mkoani Songwe Mercy Mollel alihamanika katika kikao hicho na akasema hawawezi kuchukua ushauri huo na badala yake watawahamasisha wanachama wao wavae sare za chama hicho.

"Mwenyekiti hatuwaelewi  hii hoja mmeileta hapa, sisi CCM tunajua faida na umuhimu wa Mwenge na hatuwezi kupangiwa tutawahamasisha wanachama wetu waje wakiwa wamevaa sare zao, kwanza vitenge vya Mwenge mlivyotoa sisi CCM hatuvikubali," alisema Mollel.

Hadi kikao kinamalizika saa 12:30 jioni uwamuzi wa mkoa uliopitishwa ni kwamba CCM wasije wakiwa wamevaa sare zao za chama.

Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka huu utawashwa mkoani hapa katika mji wa Mlowo uliopo katika halmashauri ya ya wilaya ya Mbozi Aprili 2 mwaka huu. 

Halmashauri ya Mbozi ina majimbo mawili ya uchaguzi ambapo jimbo la Vwawa mbunge wake ni Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga na jimbo la Mbozi ambalo mbunge wake ni Paschael Haonga wa Chadema.

Halmashauri hiyo ina kata 29 ambapo NCCR ilishinda kata 1 na Chadema ilishinda kata 10  ingawa mwishoni mwa mwaka ulioisha madiwani watatu wamerudi CCM na kufanya hadi sasa katika halmashauri hiyo wabaki wanane.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...