Na Moshy Kiyungi

Huwezi kuzungumzia historia ya muziki toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pasi kuitaja bendi ya Zaiko Langa Langa. Bendi hiyo ilianzishwa rasmi mwaka 1970 wakati huo ikijulikana kama Orchestra Zaiko.

Baadae kidogo mashabiki wakaanza kuwaita Langa Langa wakimaanisha “Kulewa” kwa kuwa nyimbo zao zilikuwa zikipigwa sana kwenye vilabu vya pombe.

Kama siyo kutoka ubavuni mwake, basi bendi nyingi, kama si zote ambazo zinazotamba nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa sasa, zimeasisiwa na wanamuziki ama waliotoka ndani ya bendi hii au katika bendi zilizoanzishwa na wakali waliopata kuipigia.

Hiyo ndiyo Zaiko Langa Langa, bendi kongwe nchini humo kwa sasa ambayo bado inaendelea kudunda licha ya wimbi kubwa la kuhamwa na wanamuziki mahiri pamoja na ushindani uliopo hivi sasa. Zaiko Langa Langa ni chuo cha muziki katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, kwa sababu bendi nyingi zinazotamba hivi sasa, ambazo zilianzishwa kuanzia miaka ya 1970, ni matunda yake.

Zaiko inaweza kulinganishwa na bendi ya Msondo Ngoma ya hapa nchini kwa historia zao zinavyokaribiana. Msondo Ngoma na Zaiko Langa Langa, zimetoa wanamuziki wengi wenye majina makubwa kimuziki.

Ukitaja wanamuziki nyota wa nchini humo akina Papa Wemba, Bozi Boziana, Dindo Yogo, Evoloko Ley Ley ‘Joker’, Defao Matumona, Koffi Olomide, na wengine wengi, chimbuko lao limetoka kwenye shina la Zaiko Langa Langa.

Bendi nyingi kama Isifi Lokole, Yoka Lokole, Viva la Musica, Langa Langa Stars, Zaiko Familia Dei, Choc Stars, Le Anti Choc, Le Grand Zaiko Wawa, Quartie Latin na nyinginezo nyingi zimetoka kwenye chimbuko la Zaiko ambayo sasa inajulikana kama Zaiko Langa Langa Nkolo Mboka, yaani ‘Wakuu wa Mji’.

Idadi kubwa ya bendi zilizotokea ubavuni mwa Zaiko Langa Langa zimekuwa zikijiita ‘Ukoo wa Langa Langa’ (Clan Langa Langa).

Bendi hizo ni Isifi Lokole iliyoanzishwa na Papa Wemba, Bozi Boziana, Evoloko Jocker na Mavuela Somo, Yoka Lokole iliyoanzishwa na Papa Wemba, Bozi Boziana na Mavuela Somo. Bendi ya Grand Zaïko Wa Wa iliyoanzishwa na Felix ‘Pepe’ Manuaku Waku aliyeungana na Shimita El Diego na Djo Poster. Bendi ya Viva La Musica iliyoanzishwa na Papa Wemba akiwa na Emeneya Mubiala na Theodore Djangi Dindo Yogo.

Bendi ya Choc Stars iliyoanzishwa na wanamuziki akina Bozi Boziana, Tshimpaka Roxy na kuungana na akina Ben Nyamabo, Carlito Lassa, na Defao Matumona.

Bozi Boziana akiungana na Deyesse Mukangi, Jolie Detta, Dodoli, Walingonda, Fifi Mofude, na wengineo waliungana na kuanzisha bendi ya L'Orchestre Anti-Choc.

Langa Langa Stars iliyoanzishwa na Waze la Mbongo Kiamuangana Mateta ’Verckys’, Evoloko Jocker, Tshimpaka Roxy, Emeneya Mabiala na Djo Mali.

Zaiko Langa Langa Familia Dei, ilianzishwa na akina Lengi Lenga, Ilo Pablo, Bimi Ombale, Beniko Popolipo, Petit Poisson, na Djimi Yaba.

Zaïko Langa Langa Nkolo Mboka yenyewe chini ya N'Yoka Longo, Meridjo, Oncle Bapius, Zamuangana, Nono Atalaku, Mbuta Matima, Malage de Lugendo, Adamo Ekula, Baroza, na Shiro Shiro. Ikaanzishwa bendi zingine za Zaiko Universel chini ya wanamuziki Meridjo na Oncle Bapius Muaka wakati bendi ya Langa Langa Rénove ikiongozwa na mwanamzuiki Evoloko Jocker.

Histori ya bendi ya Zaiko Langa Langa imekuwa ikikosewa na baadhi ya watu wakataja ilianzishwa mwaka 1970. Yasadikika kuwa bendi hii ilianzishwa rasmi Desemba 24, 1969 jijini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakati huo ikijulikana kama Orchestra Zaiko.

Wakati huo muziki wa Kongo ulitawaliwa zaidi na bendi za African Jazz ya Joseph Athanase Tchamala Kabaselleh ‘Le Grand Kalle’, African Fiesta ya Nicolas Kassanda wa Mikalay maarufu kama Dk. Nico, Tout Puisant Orchestre Kinnie Jazz (TP OK Jazz) ya L’Okanga La Ndju Pene Luambo Luanzo Makiadi Franco na hata African Fiesta National ya Pascal-Emmanuel Sinamoyi Tabu, almaarufu Tabu-Rey Rochereau, aliyoianzisha baada ya kutengana na Dk. Nico na mwaka 1970 akaibadili jina na kuiita Orchestre Afrisa Intanatinale.

Waanzilishi wa Zaiko Langa Langa walikuwa wanamuziki ambao baadhi walikuwa wanapigia bendi ndogo ndogo za mitaani na wengine walikuwa wanafunzi.

Baadhi yao ni mpiga Konga maarufu D.V. Moanda, ambaye jina lake halisi ni Vital Moanda-di Veta Marcelin Delo, Henry Mongombe, Olemi Eshar-Eshar dem'belina, Andre Bita, Mavuela ‘Somo’ Simeon, Evoloko Lay Lay ‘Joker’, Teddy Sukami, Oncle Bapius aliyekuwa akipiga bass, Zamuangana Enock le Meilleur, baba ya wapiga solo wa kizazi kipya Kongo Felix Manuaku Waku na N'Yoka Longo Mvula, anayelikana kama Jossart, ama Vieux Mbombas ambaye asili yake ni kutoka nchini Angola.

Hawa walikuwa wakipiga muziki wa Soukous. Katika upande wa Pop waliokuwa wakifungua pazia katika shoo zote za bendi hiyo, kulikuwa akina Bimi Ombale, Mbuta Matima Zephirin na Mashakado Mbuta.

Historia inaonesha kuwa wanamuziki akina Moanda, Mongombe, Marcelin, Waku, N’Yoka Longo na Andre Bita walitokea kwenye bendi ya mtaani iliyojulikana kama Bel Guide National. Wote hawa walikuwa wanafunzi wakitokea katika familia za matajiri jijini Kinshasa.

Baadaye Zaiko ikamchukua bwana mdogo aliyekuwa na umri wa miaka 19 wakati huo, ambaye alikuwa anaimba kwaya kanisani, Jules Shungu Wembadia Pene Kikumba, maarufu kama Papa Wemba. Bendi hiyo hivi sasa ipo ikiongozwa na mkongwe N’Yoka Longo Mvula.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...