Na Lorietha Laurence-WHUSM, ARUSHA
Makatibu Wakuu wa Wizara ya Habari ,Utamaduni,Sanaa na Michezo Bibi. Susan Mlawi na Katibu Mkuu Wizara ya  Elimu , Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo pamoja na Kaimu Mkuu wa Chuo cha Ufundi Arusha Dkt. Masudi Senzia wamekutana na Viongozi wa Wazee wa Kimasai ili kupata suluhu la eneo la kimila  maarufu kama Oreteti Loongaik lililopo ndani ya chuo hicho.
Kikao hicho kimefanyika leo Jijini arusha  katika Ofisi za Kaimu Mkuu wa Chuo Cha Ufundi Arusha agenda  kuu zikiwa ni kuongezewa eneo ili wazee wa kimila waweze kufanya shughuli zao za mila kwa nafasi, kupewa kibali cha kujenga nyumba kwa ajili ya kujihifadhi wakati wa mvua pamoja na kuwa na geti la kuingilia tofauti na geti la chuo.
Makatibu Wakuu hao walipata wasaa wa kuwasikiliza , kujadiliana pamoja na kutembelea eneo hilo la kimila ili kuweza kuona ni kwa namna gani wanaweza kutoa maamuzi ambayo hayataadhiri upande wowote na hivyo kufikia muafaka mzuri.
“Serikali inatambua umuhimu wa kuenzi na kudumisha mila na ndio maana tupo hapa leo ili kuweza kupata suluhisho la kudumu kuhusu eneo hili ambalo limekuwapo tangu enzi na enzi” alisema Bibi. Susan Mlawi.
Aidha Katibu Mkuu , Bibi. Susan Mlawi aliupongeza uongozi wa chuo kwa kuwaruhusu Wazee hao kuweza kufanya shughuli  za kimila katika eneo hilo na hivyo kusaidia katika kuendeleza utamaduni.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo aliwataka Wazee hao wa kimila kuendelea kufuata taratibu za kupata kibali kutoka kwa uongozi wa chuo ili kuweza kufanya vikao vyao vya kimila hadi pale suluhisho la kudumu litakapofikiwa.
“Mapendekezo yenu ni mazuri nasi tumeyapokea na tunaahidi kuyafanyia kazi  ambapo baada ya mwezi mmoja tutarudi tena mahali hapa tukiwa na majibu kutoka kwa viongozi wetu ambao ni Mawaziri wenye dhamana na Wizara hizi mbili” alisema Katibu Mkuu Dkt. Akwilapo.
Kwa Upande wa Mwenyekiti wa Wazee wa Kimasai Bw. Laiza Ole Kisongo ameishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa suala hilo na kuwapa nafasi ya kuweza kujadiliana kwa pamoja ili kufikia muafaka na kujenga taifa lenye umoja na amani.
 Katibu Mkuu Wizara ya Habari ,Utamaduni,Sanaa na Michezo Bibi. Susan Mlawi akifafanua jambo wakati wa kikao na Wazee wa Kimila wa Kimasai kilichofanyika leo Katika Chuo Cha Ufundi Arusha (ATC).

 Katibu Mkuu Wizara ya  Elimu , Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akiongea na Wazee wa Kimila wa kabila la Wamasai wakati wa kikao cha usuluhishi kuhusu eno la kimila  maarufu kama Oreteti Loongaik lililopo katika Chuo cha Ufundi Arusha.

  Mwenyekiti wa Wazee wa Kimasai Bw. Laiza Ole Kisongo akiongea  wakati wa kikao cha usuluhishi kuhusu eno la kimila maarufu kama Oreteti Loongaik lililopo katika Chuo cha Ufundi  Arusha.

 Mwakilishi wa Akina Mama kutoka Jamii ya Kimasai Bibi. Agness John akichangia jambo wakati wa kikao cha usuluhishi kuhusu eno la kimila  maarufu kama Oreteti Loongaik lililopo katika Chuo cha Ufundi Arusha.

  Viongozi wa Wazee wa Kimila wa kabila la Wamasai pamoja na  Makumu Mkuu wa Chuo cha ufundi Arusha Dkt. Erick Mgaya wakiwasikiliza Makatibu Wakuu kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bibi. Susan Mlawi na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu , Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo (hawapo katika picha) wakati wa kikao cha usuluhishi kuhusu eno la kimila  maarufu kama Oreteti Loongaik lililopo katika Chuo cha Ufundi Arusha .

 Katibu Mkuu Wizara ya Habari ,Utamaduni,Sanaa na Michezo Bibi. Susan Mlawi (Mwenye sweta jeusi na Pinki) na Katibu Mkuu Wizara ya  Elimu , Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo (katikati) wakimsikiliza Mwenyekiti wa Wazee wa Kimasai Bw. Laiza Ole Kisongo(kushoto) walipotembelea eneo la kimila maarufu kama Oreteti Loongaik lililopo ndani ya Chuo cha Ufundi Arusha.

Eneo la kimila linalojulikana kama Oreteti Loongaik ambalo ndiyo mahali Wazee wa kimila wa kabila Maasai hukutana na kufanya mashauri mbalimbali yanayohusiana na kabila hilo. Eneo hilo lipo ndani ya Chuo cha Ufundi Arusha .(Picha na Lorietha Laurence-WHUSM,ARUSHa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...