Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Amon Mpanju akiwa na Mkurugenz wa Mashtaka (DPP) Bw. Biswalo mganga na wanasheria wengine nje ya Gereza Kuu Lilungu la Mtwara baada ya kulitembelea na kuzungumza na wafungwa na mahabusu walioko ndani ya gereza hilo mjini Mtwara. 


Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara Mhe. Ngwembe akizungumza na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Amon Mpanju (mwenye miwani), Mkurugenzi wa Mashtaka DPP Bw. Biswalo Mganga (wa kwanza kushoto), Naibu DPP Dkt. Edson Makallo (wa kwanza kulia) walipomtembelea Ofisini kwake mjini Mtwara wakati timu ya wanasheria wakiongozwa na Bw. Mpanju walipokuwa mjini Mtwara kutembelea gereza kuu la Lilungu.


Naibu DPP Dkt. Edson Makallo (wa kwanza kushoto) akizungumza kitu na Mkuu wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Newala wakati timu ya wanasheria ilipokuwa wilayani humo kutembelea gereza la wilaya hiyo na kuzungumza na wafungwa na mahabusu na kutatua kero za kisheria wanazokabiliana nazo.
Hakimu Mfawidhi wa Wilaya ya Newala (katikati) akizungumza na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Amon Mpanju (kushoto) na Naibu DPP Dkt. Edson Makallo (kulia) walipomtembelea Ofisini kwake mjini Newala wakati timu ya wanasheria wakiongozwa na Bw. Mpanju walipotembelea gereza la wilaya hiyo.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Amon Mpanju na timu ya wanasheria wakiwa nje ya Gereza la Wilaya ya Newala baada ya kulitembelea na kuzungumza na wafungwa na mahabusu walioko ndani ya gereza hilo mjini Newala.
Mkuu wa Gereza la Wilaya ya Newala Mrakibu Mwandamizi wa Magereza Juma Mgunda aliyeshika karatasi akijiandaa kusoma taarifa ya gereza kwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Amon Mpanju wa kwanza kulia alipofika katika gereza la Wilaya ya Masasi kulitembelea na kuzungumza na wafungwa na Mahabusu
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Amon Mpanju na timu ya wanasheria wakiwa nje ya Gereza la Wilaya ya Masasi baada ya kulitembelea na kuzungumza na wafungwa na mahabusu walioko ndani ya gereza hilo mjini Masasi.

………………..

Timu ya Wanasheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), Mahakama, Jeshi la Polisi na Jeshi la Magereza mkoa wa Mtwara wamefanya ukaguzi katika Magereza mkoani Mtwara kusikiliza na kujionea changamoto za kisheria zinazowakabili wafungwa na mahabusu walioko ndani ya magereza mkoani humo.

Timu hiyo inayoongozwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Bw.Amon Mpanju na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Dkt. Edson Makallo imetembelea gereza Kuu la Lilungu lililoko Mtwara mjini, gereza la wilaya ya Newala na gereza la wilaya ya Masasi.

Timu hiyo imefanya ukaguzi wa maeneo yanayotumiwa na wafungwa na mahabusu ndani ya magereza hayo na kuzungumza nao ili kujua changamoto za kisheria na kijamii zinazowakabili na kuchukua hatua stahiki.

Katika ziara hiyo Timu ya wataalamu hao imechukua majina ya mahabusu ambao kesi zao ni ndogo ndogo na waliokiri kufanya makosa husika na kujutia, wenye watu wa kuwawekea dhamana, walio tayari kulipa fedha za vitu walivyoiba, au kurudisha vitu walivyoiba, kupigana, kutukanana na wako tauari kuombana msamaha, kujeruhiana na walioafikiana kumaliza kesi zao nje ya mahakama ili ziweze kufutwa na hivyo kuachiwa huru baada ya DPP kujiridhisha nayo.

Timu pia kwa kushirikiana na Mahakimu wa Mkoa na Wilaya husika wamekubaliana kufanya mapitio ya adhabu za wafungwa wa chini ya miaka mitatu ili wabadilishiwe adhabu kwa kufanya kazi za jamii au vifungo vya nje ambapo wakimaliza watakuwa raia huru.

Akizungumza ndani ya magereza hayo Naibu Katibu Mkuu Bw. Mpanju amesema ukaguzi huo ndani ya magereza hayo ni jukumu la kisheria la Wizara ya Katiba na Sheria na taasisi zinazohusika na utoaji haki nchini.

“Sisi kama Wizara na taasisi zote zilizo katika mfumo wa utoaji haki nchini ni jukumu letu kisheria kuangalia jinsi mambo yanavyoendeshwa humu ndani na wadau wetu, kutembelea huku kunatuwezesha kuona kama mwanachi anapata haki yake kwa mujibu wa Sheria, na ikiwa kuna tatizo ni wajibu wetu kumuondolea kero za kisheria akiwa humu ndani,ndio maana tunafanya ukaguzi huu na kuzungumza nanyi ili tuwasikie na kuondoa kero au malalamiko mtakayotuambia,” alisema Bw.Mpanju.

Akizungumza baada ya kubaini mahabusu na wafungwa watakaonufaika na ziara ya wataalamu hao Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Dkt.Edson Makallo amewataka wananchi hao ambao watafutiwa Mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili na wafungwa watakaopata adhabu mbadala kuwa raia wema na kubadili mienendo yao ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za ujenzi wa Taifa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...