*Wasema atakumbukwa kwa wema wake, kujitoa kwa kusaidia jamii ya Watanzania
*Wengine wasema ameacha somo...
Nape akumbuka kikao chao cha mwisho

 
Na Said Mwishehe,Globu ya jamii


VIONGOZI wa ngazi mbalimbali nchini katika Serikali ya Awamu ya Tano pamoja na wabunge wamesema wamesikitisha na taarifa za kifo cha mfanyabiashara maarufu nchini Reginald Mengi.

Mengi aliyezaliwa mwaka 1944 mkoani Kilimanjaro amefariki dunia usiku wa kuamkia leo(Mei 2,2019) akiwa Dubai katika moja ya nchi za Falme za Kiarabu.
Akizungumzia kuhusu taarifa za kifo cha Mengi, Rais Dk.John Magufuli amesema " Nimesikitishwa na taarifa za kifo cha Mzee na Rafiki yangu Dk. Reginald Mengi. 

"Nitamkumbuka kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya Taifa letu na maono yake yaliyopo ktk kitabu chake cha I Can, I Will, I Must. Poleni wanafamilia, wafanyakazi wa IPP na Jumuiya ya Wafanyabiashara."
Wakati huo huo Makau wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema moja ya vitu alivyotuachia Mzee Mengi ni ule wepesi wake wa kusaidia masuala ya kijamii na kwamba Watanzania daima atakukumbuka.

Kwa upande wake Mbunge wa Mtama mkoani Lindi Nape Nnauye amesema kuwa Mengi ameacha alama kubwa."Nimejifunza mengi kwako, Rafiki, Mshikaji, Kiongozi na Mzazi! Ulinifundisha kuwa kukata tamaa ni dhambi! 

"Msalimie mzee Sitta, mkumbushe kile kikao chetu Cha mwisho nyumbani kwako.Pumzika kwa Amani Dk. R.A Mengi,"amesema Nape wakati anaelezea masikitiko yake kutokana na kifo cha mzee Mengi. 

Akizungumzia kifo cha Mengi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Januari Makamba amesema "Pole kwa Jacqueline na Regina, Abdiel and the twins - na familia nzima ya IPP Group. Mungu ailaze roho ya Mzee Reginald Mengi peponi."

Kwa upande wake Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema hivi " Pumzika kwa amani Dk.Reginald Mengi, asante kwa ushirikiano mzuri ulionipatia katika kutekeleza majukumu yangu lakini zaidi kwa kunihimiza mara kwa mara nitamani/kufanya mambo makubwa. 

"Pengo lako ni gumu kuzibika! Pole nyingi kwa Madam JNtuyabaliwe ,watoto, ndugu, jamaa na marafiki. Poleni sana,"amesema Waziri Mwalimu.
Naye aliyewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii Lazaro Nyalandu akizungumzia kifo cha Mengi ametoa pole kwa wana familia, ndugu, jamii na marafiki wa Mengi kutokana na taarifa za kifo chake.

"Hakika, siku za maisha yetu zimehesabiwa na kuandikwa kitabuni. Ameimaliza safari yake hapa duniani. Iwe heri kwake huko ng'ambo ya mto. RIP baba yetu,"amesema Nyalandu.

Kwa upande wake Mbunge wa Iringa Mjini Mchungaji Peter Msigwa amesema kuwa haijalishi tunaishi muda gani hapa duniani, cha msingi unatoa mchango gani hapa duniani kabla ya kifo. "Dk.Mengi si tu uliwavutia wengi ,bali uligusa sana maisha ya wengi , umetuonesha kuziacha jamii zetu bora zaidi kuliko tulivyo zikuta.Pumzika kwa Amani,"amesema.

Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe amesema " Msiba mkubwa kwa Taifa na haswa kwa familia ya Mzee Reginald Mengi. Pole sana JNtuyabaliwe na Watoto, The twins. "Poleni sana Regina, Abdiel na familia nzima ya Makampuni ya IPP. Bwana ametoa na Bwana ametwaa. Mungu ailaze roho ya Mzee Reginald Mengi mahala pema anapostahili."

Mfanyabiashara maarufu Mohammed Dewji 'MO' ameandika hivi "Inna lillahi wa inna ilayhi raji'un. Mwenyezi Mungu ampe pumziko na ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Ameen.RIP Mengi."

Kwa upande wa Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema amesema watu wanagopa kifo, kimsingi tunacho ogopa ni kuwahi kufa kwani kifo hakizuiliki.
"Katika maisha ni vyema kuishi maisha ya baraka na watu wote,ili utakapotangulia maisha yako yaweze kuwa na thamani. Ninamshukuru Mungu kwa ajili ya maisha ya Dk. Mengi,kwani alijua thamani ya ubinadamu,"amesema Lema.

Mbunge wa Kawe Halima Mdee amesema amepokea kwa masikitiko makubwa sana kifo cha ndugu Reginald Mengi.Ametoa pole kwa familia , ndugu, jamii na marafiki.

"Mwaka 2019 unaendelea kuwa wa majonzi kwetu kama Taita, tunapoteza watu makini waliokuwa na mchango mkubwa sana katika ujenzi wa nchi yetu.Upumzike kwa amani Mkuu,"amesema Mdee.
Katika Enzi za Uhai wake Dkt Reginald Abraham Mengi akiwa na familia yake. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...