*Hatma ya Kocha kufahamika wiki ijayo ila bodi imemkubali 

*Asema kuhusu usajili wa wachezaji wanasubiri taarifa ya Kocha


Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

BAADA ya timu ya Simba kutangazwa kuwa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Mmilikiwa klabu hiyo Mohamed Dewji 'MO' ametangaza mikakati mbalimbali ya kuisuka timu hiyo ili iwe yenye ushindani zaidi kwa msimu ujao.

Pia ametumia nafasi hiyo kutoa pongezi kwa wachezaji, benchi la ufundi pamoja na Kocha wao kwa kufanikisha kutwaa ubingwa huo kutokana na kazi nzuri ambayo wameifanya katika msimu huu.

Akizungumza leo Mei 22 , 2019 jijini Dar es Salaam, MO ambaye pia ni mfanyabishara maarufu nchini amesema baada ya kufanikiwa kutwaa ubingwa sasa wanajipanga kwa ajili ya kuweka mikakati ya msimu unaokuja hasa kwa kuzingatia ligi itakuwa yenye ushindani mkubwa.


ALICHOSEMA KUHUSU KOCHA 


Kuhusu kocha wao MO amesema kwanza wanampongeza Kocha Patrick Aussems kwa namna ambavyo amefanikiwa kutimiza malengo aliyopewa wakati anakabidhiwa timu.Kocha alitakiwa kuhakikisha anatetea ubingwa wa Ligi Kuu lengo ambalo amelitimiza.

Na kwamba alitakiwa kuipeleka timu hiyo hatua ya mzunguko katika Michuano ya Kombe la Klabu Bingwa Afrika ambapo yeye ameifikisha Simba hatua ya robo faina ambayo ni mafanikio makubwa kwao.

" Kocha amefikisha malengo kwa kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ameiwezesha timu kuingia hatua ya robo fainali michuano ya Klabu Bingwa Afrika.Baada ya wiki moja tutazungumza naye ili kumuongeza mshahara.

"Bodi ya wakurugenzi imejiridhisha na uwezo wa kocha na bahati nzuri kwa muda ambao amekaa tayari amefahamu mazingira ya soka la Tanzania na wakati huo huo anajua kabisa wana Simba wanataka nini?

"Tutaingia naye mkataba wa kuendelea kuinoa timu yetu maana anastahili kwa hatua ambayo ametufikisha kwani ametufanya Simba tuwe na msimu mzuri,"amesema MO.


VIPI KUHUSU WACHEZAJI?

MO hakusita kueleza wazi jukumu la kuingia mikataba na wachezaji kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu itategemea na mapendekezo ya kocha baada ya kutoa taarifa yake kwa Bodi ya Wakurugenzi na wale ambao atataka kuendelea nao tutawapa mkataba mpya.

Amefafanua wataingia mkataba mipya na wachezaji wa ndani ambao watabaki katika Klabu ya Simba na wachezaji wengine watawapaleka kwa mkopo katika timu nyingi zinazoshiriki Ligi Kuu.

Pia MO amesema kwa wachezaji 10 wa kimataifa nalo wanamuachia Kocha atoe mapendekezo yake ya nani anataka abaki na nani aondoke. "Kocha atatoa mapendekezo na Bodi ya Wakurugenzi watayafanyia kazi."

Amefafanua leo usiku wanatarajia kupata taarifa ya Kocha kuhusu wachezaji ambao watabaki kwa ajili ya msimu ujao na wakati huo huo ameeleza kuna wachezaji wengine wapya watasajiliwa kwa ajili ya kuongeza nguvu hasa kwa kuzingatia ligi ijayo itakuwa ngumu na wakati huo huo wana mashindano makubwa ya Klabu Bingwa Afrika.


MAANDALIZI MSIMU UJAO SI MCHEZO

Wakati huo huo MO amesema baada ya kumalizika kwa msimu wa Ligi Kuu Bara kwa mwaka 2018/2019 pamoja na kuweka mikakati ya kusuka kikosi cha Simba, pia wanatarajia katika kipindi cha kuelekea msimu ujao wa ligi timu yao itakwenda nje ya nchi kujiandaa.

MO amesema tayari amefanya mazungumzo na baadhi ya timu kubwa zilizoko Marekani na hivyo wanaweza kwenda kuweka kambi huko au wanaweza kwenda Ureno kwani nako kuna mazungumzo yanaendelea kufanyika na itakupowa tayari watatoa taarifa ya wapi wanakwenda kupiga kambi.

Amefafanua kuwa timu ya Simba katika kujiandaa na msimu huu wa Ligi Kuu ambao umemalizika walienda kuweka kambi nchini Uturuki na mwaka juzi walikwenda Afrika Kusini , hivyo kwa mwaka huu wanajiandaa kwenda katika moja ya nchi hizo kama sio Marekani basi Ureno.


VIPI KUHUSU UBINGWA?

MO ameeleza wazi kuwa amefurahishwa na timu yao kufanikiwa kutwaa ubingwa kwa mara ya pili mfululizo na kwamba kila mchezaji atapewa pikipiki yenye thamani ya Sh.milioni 2.5 kama ahsante yake ambapo anaamini pikipiki hizo kwa kila moja itaingiza Sh.milioni tano kwa mwaka.

"Nilifanya kikao cha siri na wachezaji na katika kuwatia moyo ili kuhakikisha tunachukua ubingwa, niliwaambia kila mchezaji atapata pikipiki .Lengo langu ni kwamba pikipiki hiyo itakuwa kitega uchumi na ndani ya mwaka mmoja mchezaji anaweza kumpa ndugu yake akawa anamletea Sh.15000 kila siku.

"Baada ya mwaka mmoja atakuwa amepata Sh.milioni tano na kisha pikipiki hiyo kumuachia ndugu yake ili naye aweze kujipatia kipato.Hivyo taarifa za kwamba nitawapa Sh.milioni tano kila mchezaji naweza kusema si sahihi au sahihi lakini binafsi niliahidi pikipiki,"amesema MO.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...