Benny Mwaipaja, WFM, Washington D.C
BENKI ya Dunia imeahidi kuipatia Tanzania mkopo wenye masharti nafuu na msaada wenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.7 sawa na takriban shilingi trilioni 4 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020.
Ahadi hiyo imetolewa mjini Washington D.C nchini Marekani na Makamu wa Rais wa Benki hiyo anayeshughulikia Kanda ya Afrika Bw. Hafez Ghanem, alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango.
Bw. Ghanem amemhakikishia Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwamba uhusiano kati ya Serikali na Benki yake bado uko imara na kwamba benki hiyo iko tayari kushirikiana na Tanzania ili iweze kufikia maendeleo yanayo tarajiwa.
Miongoni mwa miradi itakayonufaika na mkopo na msaada huo ni mpango wa elimu ambapo benki hiyo imeongeza ufadhili kutoka dola milioni 300 hadi dola milioni 400 na mradi wa kusaidia kaya masikini kupitia TASAF ambapo benki hiyo imeamua kuongeza kiwango cha fedha kutoka dola milioni 300 hadi kufikia dola milioni 450.
Kiasi kingine cha fedha kitatumika kutekeleza miradi mbalimbali katika sekta za miundombinu ya barabara, maji, Tehama, Afya, kilimo, hifadhi ya jamiim Nishati, utawala bora, lishe, sekta ya fedha, biashara, mazingira na maliasili pamoja na maji nk.
Akizungumza kwenye kikao hicho Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ameishukuru Benki hiyo namna inavyoisaidia nchi katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii ambapo mpaka sasa Benki hiyo imefadhili miradi 21 ya maendeleo kwa gharama ya dola za Marekani bilioni 4.8, sawa na takriban shilingi trilioni 11.
Ameahidi kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika utekelezaji wa masuala mbalimbali na kuiomba benki hiyo iendelee kuisaidia nchi ili iweze kufikia maendeleo yaliyokusudiwa ikiwemo kuondoa umasikini wa  wananchi.
Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango, ukimshirikisha pia Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Prof. Florens Luoga, upo mjini Washington D.C nchini Marekani kuhudhuria mikutano ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF, taasisi ambazo Serikali ina hisa.
 Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (katikati) akifurahia jambo lililozungumzwa na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Kanda ya Afrika Bw. Hafez Ghanem (hayuko pichani) wakati wa mkutano wa ujumbe wa Tanzania na uongozi wa Benki hiyo Mjini Washington D.C, Marekani. Kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi-Zanzibar Bw. Khamis Mussa Omar na kushoto ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Prof. Florens Luoga.
 Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Kanda ya Afrika Bw. Hafez Ghanem, akiihakikishia Tanzania kwamba Benki yake itaipatia dola za marekani bilioni 1.7 ili iweze kutekeleza miradi yake mbalimbali ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika kipindi cha mwaka mmoja ujao wa fedha 2019/2020.
 Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Dkt. Yamungu Kayandabila (kulia) na Kamishna wa Bajeti kutoka Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Mary Maganga, wakifuatilia kwa makini mazungumzo kati ya Waziri wa Fedha na Mi[pango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Bw. Hafez Ghanem (hawako pichani) mazungumzo yaliyofanyika Mjini Washington D.C, Marekani, ambapo Benki hiyo imeahidi kuipatia Tanzania karibu shilingi trilioni 4 kwa ajili ya kutekeleza miradi yake mbalimbali ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika mwaka wa Fedha 2019/2020.
 Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (kushoto) akiteta jambo na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania Bi. Bella Bird mara baada ya kumalizika kwa mkutano kati ya Ujumbe wa Tanzania na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Kanda ya Afrika Bw. Hafez Ghanem, Mjini Washington D.C nchini Marekani.
Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Balozi Wilson Masilingi (katikati) akizungumza jambo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango (kulia) na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Prof. Florens Luoga (kushoto) kabla ya kuanza kwa mkutano kati ya Ujumbe wa Tanzania na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Kanda ya Afrika Bw. Hafez Ghanem, Mjini Washington D.C nchini Marekani. (Picha na Benny Mwaipaja, WFM, Washington D.C)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...