Na Moshy Kiyungi
Jangwa la Mkoa wa New Mexico, huko nchini Marekani July 16, 1945, kulifanywa jaribio la mwanzo la kuliripua bomu la Atomic ambalo liliibadilisha dunia yetu. Bomu hilo lilikuwa na nguvu mara elfu mbili zaidi kuliko bomu lolote lililokuweko hapo kabla.

Bomu la mwanzo la atomic lilitengenezwa huko Los Alamos, katika maabara ya siri iliyokuweko katika milima ya New Mexico. Mwanafizikia Robert  Oppenheimer aliiongoza shughuli hiyo katika kipindi cha chini ya miaka miwili. Hapa nchini Tanzania kulianzishwa bendi ya muziki wa dansi iliyobeba jina la Atomic Jazz.

Ilikuwa ‘nguvu’ mithiri ya bomu la Atomic kwa bendi pinzani ya Jamhuri Jazz zote zikiwa makazi katika mji wa Tanga wakati huo. Atomic Jazz ilikuwa na wanamuziki mahiri waliweza kupiga muziki uliokuwa ukileta ushindani mkubwa kwa Jamhuri Jazz. Jiji la Tanga ambalo wakati huo ulikuwa mji, ndilo linalotajwa kwamba ndiko muziki wa dansi uliingia ukitokea katika mji wa Mombasa nchini Kenya.

Yaelezwa kwamba muziki huo ulianza kwanza kwa kuundwa klabu ambapo watu walialikana kwenda kucheza aina mbalimbali za muziki wa Kizungu. Mtindo maarufu uliotumiwa wakati huo unaojulikana kama Ballroom dancing. Aina hizi za klabu zilianzia katika mji wa Mombasa nchini Kenya na kuingia nchini humu kupitia Tanga, kisha kupelekwa Dar es Salaam.

Klabu iliyokuwa maarufu mjini Tanga wakati huo iliitwa ikiitwa Tanga Young Comrades Club. Siku zilivyokuwa zikisonga mbele, klabu nyingine ikaanzishwa, ikaitwa New Generation Club ambayo ilianzisha matawi miji mbalimbali. Atomic Jazz ilikuwa ni moja kati ya bendi zilizowika kwa muziki nchini wakati huo.

Zingine zilizotamba wakati huo ni za mahasimu wao Jamhuri Jazz, Kilwa Jazz, Western Jazz na Dar Jazz zote za kutoka mkoani Pwani wakati huo, sasa ni mkoa wa Dar es Salaam. Morogoro Jazz, Cuban Marimba za mkoani Morogoro, Tabora Jazz na  Kiko Kidds zilizokuwa mkoani Tabora, zilikuwepo zikifanya ushindani mkubwa katika muziki.

Mji wa Tanga wakati huo ulikuwa na vikundi vingine maarufu vya muziki wa dansi na taarabu zikitoa burudani maridhawa kwa wakazi wake mji huo na viunga vyake. Vikundi hivyo ni pamoja na bendi White Star, Amboni Jazz, Lucky Star, Black Star na kadhalika. Ikumbukwe kwamba vikundi hivyo vilitoa wanamuziki wengi wa dansi na taarabu ambao baadhi yao bado wapo katika tasnia ya muziki wa dansi na taarabu.

Bi. Shakila Bint Said na Bi. Asmahani waliokuwa waimbaji mashuhuri wa muziki wa taarabu, walitoka katika kundi la Lucky Star pamoja na mwanamuziki wa bendi ya The Kilimanjaro ‘Wana Nje nje’ Waziri Alli ni mfano wa wakongwe walitoka mjini Tanga. Bila ya kuwasahu ndugu wawili George na Wilson Peter Kinyonga walianzia safari yao ya kwenda Kenya wakiwa katika bendi ya Jamhuri Jazz.

Huko wakauda bendi ya Simba Wanyika hatimaye Les Wanyika na nyinginezo. Miaka ilivyokuwa ikisonga mbele, bendi zingine za Jamhuri Jazz na Atomic Jazz zikaanzishwa katika mji huo. Bendi hizo zilikuwa zikishindana kutoa burudani kwa wapenzi na mashabiki wake waliokuwa katika mji huo sanjari na  viunga vyake.

Makala haya yanaizungumzia bendi ya Atomic Jazz, iliyokuwa ikipiga muziki wake ikitumia mtindo wa ‘Kiweke’ uliokuwa maarufu hususani kwa wapenzi na mashabiki wa bendi hiyo. Atomic Jazz alikuwa na wanamuziki wengi ambao kwa pamoja  walileta changamoto kubwa dhidi ya wapinzani wao wakubwa bendi ya Jamhuri Jazz.

Bendi hiyo ilikuwa ikimilikiwa na Bwana Julius Kiluwa, aliyeweza kukusanya wanamuziki mahiri katika tasnia ya muziki wa dansi. Baadhi ya wanamuziki hao ni John Mbula aliyekuwa akipuliza Saxophone, Rodgers aliyekuwa  mwimbaji wakati John Kiluwa alikuwa mpiga tumba.

Huyo John alikuwa ni ndugu wa mmiliki wa bendi Julius Kiluwa. John Kijiko alikuwa akiliungurumisha gitaa la solo, Hemed Mganga alikuwa akisimama kwenye gitaa la rhythm. Hemed pia aliwahi kupiga muziki katika bendi ya Orchestra Makassy na ndie baba mzazi wa mwimbaji wa kizazi kipya Kassim Mganga.

Gitaa zito la besi lilikuwa likiungurumishwa na Mohamed Mzee. Kama nilivyokujuza awali kwamba Atomic Jazz ilikuwa na wanamuziki wenye weledi mkubwa katikia muziki. Waliweza kutunga na kupiga nyimbo nyingi ambazo zilirekodiwa wakati huo.

Baadhi ya nyimbo hizo zilikuwa ni za Ufukara umezidi, Vipi mpenzi wangu, Mahakimu, Madoo mpenzi wangu, Mimi ni mtoto wa Watu, Nakujutia Salima, Nakupenda ni Raga, Dunia ina mambo, Usitamani kitu na Wataka nini mpenzi.

Wimbo wa ‘Mado mpenzi wangu’ ulijijengea heshima kubwa kufuatia ujumbe uliokuwa ukijieleza. Ulikuwa na ujumbe wa kweli kutoka kwa mwanamuziki mmoja kwenda kwa mpenzi wake. Wimbo huo ulikuwa ni utunzi wa mpenzi wa Atomic Jazz, aliyekuwa amekubuhu kwa kuihusudu bendi hiyo wakati huo.

Aidha bendi ya Atomic Jazz iliweka jina la wimbo huo kwenye jarada la santuri. Msomaji wa makala haya kwa ridhaa yako naomba usome ubeti wa kwanza wa wimbo wa Dunia ina mambo. “Dunia ina mambo mengi, ya furaha na shida, kila uonapo raha ukumbuke mwisho utapata tabu, hasa sisi vijana wa leo mambo yetu ni mengi shida zikikufikia unalialia na kupata tabu…”

Haya ni maneno mazuri yenye mafundisho kwa vijana wa wakati ule na hata wa hivi sasa. Ni matumaini yangu kwa vijana wanaoinukia katika tasnia ya muziki kuzisaka nyimbo za wanamuziki wa zaman, wazisikilize yawezekana wakaambulia mambo mengi yakuwasaidia katika muziki.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...