*Akagua mradi wa ujenzi wa kituo cha mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani Mbezi Louis, aridhishwa na kasi

Na Leandra Gabriel, Michuzi TV

MEYA wa Manispaa ya Ubungo Boniface Jacob leo amekuwa na wakati mgumu baada ya Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda kumtolea uvivu Meya huyo kwa kile kilichoelezwa ni kukosa nidhamu kwa kudanganya wananchi kuwa yeye ndio amefanikisha mradi wa ujenzi wa Kisima cha maji Kata ya Mbezi Makabe wakati Rais Dkt.John Magufuli ndiye aliyetoa fedha hizo kiasi cha Shilingi milioni 611 kwa ajili ya kumaliza kero za maji kwa wananchi.

Hayo yamejiri leo wakati wa mwendelezo wa ziara ya ukaguzi miradi ya Maendeleo Mkoa wa Dar es salaam ambapo Makonda ameshangazwa kuona Meya anakijinadi mbele ya wananchi na viongozi kuwa yeye ndiye aliyefanikisha upatikanaji wa fedha hizo na ndio aliyeweka saini badala ya kumshukuru Rais Dkt. John Magufuli kwa  kutoa fedha hizo.

 Makonda amesema kitendo hicho ni utovu wa nidhamu kwa viongozi wanaotoa fedha kwa ajili ya kutatua kero za wananchi ambapo amemtaka Meya huyo kuwa na shukrani kwa viongozi bila kujali itikadi za kisiasa.

Mradi wa ujenzi wa kisima cha Maji Mbezi Makabe unagharimu zaidi ya Shilingi Million 611 zilizotolewa na Rais Magufuli na unatarajiwa kunufaisha zaidi ya Wakazi 75,000.

Wakiwa katika ujenzi wa ofisi za Manispaa ya Ubungo Meya Jacob amewahimiza wasimamizi wa mradi huo ambao ni wakala wa majengo nchini (TBA) kukamilisha mradi huo kwa wakati kabla ya mwaka kuisha na wao kama viongozi watasimamia hilo.

Wakati huo huo Makonda ametembelea ujenzi wa kituo kipya cha mabasi yaendayo Mikoani na nchi jirani mradi unaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 50 na hadi kufikia Machi mwaka huu ulikua umekamilika kwa asilimia 12.5.

Akiwa katika mradi huo Makonda amehimiza kuzingatia ushirikishwaji wa wazawa katika miradi hiyo mikubwa ili waweze kunufaika zaidi na hata malighafi zinazotumika katika ujenzi zitumike zile zinazozalishwa nchini ili kuongeza kipato kwa wananchi na taifa zaidi.

Akiwa Wilayani humo RC Makonda ametembelea miradi ya ujenzi wa kituo kipya cha mabasi, ujenzi wa ofisi za Manispaa, ujenzi wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya na mradi wa maji kupitia kisima kinachojengwa Mbezi Makabe.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...