Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

BALOZI wa Misitu nchini ambaye pia ni Miss Tanzania namba mbili Nelly Kazikazi amewashauri Watanzania wote nchini na hasa vijana kushiriki kikamilifu katika kutunza misitu iliyopo nchini huku akisisitiza kuna kila sababu ya kuwa na utaratibu kwa kila mmoja wetu kupanda miti.

Wakati Balozi wa Misitu akihamasisha upandaji miti, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) umesisitiza kuendelea na mkakati wake wa kuhakikisha inarejesha misitu ya asili katika maeneo ambayo imeharibiwa kwa kupanda miti ya asili kadri inavyowezekana ukiwemo Msitu wa Pugu ambao ndio mapafu ya Jiji la Dar es Salaam.

Hayo yameelezwa jana kwa nyakati tofauti baada ya kupandwa kwa miti zaidi ya 300 ya asili aina ya Mkakangazi katika Msitu wa Pugu mkoani Pwani. Wakati wa upandaji huo wa miti mbali ya kuwepo kwa maofisa wa TFS na Balozi wa Misitu, pia walikuwepo wadau wengine ambao ni wanafunzi wa Shule ya IST ya jijini Dar es Saalam.

Akizungumzia umuhimu wa kupanda miti, Balozi wa Misitu Nelly Kazikazi amesema vijana wanapaswa kutambua thamani ya misitu nchini na kuhakikisha wanashiriki kuilinda na kwamba wasidharau misitu kwani faifa zake nyingi na hivyo ni vema wakahamasika kuingeza badala ya kuipunguza.

"Nawahamasisha vijana wenzangu tuongeze namba ya misitu, tuwe na uaminifu kwa kupanda miti kadri tunavyoweza.Nafahamu wapo wanaokata miti kwa ajili ya mahitaji mbalimbali ya kibadamu lakini ni vema sote kwa umoja wetu tukapanda miti.

"Tunahitaji hewa safi ambayo inatokana na miti.Tunahitaji kivuli na kubwa zaidi misitu ule ukijani wake unaleta faraja kwa maisha ya binadamu,"amesema Nelly na kuongeza kwa kuwa mbali ya kuwa balozi wa misitu ni mwanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha(IFM), hivyo atahamasisha wanafunzi wengine kutambua thamani ya misitu iliyopo nchini. 

Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani Nanzia Charles amesema katika Msitu wa Pugu wenye hekta zaidi ya 2000 kuna miti iliyoharibiwa sana huko nyuma, kwa hiyo wanaendelea kupanda miti kwa lengo la kuufanya msitu huo kubaki kwenye uasili wake.

"Msitu wa Pugu na ule wa Kazimzumbwi tunasema ndio mapafu ya Dar es Salaam na kwa mazingira hayo TFS tumekuwa makini kuilinda na kila mara tunapanda miti katika maeneo ambayo tunabaini umefanyika uharibifu.Pia tunafahamu msitu wa Pugu ni wa asili na hivyo miti ambayo tunairejesha ni ile ya asili,"amesema Charles.

Kuhusu kuharibiwa kwa msitu wa Pugu amesema ulianza mwaka 2000 na sababu kubwa imetokana na msitu huo kuwa karibu na jiji la Dar es Salam, hivyo baada ya kubaini waliweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha msitu unabki salama ikiwa pamoja na kuweka walinzi na kupanda miti mara kwa mara na kuanzisha Kamati za mazingira kwa kushirikisha wananchi wanaouzunguka misitu.

Wakati huo huo Mkurugenzi wa Kampuni ya Ashton Media inayojihusisha na utenegezaji wa mabango ya matangazo Abbas Hirji amesema kampuni yao imeamua kushirikiana na TFS kutoa elimu kuhusu umuhimu wa utunzaji misitu na kufafanua kuna changamoto kubwa ya uharibifu wa mazingira.

"Ukiwa chini huwezi kuona uharibifu ambao umefanyika katika misitu yetu lakini ukiwa kwenye ndege utaona namna ambavyo moshi unawaka katika misitu kwasababu tu ya baadhi ya watu kuandaa mkaaa.Misitu yetu inaharibiwa sana.Hivyo tukaona tunalojukumu la kushirikiana na TFS ili tutoe elimu ya utunzaji misitu kwa faida yetu na watakaokuja.

"Mabango ambayo tumeyatengeneza yanazungumzia utunzaji wa misitu kupitia jumbe mbalimbali ambazo zipo kwenye mabango, tunaamini kwa kufanya hivyo tutakuwa tumesaidia kutoa elimu ya kutunza misitu yetu.Ni wajibu wetu kuilinda na kuitunza, hivyo tutaendelea kushirikiana na TFS ili kufanikisha dhamira njema ambayo kampuni yetu inayo kwa nchi yetu,"amesema Hirji .

Wakati huo huo Ofisa Misitu Mkuu Ugavi na Uenezi kutoka TFS 

Shaaban Kihulah amesema Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania umejipanga kuendelea kushirikiana na wadauo wote kuhakikisha misitu inatunzwa na ile ambayo imeharibiwa basi inarejeshwa kwenye uasili wake.

Amesema katika kuhakikisha malengo hayo wanafanikiwa wameamua kushirikiana kwa karibu pia na wanafunzi wa shule mbalimbali na vyuo kwa kuamini kwamba kwa kufanya hivyo idadi ya mabalozi wa misitu itaongezeka na kuondoa tatizo la uharibifu.

Katika kushirikiana huko na wanafunzi amesema katika upandaji miti wa Msitu wa Pugu wameshirikiana na wanafunzi wa Shule ya IST na wanaamini utamaduni huo utaendelea siku hadi siku.
 Balozi wa Misitu nchini ambaye pia ni Miss Tanzania namba mbili Nelly Kazikazi akipanda mti katika Msitu wa Pugu ikiwa ni ishara ya kuhamasisha watanzani kujenga utamaduni wa kupanda miti na kulinda misitu nchini
 Mwanafunzi wa Shule ya IST ya jijini Dar es Salaam Sallah Hirji akipanda mti katika Msitu wa Pugu ambapo baada ya kupanda mti amehamasisha watoto wengine nao kujenga utamaduni wa kutunza misitu nchini
 Baadhi ya maofisa wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) wakiwa na wafanyakazi wa Kampuni ya Ashton pamoja na wanafunzi wa shule ya IST katika bango ambalo linazungumzia umuhimu wa kutunza miti
Balozi wa Misitu ambaye pia ni Miss Tanzania namba mbili akiwa katika mlango wa kuingia katika pango la popo lililipo katika Msitu wa Pugu baada ya kupanda miti ndani ya msitu huo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...