GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Florens Luoga, amesema elimu kuhusu masuala ya fedha ni muhimu katika mfumo mzima wa taarifa za mikopo ili kuwawezesha Watanzania kupanga matumizi bora ya mikopo.

Prof Luoga alitoa kauli hiyo katika uzinduzi wa kampeni ya uelimishaji umma kuhusu taarifa za mikopo na fedha iliyoratibiwa na BOT kwa kushirikiana na taasisi ya International Finance Corporation ambayo ni mwanachama wa Kundi la Benki ya Dunia.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mpango, Dk. Philip Mpango, Prof Luoga alisema taarifa za mikopo na elimu ya fedha ni muhimu ili kuhakikisha Watanzania wanaondokana na matumizi ya anasa ya mikopo.

“Kampeni hii ya elimu kwa umma inalenga kuwaelimisha watumiaji wa huduma za fedha na wadau wengine kukuza uelewa wao kuhusu taarifa za mikopo ili kuongeza ushiriki katika matumizi ya taarifa za mikopo hapa nchini,” alisema.

Aidha, Meneja Msaidizi, Mfumo wa Kumbukumbu za Wakopaji kutoka BoT, Nkanwa Magina alisema kampeni hiyo ya miezi mitatu inalenga kuongeza uelewa, mwamko kuhusu taarifa za mikopo na kukuza upatikanaji wa mikopo.

”Kauli mbiu katika kampeni hiyo ni: “Pata Taarifa Yako ya Mikopo Leo. Angalia hali yako ya kifedha ili kupanga mustakabali wako bora wa kesho” inaungwa mkono na wadau mbalimbali katika sekta ya huduma za fedha.

“Wadau hao wameahidi kusaidia kusambaza ujumbe kuhusu umuhimu wa upatikanaji wa mikopo na jinsi Watanzania wanavyoweza kuishi maisha bora kwa kuweza kupata taarifa za mikopo yao na kujua historia ya mikopo yao,” alisema.

Alisema usimamizi mzuri wa mikopo na historia nzuri ya mikopo ni muhimu katika kuwezesha kupata mkopo nafuu."Kuhakiki taarifa yako ya mikopo mara moja kwa mwaka ni huduma inayopatikana bila malipo, tena itakuletea mafanikio kwa kukuandaa vema utakapoenda kuomba mkopo. 

"Historia nzuri ya mikopo inaweza kusaidia kustahili viwango vya chini vya riba na ada, hivyo kuondokana na kutenga fedha kwa ajili ya dharura na gharama zisizotarajiwa," alisema. 

Alisema mikopo inasaidia kupata mahitaji ya sasa, kama vile nyumba au ada ya shule ya mtoto wako, kwa kuzingatia ahadi yako ya kulipa kwa awamu na kwa muda uliopangwa.Aidha, Meneja wa IFC - Tanzania, Manuel Moses alisema taarifa ya mikopo inaonesha taarifa binafsi; utambulisho na taarifa ya mawasiliano na ikiwezekana historia ya ajira; idadi na aina za akaunti za mikopo.

Naye Meneja Maendeleo ya Biashara kutoka Dun & Bradstreet, Josephine Temu alisema kwa sasa, kuna taasisi mbili zilizopatiwa leseni na Benki Kuu ya Tanzania kuandaa na kutoa taarifa za mikopo hapa Tanzania ambazo ni Creditinfo Tanzania Limited na Dun & Bradstreet.Alisema taasisi hizo zinakusanya na kutunza taarifa za mikopo na kutoa taarifa za mikopo kwa kampuni au watu wanaozihitaji kama vile benki. 

Alisema ripoti hiyo ya mikopo inaweza kutolewa na taasisi hizo (Creditinfo na Dun & Bradstreet) mara moja kwa mwaka bila malipo.“Ili kupata taarifa ya mikopo unatakiwa kuwasilisha nakala ya kitambulisho chako cha taifa au kingine kama leseni ya udereva, hati ya kusafiria. Jaza na wasilisha fomu ya maombi ya taarifa yako ya mikopo katika taasisi zinazoandaa taarifa za mikopo ambazo kwa sasa ni Creditinfo au Dun & Bradstreet," alisema.

Akifafanua kuhusu mambo muhimu ya kuangalia kwenye taarifa ya mikopo, Meneja Maendeleo ya Biashara kutoka Creditinfo, Tonny Missokia alisema muhimu ni taarifa binafsi kama vile jina, hadhi ya ndoa, anwani, taarifa za ajira na namba za mawasiliano ni sahihi.
 Meneja Msaidizi, Mfumo wa Kumbukumbu za Wakopaji kutoka BoT, Nkanwa Magina akizungumza katika warsha ya kuhusu elimu ya taarifa za fedha na ripoti za mikopo kwa wanafunzi wa Chuo kikuu cha Dodoma.
 Meneja Msaidizi, Mfumo wa Kumbukumbu za Wakopaji kutoka BoT, Nkanwa Magina akizungumza katika warsha ya kuhusu elimu ya taarifa za fedha na ripoti za mikopo kwa wanafunzi wa Chuo kikuu cha Dodoma.
 Wataalam wa Benki Kuu ya Tanzania, Creditinfo na Dun & Bradsheet wakitoa elimu kuhusu umuhimu wa taarifa za mikopo kwa mwananchi eneo la Nyerere Square mchana huu. Kampeni hiyo inaendeshwa kwa pamoja na Benki Kuu ikishirikiana na International Finance Corporation ambayo ni sehemu ya kundi la Benki ya Dunia

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...