Na: Moshy Kiyungi,Dar es Salaam

Jeuri ya pesa inaweza ikampandisha au kumshushia mtu umaarufu, hadhi hata heshima iliyoisaka kwa kipindi kirefu.

Pesa zikiwa nyingi kibindoni, husabisha dharau kwa mwingine asiyenacho, yupo radhi hata kumtemea mate utosini!

Tunashuhudia baadhi ya Watanzania wenzetu wanaopelekwa Ughaibuni, wakiahidiwa kupata ajira murua, lakini huko huambulia kufanyishwa kazi za ndani mithiri ya watumwa.Humu nchini wapo baadhi ya watu wamekuwa wakiwaajiri kaka na dada wa ndani wakiwafanyisha kazi nyingi kwa ujira mdogo pasi soni wala huruma.

Makala hii inamzungumzia mwanamuziki mkubwa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Koffi Olomide.Nguli huyu anayemiliki utajiri wa sawaswa na shilingi bilioni 40 za Kitanzania, yaelezwa kuwa ukiwataja wanamuziki matajiri, Koffi ni mmoja wao.

Olomide anamiliki hoteli yenye hadhi ya nyota 5, ana hisa kwenye Kampuni kadhaa ndani ya nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na nje.Ukwasi huo huenda ndiyo sababu ya ‘Wingu jeusi’ kumyemelea.

Mwaka jana aliingia kwenye mlolongo wa matajiri wasio na huruma wala staha kwa wafanyakazi wao.Koffi Olomide anakabiliwa na misukosuko lukuki iliyoisababisha mwenyewe kwa vitendo vyake vya kujichukulia sheria mkononi.

Mwanamuziki huyo mwaka jana alikataliwa kuingia nchini Zambia, ambako alitaka kufanya maonesho ya muziki kutokana na makosa mengi aliyoyafanya nchini Ufaransa.

Kuzuiliwa kwa Koffi Olomide kunatokana na ushawishi mkubwa wa Balozi wa Ufaransa nchini Zambia, Bwana Sylvain Berger, aliyesema kuwa mwanamuziki huyo anayo mashitaka nchini Ufaransa yanayomtuhumu kumshambulia mpigapicha wakati alipofanya ziara nchini humo.

Balozi Berger alitishia kuwatumia maofisa wa Polisi wa Kimataifa (Interpol), kumkamata mwanamuziki huyo, akisema kuwa mashitaka yake bado hayajafutwa nchini Ufaransa.Berger alijinasibu kwa kusema kuwa atashirikiana na serikali ya Zambia, kumkamata Olomide, iwapo atathubutu kuingia nchini humo.

Hata hivyo, kabla ya kupigwa marufuku, Koffi alijinasibu kuwa anaipenda nchi ya Zambia, huku akisema anataka hapo ndiko yawe makazi yake ya pili baada ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Mopao alikaririwa na kituo kimoja cha redio nchini Zambia, akiomba msamaha kuahirishwa kwa onesho la hilo kutokana na marufuku hiyo.Pamoja na hayo, alikana mashitaka yaliyosababisha apigwe marufuku kuingia nchini humo, bila kuingia kiundani kuhusu tuhuma zinazombabili.

Nyota huyo anayevuma kwa kupiga muziki mzuri na utanashati wa mitindo ya mavazi yake na maisha ya kifahari, amewahi kukumbwa na kashfa kama hizo katika miaka iliyopita.

Kumbukumbu zinaonesha mwaka 2008, alidaiwa kumpiga na kumvunjia kamera kibabe mpigapicha wa shirika la habari la RTGA!Olomide alifanya hivyo baada mpigapicha huyo kuingia sehemu moja ya burudani katika mji wa Kinshasa nchini DRC, kutofautiana kuhusu vibali vya kupiga picha.

Sakata hilo lilikuwa kubwa kiasi cha uongozi wa Bunge la Kitaifa kuingilia kati na kusulihisha mgogoro uliokuwepo kati ya mwanamuziki huyo na mmiliki wa kituo cha luninga hiyo.Olomide aliwahi pia kupigwa marufuku kufanya onesho Ulaya kutokana na kesi nyingine ya kuhangaisha wasakataji densi wake.

Aidha mwaka 2016, Koffi Olomide alinaswa kwenye kamera akimdharirisha mmoja wa wanenguaji wake kwa kumpiga teke baada ya kutua kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyata nchini Kenya.

Kutokana na tukio hilo serikali ya nchi hiyo, ilimuamuru mwanamuziki huyo kuondoka mara moja nchini humo, kutokana na kutokubaliana na vitendo vya udharirishaji kwa wanawake.Onesho lililokuwa limepangwa kufanya jijini Nairobi lilifutwa, huku wapenzi na mashabiki wake wakibaki wakisubiri kwa hamu.

Kama hiyo haitoshi, mwaka 2012, Koffi alipatikana na hatia ya kumshambulia na kumjeruhi msimamizi wake wa karibu, Diego Lubaki, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.Katika shambulio hilo, Olomide alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela.

Lakini hakukitumikia kifungo hicho gerezani baada ya kulipa faini.Ilidaiwa kuwa mwanamziki huyo alimshambulia Lubaki, kutokana na ubishani baina yao juu ya deni la dola 3,700.

Kisa kingine cha nguli huyu wakati mmoja alilighadhabisha Kanisa Katoliki alipojiongezea jina “Benedict wa 16 wa Kongo”, jina ambalo lilikuwa jina la Papa Benedict wa 16 wakati huo.

Koffi ni nani?

Wasifu wa mwanamuziki huyu unaeleza kuwa majina yake halisi anaitwa Antonie Christophe Agbepa Mumba. Alizaliwa Julai 13, 1956 katika mji wa Kisangani huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Olomide ana asili wa nchi mbili za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Sierra Leone.Mama yake ni raia wa Kongo DRC, akitokea katika kabila la Songye ambalo linapatikana katika mkoa wa Kasai. Baba yake ni mwenye asili ya nchi ya Sierra Leone.

Kwa mujibu wa mila na utamaduni wa kabila la babu zake, mama yake alimpa jina la ‘Koffi’ kutokana kuwa alizaliwa siku ya ijumaa.Olomide kuna kipindi alijartibu kuiingia katika uringo wa siasa nchini DRC, lakini alikumbana na vikwazo lukuki kikiwamo cha uraia wake kutiliwa mashaka.

Akiwa bado ‘kinda’ Koffi alipachikwa jina bandia la ‘Antoine Makila Mabe' likiwa na maana ya 'damu mbaya ya Antony’.Alianza safari ya muziki mwanzoni mwa miaka ya 1970, katika bendi ya Viva la Musica, iliyokuwa na wanamuziki magwiji akiwemo kiongozi wa bendi hiyo, Papa Wemba.

Koffi alianza kupiga muziki katika bendi hiyo akiwa kama mtunzi wa nyimbo na baadaye aligeukia katika uimbaji.Olomide pamoja na kupenda muziki tangu akiwa mtoto, ndoto zake kubwa zilikuwa awe mchezaji wa mpira wa miguu.

Kama Wahenga wasemavyo kuwa “Atafutaye hachoki, akichoka ujue kaisha pata”, mwaka 1986 alianzisha bendi iliyofahamika kwa majina ya Quartier Latin International.Baada ya miaka kadhaa kupita, bendi hiyo alijizolea umaarufu Kimataifa hususan katika Bara la Afrika na Ulaya.
Baadhi ya albamu zake zilizotoka ni Tcha Tcho ya mwaka 1990, Haut da gamme ya mwaka 1992, Noblesse Oblige ya mwaka 1994 na Magie ya mwaka 1995.

Zingine ni pamoja na Gagi ya Film Diva ya mwaka 1995, V 12 ya mwaka 1996, Loi ya mwaka 1997, Droit de Veto ya 1998, Attent ya mwaka 1999, Force de frappe ya mwaka 2000, Efrakata ya mwaka 2001, Affaire d’ Etat ya mwaka 2003, Monde arabe ya 2004 na Bord Ezang Kombo ya 2008.

Antoine Koffi Olomide alikulia katika familia ya watu wenye uwezo wa kati na mahali ambapo elimu ilikuwa ikipewa kipaumbeleAlipoanza kupevuka akiwa na umri wa miaka 18, wakati huo akiwa mwanafunzi kijana, alivutiwa sana na usanii pamoja na muziki, ndipo alipoanza kutunga na kuimba nyimbo.

Kwa mujibu wa historia hiyo, Koffi alikuwa ana akili sana darasani hali ambayo ilimfanya apate wadhamini wa kumlipia kwenda kusoma mjini Bordeaux, Ufaransa ambapo alipata Shahada yake ya kwanza ya Biashara na Uchumi.

Mbali na shahada hiyo inaeleza pia ana shahada ya pili katika masuala ya hisabati kutoka chuo kikuu cha Paris, Ufaransa. Akiwa Paris alianza kujifunza kupiga gitaa na kuandika nyimbo na aliporudi drc alijiunga na bendi ya muziki ya muziki ya viva la musica ambayo ilikuwa ikiongozwa na Papa Wemba.

Baada ya kujiunga na bendi hiyo Koffi aliimarisha mtindo wa polepole wa soukous uliokuwa umeisha umaarufu aliouita Tcha Tcho.Baadaye aliamua kujitenga na kundi hilo na kuanza kuimba kama mwanamuziki wa peke yake ‘soloist’ na hadi mwaka 1986, alipounda bendi yake aliyoipa jina la Quartier Latin.

Baada ya miaka kumi ya mafaniko yake, akatamani kuwa mwanamuziki wa Kimataifa. Ilipofika mwaka 1988 wimbo wa 'Henriquet' ukatokea kuwa mkali uliopelekea kupachikwa jina bandia la ‘Golden Star'.

Koffi olomide aliyafurahia mafanikio zaidi baada ya kuandika wimbo akiwa na binti yake pekee Minou, ukiitwa D'elle et Moi' miaka ya 1990.Koffi toka mwaka 1990 hadi 1994, alifurahia kukua kwa mafaniko yake ambayo kwa kipindi cha miaka chini ya minne, alifyatua zaidi ya album saba zikiwa chini ya jina lake na kundi lake la 'Quartier Latin’.

Mwaka 1992 alichaguliwa kuwa mwimbaji bora wa kiume na mshindi wa video bora katika shindano la African Music Awards mjini Abidjan, Ivory Coast.Yaelezwa kwamba ujuzi wa aina yake, mpangilio mzuri wa muziki kumempa umaarufu mkubwa ndani na nje ya nchi yake ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Antoine koffi Olomide alifyatua albam yake kali inayotamba ya Abracadabra, iliyonguliwa na albam za Ngounda, Efrakata, Tcha Tcho, Haute de Gamme – Koweit, Rive Gauche.

Baadhi ya nyimbo za nguli huyu ni pamoja na loi, Magie, Stila, Sexy Pop, Rounge A Levre, Etant Civil, Round Poit, San suit, Respect 2, l Autre la, Miss Dess, Nolesse Oblige na Escola Phamacien. Wimbo wa Phamacien sehemu kubwa ya uimbaji ametamba aliyekuwa mwimbaji wake Fally Ipupa.

Mwaka 1998, Koffi akiwa katika jiji la Paris nchini Ufaransa, alikimbiwa na wanamuziki takribani wote, baada ya onesho kubwa lilofanyika katika ukumbi wa Olympia.

Bendi hiyo ilisambaratika na baadhi ya wanamuziki wake wakaenda kuunda bendi yao ya Orchestra ‘Quartier Latin Academia.Baada ya tukio hilo, Olomide hakuteteleka kabisa kwani haikuchukuwa kipindi kirefu akaibua tena vijana wengine wenye vipaji toka sehemu mbalimbali nchini humo.

Amewafundisha wanamuziki wengi chipukizi ambapo wengine wameamua kujitegemea na kusimama wenyewe katika kazi za muziki na wengine bado wapo na bendi hiyo hiyo .Baadhi ya wanamuziki ambao ameshawatoa ni Fele Mudogo, Motana Kamenga, ambaye alitimka kwenda kujiunga bendi ya Big Star ya General Defao.

Wengine ni pamoja na Bruno Mpela, Soleil Wanga, Sam Tshintu, Suzuki 4 by 4, Ferre Gola na Fally Ipupa.

Olomide aliwahi kufika hapa nchini mwezi Desemba 2012 ambapo ‘alimwaga’ burudani kamambe zilizokonga nyoyo za Watanzania walihudhuria onesho lake lililofanyika katika viwanja vya Leaders, Kinondoni jijini Dar es salaam.

Nyimbo zake mpya zinazotamba hivi sasa ni Tshou Tshou, Nyataquance, Selfie, Mbirime, Afrakata, Charisma, Salopette, L’amour N’existe pas, Diaspora na Sixieme.

Koffi Olomide ni baba wa familia ya mke na watoto saba. 

Koffi Olomide Julai 13, 2018 alitimiza miaka 62, huku akiendelea na shughuli za muziki licha misukosuko hiyo kumharibia kazi yake. 

Hata hivyo nguli huyo Koffi ametangaza kung’atuka kwenye shughuli ya muziki baada ya kutoa albamu yake mpya ambayo iko studio kwa sasa, Hii itakuwa ni Albamu ya 20 ya mwanamuziki huyu ambaye anamaliza akiwa na mafanikio na mpaka sasa albamu zake tatu zimeorodheshwa kwenye orodha ya albamu 1,000.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...