* Awalipua wanaotekeleza miradi chini ya viwango na kwa kusuasua

*Amwagiza DC Kinondoni kuhakikisha vibarua wanalipwa stahiki yao bila makato

Na Leandra Gabriel, Blogu ya Jamii
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda leo Aprili 15 amefanya ziara yake katika Manispaa ya Kinondoni na kukagua miradi ya kimaendeleo inayotekelezwa huku akiwataka watendaji kukamilisha miradi hiyo kwa muda muafaka kama ilivyopangwa ili wananchi waweze kunufaika na miradi hiyo.

Akizungumza mara baada ya kutembelea takribani  miradi  tisa Makonda amesema kuwa kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo inaridhisha huku akiwataka wasimamizi wa mradi wa ujenzi wa soko la kisasa la Magomeni kutokubaliana na mshauri ambaye amekuwa akibadilisha michoro na vipimo hasa kwa kupunguza wakati ujenzi ukiendelea hali inayopelekea majengo kutofaa kwa matumizi ya baadaye.

Ameeleza kuwa Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais Dkt. John Magufuli imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha huduma za muhimu zinapatikana kwa wananchi huku akieleza kuwa ujenzi wa kituo cha afya cha Kigogo kati kitakachokamilika Mei 30 kitapunguza adha kwa wananchi kwa kuwa hadi kukamilika kwake huduma zote zikiwemo za upasuaji zitakuwa zinapatikana na zitahudumia eneo hilo lenye wakazi zaidi ya elfu sabini.

Akiwa katika shule ya sekondari Mzimuni Makonda amekagua mradi wa ujenzi wa madarasa 6 na kuzungumza na wanafunzi wa shule hiyo ambapo amewataka kuwa nidhamu, malengo na kusikiliza wanachofundishwa na walimu wao.

Aidha RC Makonda ametembelea ujenzi wa barabara ya barafu Mburahati ambapo ameeleza kutoridhishwa na ujenzi huo ambao upo chini ya kiwango na kuagiza kandarasi inayosimamia ujenzi wa barabara hiyo kufanya kazi usiku na mchana kwa viwango vinavyostahili kabla hajarudi tena kwa ajili ya ukaguzi. Pia amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Daniel Chongolo kuhakikisha kuwa vibarua wanaofanya kazi katika eneo hilo wanalipwa gharama za shilingi 12,500 kwa siku kama wanavyostahili na hiyo ni baada ya vibarua hao kutoa malalamiko kuhusu malipo yao kwa Rc Makonda.

Katika mradi wa barabara ya Ubungo (Simu 2000) Makonda amesema kuwa ujenzi huo ukamilike kwa wakati huku akieleza fedha za ujenzi wa mita 200 ambazo zimechukuliwa na zitajengwa na Manispaa inayosimamia ujenzi wa Flyover (Ubungo) zikatengeneze barabara ya Shekilango hadi Ubungo Maziwa ili kupunguza adha kwa watumiaji wa barabara hiyo.

Aidha Makonda ameeleza kufurahishwa na ujenzi wa soko la Sinza, kituo cha afya Msasani, na ujenzi wa kituo cha afya cha Kigogo kati ambacho Manispaa ilijiongeza kwa kununua majengo na kuyakarabati ili waweze kuhudumia afya za wananchi hao.

Katika ziara hiyo Makonda ametembelea na kukagua; ujenzi wa soko la kisasa la Magomeni, ujenzi wa vyumba vya madarasa 6 katika shule ya Sekondari Mzimuni, ujenzi wa kituo cha afya cha Kigogo kati, ujenzi wa barabara ya Barafu Mburahati, ujenzi wa mitaro Tandale, ujenzi wa barabara simu 2000 Ubungo, ujenzi wa soko Sinza, ujenzi wa barabara ya Mabatini pamoja na ujenzi wa kituo cha afya Msasani.

Ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam iliyoanza Aprili 13 kwa kutembelea Manispaa ya Kigamboni imelenga kukagua miradi yote ambayo inasimamiwa na Serikali na hiyo ni sambamba na kulinganisha taarifa zinazopelekwa ofisini kwake na kile kinachotendeka katika maeneo husika.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda akikatisha katika barabara ya Barafu Mburahati jijini Dar es salaam wakati akikakugua ujenzi wa barabara hiyo, leo jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda (katikati) akikagua ujenzi wa mtaro katika eneo la Tandale jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake aliyoifanya leo katika Manispaa ya Kinondoni, kulia ni Mkuu wa Wilaya hiyo Daniel Chongolo, leo jijini Dar es Salaam. 
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda akikagua ujenzi wa barabara ya Barafu Mburahati ambako ameagiza kasi na viwango vitumike katika ujenzi huo na amemwagiza Mkuu wa Wilaya hiyo Daniel Chongolo kuhakikisha vibarua wanalipwa stahiki yao bila makato yasiyo na msingi, leo jijini Dar es Salaam. 
Muonekano wa jengo la kituo cha afya Msasani, Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...