Wananchi wanaonufaika na mpango wa kunusuru kaya maskini (TASAF) wametakiwa kutunza na kuiendeleza miradi waliobuni na kutekelezwa na serikali ili iendelee kuwahudumia na kuwanufaisha mara baada ya kumalizika kwa kipindi cha miradi hiyo.

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Shaaban Seif Mohamed alieleza hayo wakati alipokuwa katika ziara maalum iliojumuisha Wilaya ya Magharibi “A”na Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa lengo la kukagua miradi hiyo ya TASAF awamu ya tatu na kusikiliza changamoto zinazowakabili wananchi hao ili kuzipatia ufumbuzi.

Katibu Mkuu Shaabani alisema, serikali imekuwa mstari wa mbele katika kuwaanzishia wananchi wake miradi mbali mbali lakini hujitokeza changamoto ya kuilinda na kuendeleza miradi hiyo pale serikali inapoiwacha mikononi mwa wananchi pindi miradi inapofikia ukingoni.

Akikagua kituo cha Afya kilichopo Kianga na Nyumba ya Madaktari iliopo Matamwe Kijini ambavyo vyote vimesaidiwa kupitia Mradi wa TASAF Katibu Mkuu amesema wananchi wanapaswa kuiendeleza miradi hiyo kwa niaba ya serikali na wasisite kuwachukulia hatua endapo watawaona watu wasiokuwa waaminifu wakiharibu miradi yao.

“Baadhi ya watu hawathamini jitihada za serikali ambazo zinalenga kuwaletea maendeleo wananchi wake, hivyo hufanya hujuma za makusudi nawaombeni msisite kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria za nchi” Alieleza Katibu Shaaban.

Katika ziara hiyo ametembelea mradi wa Kilimo katika bonde la kizimbani bonde ambalo Mpango wa kunusuru kaya maskini umeliendeleza kwa kuligawa kwa kujenga matuta maalum na kuweka miundombinu ya kupitishia maji kwa vile serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Dk. Ali Mohamed Shein itaendeleza jitihada hizo.

Akitolea ufafanuzi suala la baadhi ya watu kutoa upinzani kwa kuwabeza na kuwapuza katika shughuli zao za kilimo alisema serikali italipatia ufumbuzi suala hilo kwa kuendelea kuwaelimisha watu hao ili waachane na vitendo visivyofaa ili lengo la serikali la kuwaletea maendeleo wananchi wake liweze kufikiwa.

Wakulima walionufaika na mradi wa kupunguza Kaya Maskini walimueleza Katibu Mkuu kupitia ziara yake hiyo kuwa, wameishukuru serikali ya mapinduzi kutokana na miradi walioanzishwa imewaletea matunda kwa kupata kipato kinachowasaidia katika kutatua matatizo yanayowakabili.

Pamoja na mambo mengine wananchi hao kupitia katibu mkuu huyo wameiomba serikali kuwapatia vifaa vitakavyowasaidia kuendeleza shughuli zao za kilimo ili waweze kuzalisha za kupata kipato cha ziada.

Akiwa katika kijiji cha Kijini Katibu mkuu Shaaban alipokea changamoto inayolalamikiwa na wananchi hao juu ya kukosekana kwa daktari wa kudumu katika spitali yao licha ya kuchukuwa jitihada ya kujenga nyumba maalum ya kulala daktari pamoja na kuweka miundombinu yote ikiwemo umeme, maji safi na salama.

Wamesema kukosekana kwa daktari wa kulala kijijini hapo kumepelekea wananchi wanapatwa na maradhi nyakati za usiku kupata usumbufu na kupelekea kutafuta huduma masafa marefu.

Nae Mkurugenzi Uratibu wa shughuli za serikali SMT, SMZ Khalid Bakar Amrani amewaeleza wananchi hao kuwa hivi sasa serikali ipo katika mchakato wa kuwapelekea awamu nyengine ya TASAF. hivyo amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kupitia kwa masheha katika shehia zao na kutoa taarifa sahihi zitakazoisaidia serikali kupanga mipango yake.

Ziara hiyo ya Katibu mkuu imejumuisha shehia za Kianga, Kizimbani, Donge mbiji, na matemwe kijini ambapo amepata fursa ya kutembelea miradi ya ujenzi wa Vituo vya Afya na Kilimo iliyobuniwa na wanakaya husika.

Kassim Salum Abdi
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Mashamba ya kilimo cha mpunga cha Kizimbani yanayoendelezwa na Wakulima kupitia Kaya Maskini chini ya Mradi wa Tasaf Awamu ya Tatu.
Wanakaya Maskini wa Kijiji cha Donge Mbiji wakifurahia ujio wa Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Shaaban Seif hayupo pichani alip[ofanya ziara ya kuangalia changamoto zinazowakabili.
Sheha wa Shehia ya Donge Mbiji Abdulla Machano Haji akitoa maelezo kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Shaaban Seif alipofika kuangalia changamoto zinazowakabili.


Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Shaaban Seif Mophamed akizungumza na Wananchi wa Matemwe Kijini kwenye Kituo cha Afya cha kijiji hicho alipokuwa katika zaiara ya kutembelea Miradi ya Tasaf iliyobuniwa kwa Kaya Maskini.Wa kwanza kutoka Kushoto ni Mkurugenzi Uratibu wa shughuli za serikali SMT, SMZ Khalid Bakar Amrani.
Muonekano wa Kituo cha Afya cha Shehia ya Kianga kilichojengwa kupitia Mradi wa Tasaf Awamu ya Tatu kikiwa katika hatua ya mwisho lakini tayari kimeanza kutoa huduma.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...