Na Leandra Gabriel, Blogu ya Jamii
MAMLAKA ya Zimamoto ya Jiji la Paris imetangaza kuwa wamefanikiwa kudhibiti moto uliokuwa ukiwaka katika jengo la kanisa la kale la Notre Dame. Ingawa bado kuna moto unaendelea kuwaka katika paa moja wapo la jengo hilo maarufu la utamaduni.
Moto uliolipuka na kushika paa lililoezekwa kwa mbao ulienea kwa masaa manne huku ukiharibu kabisa upande wa juu wa ghorofa wenye urefu wa mita 93.
Wazima moto takribani 400 wamehusika katika kuzima moto huo, huku maji ya kuzima moto yakimwagwa kwa njia ya anga ili kuokoa jengo hilo lenye miaka 850 tangu kujengwa.
 Shirika la utangazaji la Al Jazeera limeripoti kuwa, Mkuu wa kitengo cha zimamoto Jean-Claude Gallet ameeleza kuwa eneo kubwa la kanisa limeweza kuokolewa na kwamba hata mnara wa kengele ambao ndio ulikuwa hatarini kufikiwa na moto upo salama.

Vyombo vya habari vya Ufaransa vimeeleza kuwa kuna uwezekano mkubwa moto umetokana na shughuli za ukarabati zilizokuwa zinaendelea kwenye jengo hilo la kihistoria. Ofisi ya Upelelezi ya Paris imeeleza inaendesha uchunguzi juu ya sababu ya kutokea kwa moto huo.

Msinyori Patrick Chauvet ameeleza sehemu kubwa ya kuvutia ya jengo imeweza kubaki salama.

 Rais wa Ufaransa Macron Emmanuel ameeleza kuwa, ‘Kwa kiwango kikubwa uharibifu haujatokea, ingawa vita vya moto hivi havikushindwa kwa ukamilifu wake’. Ameitaja Notre Dame kama kiini cha maisha ya wafaransa. Hivyo ametoa wito kulijenga upya jengo hilo.
‘Ni jambo ambalo lilitegemewa na wafaransa, hii ilistahili kuhifadhi historia yetu! Ni sehemu ya mwisho kujivunia’ alieleza waandishi wa habari.

Wakazi wa Paris na watalii walijikusanya kutazama tukio hilo la kuogofya likiendelea karibu na kingo za mto Seine huku wahudumu wa dharura wakizima moto. Jengo hilo lilikuwa kwenye ukarabati wa gharama ya dola milion 6.8.
Msemaji wa kanisa amesema kuwa eneo lote lililokuwa na mbao zilizoezekwa karne ya 12 limeungua.

Wakazi wa karibu na jengo hilo waliondolewa kama tahadhari ikitokea jengo hilo likiangushwa na moto uliokuwa unawaka katika jengo la kanisa ameeleza Meya wa paris,  Anne Hidalgo.

Mashuhuda walikuwa wakilia kuona jengo hilo linaungua. Na tahadhari imetolewa kwa wote wanaopita karibu na jengo la kanisa.

Inasikitisha kuona jengo hili likiwaka moto, Kanisa hili ni alama ya jiji la Paris duniani kote! Mtoto Claire, ameeleza "Notre Dame ni moyo wa Paris na niliposikia tu jengo linawaka moto nikajiuliza tutabaki na nini?" Alieleza

Jengo hilo limekuwepo tangu wakati wa vita vya kidini, miaka zaidi ya 850 iliyopita lilianza kutumika na tayari matajiri wawili nchi Ufaransa  wanatoa euro milioni 300 kulitengeneza kanisa hilo. Bilionea Francois-Henri Pinault anatoa euro milioni 100, huku bilionea Benard Arnault akitoa euro milioni 200.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...