Na Karama Kenyunko, Globu ya Jamii
WATU watano wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka ya kuchapisha picha za ngono kupitia mtandao wa kijamii wa WhatsApp.

Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka yao leo Aprili 9, na wakili wa serikali Jenipher Masue ambaye amesema washitakiwa ni Willium Kimaro (35), Oscar Mariselian maarufu Wizkid (30), mkazi wa Nkuungu Dodoma, Doa Godfrey (36), mfanyabiashara, Feisal Mohammed (27) mkazi wa Ilala, Adulrahman Muhidin (34) mkazi wa Temeke Dar es Salaam ambaye ni Ofisa Usafirishaji.

 Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Augustina Mmbando imedaiwa kila mshitakiwa anakabiliwa na shitaka moja kinyume na Sheria ya Makosa ya Mtandao kifungu namba 14 (1) (a) na kifungu cha (2) (a) namba 14 ya mwaka 2015 ambapo wanadaiwa kutenda makosa hayo Aprili 4 na 5, 2016 maeneo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Imedaiwa, Aprili 4, 2016 Mariselian alichapisha picha za ngono kupitia mtandao wa WhatsApp huku akijua kuwa ni kinyume na sheria huku  Kimaro, Godfrey, Mohammed na Muhidin walichapisha picha chafu  kupitia mtandao huo ambazo ni kinyume na sheria hiyopia.

Hata hivyo, wshitakiwa hao wamekana kutenda makosa hayo na wameachiwa huru kwa dhamana baada ya kutimiza masharti yaliyowekwa na mahakama ambayo yaliwataka kila mmoja kuwa na mdhamini mmoja kutoka taasisi inayotambulika mwenye kitambulisho ambaye atasaini bondi ya Shilingi milioni tano. 

Aidha, mahakama imewataka wadhamini kuhakikisha wanatimiza wajibu wao wa kuhakikisha washitakiwa wanafika mahakamani hapo kila tarehe kesi hiyo itakapotajwa

Pia alisema kwa mshitakiwa ambaye ni mkazi wa Dodoma, kuhakikisha kuwa anafika mahakamani kwa sababu mahakama haikutaka kuzuia washitakiwa kutoka nje ya Dar es Salaam kwa sababu hiyo.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na Hakimu Mmbando ameahirisha kesi hiyo hadi Mei 9, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...