Na Moshy Kiyungi, Dar es Salaam.
Kifo cha mwanamuziki wa muziki wa Jazz kutoka nchini Zimbabwe Oliver Mtukudzi ‘Tuku’ kimewaacha katika majonzi makubwa baadhi ya wapenzi wamuziki huo. Tuku alifariki dunia Januari 23, 2019 katika hospitali ya Avenues mjini Harare nchini Zimbabwe akiwa na umri wa miaka 66.

Oliver alikuwa amelezwa hospitalini humo kwa ajili ya kupaitiwa matibabu baada ya kuugua kwa muda mrefu. Kabla hajalazwa mwanamuziki huyo alikuwa katika ziara za kimuziki katika nchi mbalimbali duniani. Ilimlazimu kuzikatiza sababu ya maradhi yaliyokuwa yakimsumbua.

Tuku aliibeba Tuku Music kama beji ya heshima na kuipa hadhi sanaa ya Afrika, alifariki dunia tarehe sawa na ile ambayo rafiki yake, mkongwe wa muziki, Hugh Masekela alifariki dunia, Afrika Kusini, mwaka jana 2018. Aliwahi kuja nchini Tanzania mwaka 2011 kwa kazi hiyo, akaimba nyimbo nyingi kuhusu Ukimwi, ukiwemo Todii ambao ni Lifetime song.

Oliver atakumbukwa kwa vibao vyake vingi vilivyotikisa Ulimwengu wa muziki, hasa wimbo wa 'Neria' na 'Todii'. Baadhi ya Wabunge nchini Zimbabwe walitoa pole kwa familia na mashabiki wa Mtukudzi huku wakimtaka Rais kutangaza msiba wa Kitaifa.

"Tumepoteza nembo ya Taifa namwandikia rais Emmerson Mnangagwa kuomba atangaze msiba wa taifa kwa heshima ya shujaa huyu kwa mchango wake wa kitaifa kwenye sekta ya muziki, sanaa na utamaduni'', alisema mbunge wa Norton Temba Mliswa.

Moja ya viongozi wengine waliotoa pole ni Waziri wa zamani wa Elimu, Michezo, Sanaa na Utamaduni nchini Zimbabwe David Coltart ambaye amesema "Pumzika kwa amani Oliver Mtukudzi, kama kuna mtu yeyote amewahi kuitangaza Zimbabwe ni wewe. Asante kwa kutufanya tufurahi kwa muda mrefu."

Mtukudzi maarufu kama ‘Tuku’ alikuwa ni msanii na mwandishi mashuhuri wa ngoma mbalimbali huku akiwa ni moja ya wasanii wenye albam nyingi zaidi akiwa nazo zaidi ya 60. Mapema mwaka jana 2018, alilazwa katika hospitali moja mjini Harare kwa shinikizo la damu. Hata hivyo aliruhusiwa na hali yake ikaimarika.

Mwanamuziki huyo alishawahi kufanya muziki na msanii wa Bongo Fleva, Lady JayDee wimbo unaoitwa “I am who I am” au ka lugha yetu ya Kiswahili 'Mimi ni Mimi' wakiimba kwa lugha za Kishona na Kiswahili. Baada ya kifo cha nguli huyo Lady JayDee alisema Oliver Mtukudzi alikuwa mwanamuziki mrahisi kufanya naye kazi kutokana na tabia yake ya kumpokea mtu jinsi alivyo.

Alitamka kuwa mara baada ya yeye kukutana na Oliver Mtukudzi, alimshauri vitu vingi kuhusu muziki kitu ambacho kimempa faida. "Baada ya hapo mambo yalibadilika kutokana na ushauri aliyonipa, namna ya kufanya muziki wa ‘live’ na kuhusisha vionjo vya Kiafrika kwenye muziki wangu," alisema Lady JayDee.

Kwa upande wake msanii wa mkongwe wa muziki nchini, Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’ alieleza kuguswa na kifo cha Oliver Mtukudzi kwa kuwa alikuwa akiupenda sana muziki wake. "Nimeshtushwa na kifo chake pili imeniuma sana kwa sababu nilikuwa nampenda na napenda kazi zake" alisema Kiki.

Mdua wa muziki Songoro Mnyonge wa Dar es Salaam, kwa upande wake alimuelezea Oliver kuwa Afrika imempoteza mwanamuziki nguli aliyekuwa mcheshi, akiimba kwa hisia huku akilicharaza gitaa lake. Mnyonge amesema kuwa muziki wake utaishi milele, kwani vionjo vyake ni vya kipekee. Songoro alisema aliwahi kuzungumza na marehemu Tuku katika jiji la Harare ambapo alimwambia kuwa robo tatu ya maisha yake amehudumu katika muziki.

Licha ya kuitangaza Zimbabwe duniani kote kupitia kwa muziki wake, Tuku pia alikuwa ni mpigania haki za binadamu duniani pamoja na kuwa balozi wa hisani wa Shirika la umoja wa mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.

Wasifu wake

Oliver Mtukudzi alizaliwa Septemba 22, 1952 mjini Highfield, Harare nchini Zimbambwe. Alikuwa ni miongoni mwa wanamuziki walio maarufu kwa muda mrefu katika nchi hiyo ya Zimbabwe. Oliver alianza kutambulika zaidi kimuziki baada ya kuingia katika Kundi la Wagon Wheels mwaka 1977, akiwa na wenzake kadhaa akiwamo Thomas Mapfumo.

Wimbo wake wa kwanza ulikuwa wa ‘Dzandimomotera’ ulioheshimika sana, na hapo ndipo alipotoka na albamu yake ya kwanza iliyomletea mafanikio makubwa zaidi. Nguli huyo alitoa alitoa albamu kuanzia mwaka 1978, za Chokwadi Chichabuda na Muroi Ndiani za mwaka 1979. Mwaka 1981 alitoa albamu ya Shanje na Pfambi na katika kipindi cha mwaka 1982, akaacxhia albamu ya Maugira na Please Ndapota wakati mwaka 1983, alikuja na alamu ya Nzara na Oliver’s Greatest Hits.

Albamu nyingine za mhenga huyo zilikuwa za Hwema Handirase, Mhaka, Gona,Zvauya Sei, Wawona, Nyanga Yenzou, Strange, Isn’t It?, Sugar Pie, Grandpa Story, Chikonzi, Pss Pss Hallo na Shoko. Mtukudzi hakuishia hapo kwani aliachia albamu zaingine za Mutorwa, Rombe, Rumbidzai Africa, Ziwere MuKobenhavn, Was My Child, The Other Side na Live in Switzerland.

Zingine ni pamoja na Ndega Zvangu, Dzangu Dziye, na Tuku Muzic na nyingine nyingi.

Aidha, Mtukudzi aikuwa ni mmoja wa wanakundi la Mahube, lililokuwa ni la muziki la nchi za Afrika Kusini. Alikuwa ni baba wa watoto watano na wajukuu wawili. Watoto wawili kati ya hao, ni wanamuziki.

Mtukudzi amefariki akiwa na umri wa miaka 66, alikuwa baba wa watoto watano na wajukuu wawili. Alikuwa kati ya watoto sita dada zake wanne na wa kiume wawili, mmoja ambaye alikuwa kaka yake alikwishafariki.

Licha ya muziki Tuku alikuwa akifurahia kuogelea katika bwawa lake (swimming pool) ambalo lina umbo la gitaa la solo. Mwanamuziki huyo wa Kimataifa alikwisha tunukiwa tuzo ya tatu na kuweza kutoa zaidi ya albamu 40.

Oliver alishinda tuzo nyingi mno hata nyingine hakuweza kuzikumbuka. Moja ya tuzo hizo ni ile iliyobeba heshima ya udaktari kutokana na kuwa mshauri na balozi mzuri wa muziki.

Mwaka 2003 alitunukiwa tuzo kubwa ya heshima na Chuo Kikuu cha Zimbabwe kwa kutambua mchango wake na kujitolea katika kujenga muziki na msukumo kwa wasanii wa kizazi kipya nchini Zimbabwe, huku akionesha ushawishi kwenye kazi za wasanii hao kwa miongo kadhaa.

Mwaka 2009, Chuo Kikuu cha Wanawake cha Afrika kilimpatia tuzo ya shahada ya sanaa na kumwelezea mwanamuziki huyo kama mbunifu wa hali ya juu kuwahi kutokea nchini Zimbabwe katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita.

Wengi wanamfahamu Mtukudzi kutokana na umahiri wake mkubwa katika medani ya muziki, utambulisho wake mkubwa ukiwa ni sauti yake nzito na ya kipekee. Licha ya Oliver kuwa mwanamuziki, pia ni mfanyabiashara, mwanaharakati wa haki za binadamu na balozi wa UNICEF Kusini mwa Bara la Afrika.

Mara nyingi Tuku alikuwa akiimba nyimbo katika lugha tatu tofauti za Kishona, Kindebele na Kiingereza. Alikuwa akichanganya ala za muziki wa kiasili kwenye nyimbo zake, jambo lililompa umaarufu mkubwa dunia nzima.

Tofauti na wenzake katika kundi la Wagon Wheels waliokuwa wa kimwimba vibaya Rais wa zamani wa nchi hiyo, Robert Mugabe, Mutukudzi alikuwa akimsifia sana na kusababisha anufaike kwa misaada mbalimbali kutoka serikalini.

Kati ya wasanii wenzake waliokuwa wakiunda kundi la Wagon Wheels, ni yeye pekee aliyekuwa amebakia kufuatia wenzake wote kufa kwa Ukimwi. Mwaka 2010, mwanawe kipenzi, Sam Mutukudzi, ambaye naye alikuwa mwanamuziki, alifariki dunia kutokana na ajali mbaya ya gari. Mutukudzi amekuwa akidaiwa mara kwa mara kwamba alikuwa mwathirika wa ugonjwa wa Ukimwi, ingawa mwenyewe alikuwa akikanusha vikali madai hayo.

Hivi karibuni, mashabiki wake nchini humo walipatwa na mshangao mkubwa baada ya kitabu kiitwacho ‘Tuku Backstage’ kuvuja kikiwa na kashfa nyingi za ngono zinazomhusu gwiji huyo, mwandishi akiwa ni Shepherd Mutamba.

Oliver Mutukudzi ameacha albamu za nyingi baadhi yake ni kama ‘Ndipeiwo Zano’ ya mwaka 1978, ikarudiwa tena mwaka 2000, ‘Chokwadi Chichabuda’ na ‘Muroi Ndiani?’ za mwaka 1979, ‘Shanje’ na ‘Pfimbi’ za mwaka 1981, ‘Nhava’ ya mwaka 2005, ‘Wonai’ ya 2006, ‘Tsimba Itsoka’ na nyingine nyingi.

Safari yake ya muziki ilianza mwaka 1977, alipojiunga na bendi ya Wheels ambako alikuwa akiimba na Thomas Mapfumo ambako walitoa muziki wao wa kwanza wa Dzandimomotera ambao ulifanya vizuri sana na kupelekea utoaji wa albamu yao ya kwanza ambayo pia ilifanya vizuri katika soko la muziki.

Sauti yake yenye mvuto wa kukwaruza , ilikuwa ndio utambulisho mkubwa ndani na nchi ya Zimbabwe. Nyimbo zake nyingi alikuwa akiimba kwa lugha yake ya Kishona na kundi lake la Zimbabwe KoreKore. Pia alikuwa akichanganya na lugha na midundo ya asili na kufanya muziki wake uwe na mvuto wa kipekee.

Wanamuziki wengi wa Zimbabwe na wa Afrika wamenufaika na mafunzo ya kimuziki kwa njia moja ama nyingine katika kipindi chote cha maisha yake ya kimuziki. Mwaka 2010 alituzwa Tuzo kutoka chuo kikuu cha Zimbabwe, ya The international Council of Afrinana Womenism Award. Hiyo ilitokana na mchango wake mkubwa wa kuwainua wanawake kupitia Sanaa ya muziki.

Hata hivyo kila mtu kwa ujumla huwa anamapenzi ya kitu fulkani kwenye maisha yake ya kkila siku anapokuwa akipata fulsa ya kupumzika baada ya kazi ya kutafuta riziki yake. Wapo wanapenda kuangalia mpira wa miguu, sinema, kufanya mazoezi, kuangalia mifugo yao, bustani, na wengine kuwatembelea wagonjwa na ndugu zao na kuongelea. Hali hiyo hufanywa na baadhi ya nyota ili kupunguza mawazo, yao baada ya kazi zao nzito.

Mwanamuziki Oliver Mtukudzi ‘Tuku’ kila mara alipokuwa akipata muda wa kupumzika, alikuwa anapenda sana kuogelea kwenye bwawa lake (swimming pool) ambalo limejengwa kwa umbo la gitaa. Alikuwa anafurahi sana kupumzika hapo huku akiangalia umbo laeneo la bwawa hilo ambappo aliwahi kudai kuwa lilikuwa linampa faraja kujua wajibu wa kazi yake.

Aidha Tuku alikuwa amejaaliwa vipaji vingi kikiwemo cha uigizaji. Aliweza kutengeneza filamu ya Jit, Neria na Tsisi Dangarembga mwaka 1993. Oliver Mtukudzi ‘Tuku’ haupo duniani ila muziki wako utadumu daima milele. Mungu aipumzishe roho yako pahala pema peponi, Amina.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...