Mkuu wa Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam Sophia Mjema akijiandaa kukabidhi bodaboda ambazo zimetolewa na wilaya hiyo ili kukopesha wananchi.Mikopo hiyo ya bodaboda imetolewa leo viwanja vya Mashujaa Mnazi Mmoja

*Pia kuna mikopo ya Bajaji, bodaboda ili kuinua maisha ya wananchi

Na Said Mwishehe, Globu ya jamii

HALMASHAURI ya Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam imetoa mkopo wa Sh.bilioni 1.7 kwa vikundi 295 kwa lengo la kuwajengea uwezo kiuchumi, huku Mkuu wa Wilaya hiyo Sophia Mjema akiwataka waliopewa mkopo huo kurejesha kwa wakati ili wengine nao wakopeshwe.

Kwa mujibu wa Ilala utolewaji wa mkopo huo wa fedha kwa wananchi uliokwenda sambamba na utoaji wa mikopo ya bajaji 30 na bodaboda 29, ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ambayo inazungumzia kuwawezesha wananchi kiuchumi .

Pia imeelezwa ni mkakati wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk.John Magufuli iliyodhamiria kuinua maisha ya wananchi wanyonge kwa kuwajengea uwezo wa kiuchumi.

Akizugumza leo Aprili 17, 2019 wakati wa kukabidhi mkopo huo kwa vikundi 295, Mkuu wa Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam Sophia Mjema amesema waliopewa mkopo huo wanapaswa kurejesha kwa wakati ili wengine nao wakope na kwa kufanya hivyo wananchi wengi watakuwa wameinuka kiuchumi.

"Leo hii Wilaya ya Ilala tumetoa mkopo wa fedha wenye thamani ya Sh.bilioni 1.7 kwa alili ya kukopesha vikundi mbalimbali ndani ya Wilaya yetu.Hata hivyo lengo letu ni kutoa mkopo zaidi na kati ya Mei na Juni mwaka huu tutatoa tena mkopo wenye thamani ya Sh.bilioni mbili na lengo letu ni kutoa Sh.bilioni nne.

"Mbali ya kutoa mkopo wa fedha, tumetoa mkopo wa bajaji, pikipiki na mkopo wa vifaa vya kilimo kulingana na mahitaji ya vikundi ambavyo vimepwa mkopo huu.Kazi yetu kubwa wasaidizi wa Rais wetu mpendwa ni kutimiza ndoto zake ambazo anataka kuona wananchi wa hali ya chini wanakuwa na maisha mazuri.

"Hivyo kitendo cha kutoa mkopo huu Ilala tunakwenda kuinua maisha ya wananchi wetu, tunaamini wapo ambao wamepata mkopo huu na baada ya kipindi kifupi watakuwa matajiri wakubwa,"amesema Mjema.

Ametoa rai kwa wananchi kuendelea kumuombea Rais Magufuli awe na maisha marefu na hatimaye aweze kutimiza ndoto zake za kuwaletea maendeleo Watanzania wote na kwamba Ilala itaendelea kuweka mikakati ya kuendelea kuinua maisha ya wananchi.

Mjema amesema viongozi wa Chama na Serikali wameungana na wataendelea kufanya kazi kwa bidii. "Kila jambo ambalo linafanyika katika taifa hili yamo kwenye Ilani ya uchaguzi. Kutoa bajaji, boda boda ,kutoa mikopo ya fedha ni utekelezaji wa Ilani".

Wakati huo huo Mjema amesema Rais Magufuli anawapenda Watanzania na kwamba alianza kutoa vitambulisho vya wajasirimali na sasa wanatamba na kuwataka waendelee kutamba na kwamba mikopo iliyotolewa haina riba. 

Awali Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam amesema kuwa jumla vikundi 295 vimenufaika na mkopo huo na kwamba wataendelea kutoa na kwamba wamejipanga kutoa Sh.bilioni nne licha ya kwamba leo tayari wametoa Sh.bilioni 1.7.

"Hadi sasa jumla ya 3, 209 wanafuika na mkopo ambao umetolewa na kati ya hao wanawake ni 2, 744 na kwa upande wa vijana ambao wamenufaika hadi sasa ni 332.Hata hivyo tunaamini waliokopeshwa bajaji na pikipiki watarudisha fedha kwa wakati,"amesema.

Ameongeza mikopo inalenga kupunguza umasikini wa kipato kwa wananchi wa Manispaa ya Ilala na kufafanua kuna vikundi ambavyo vimeomba mikopo ya vifaa vya kilimo.Pia kutokana na mkopo huo wapo ambao wamekopa kwa ajili ya kuanzisha viwanda vidogo vidogo , hivyo matarajio ni kuanzishwa viwanda vidogo 150 ndani ya Wilaya hiyo.
 Mkuu wa Wilaya ya Ilala Sophia Mjema(wa pili kushoto) akifurahia jambo baada ya kutoa hutuba kwa vikundi mbalimbali ambavyo vimekabidhiwa mkopo wa bajaji,bodaboda na fedha
 Mkuu wa Wilaya ya Ilala Sophia Mjema akiwa amepakizwa kwenye pikipiki baada ya kukabidhiwa kwa vikundi ambavyo vimepewa mkopo wa bodaboda
 Viongozi wa Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Sophia Mjema wakicheza muziki kabla ya tukio la kukbidhi mkopo kwa wananchi ambao wamejiunga kwenye vikundi mbalimbali
 Bajaji ya mkopo iliyotolewa na Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam ikiwa na ujumbe maalum kuhusu bajaji hizo ambazo ni za mkopo
 Sehemu ya wananchi wa Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam wakicheza muziki wakati wa utolewaji wa mikopo ambapo baadhi ya wamepata mkopo wa fedha, bajaji na bodaboda
Baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam wakiwa katika moja ya bajaji ambayo ni ya mkopo iliyotolewa na wilaya hiyo

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...