Na Lilian Lundo - MAELEZO, Dodoma
Wanafunzi Innocent Shirima na Sada Kimangale kutoka shule za Sekondari Moshi (Kilimanjaro) na shule ya Sekondari Kwemnabara (Tanga) wameshinda nafasi ya kwanza ya uandishi wa insha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kwa mwaka 2018.
Wanafunzi hao wamepewa vyeti na zawadi kwa ngazi ya kitaifa, leo Jijini Dodoma na Kaimu Katibu Mkuu ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Dkt. Ave Maria Semakafu.
Akitoa hotuba wakati wa utoaji wa vyeti kwa wanafunzi hao, Dkt. Semakafu amesema Watanzania waache kujizalilisha kwa kusema shule za Serikali sio bora, kwani watoto hao wanaozalilishwa wakienda kwenye ngazi ya Kimataifa wanafanya vizuri.
"Tukio la leo linatuma ujumbe kwa wale wote wanaoiponda elimu ya Tanzania, kwani washidi wa kwanza wa insha za EAC na SADC wote wanatoka katika shule za Serikali  ambazo zinapondwa kila siku," amesema Dkt. Semakafu.
Ameeleza kuwa, walioifikisha Tanzania hapa ilipo ni Watanzania waliosoma hapahapa Tanzania na wala sio watu waliosoma nje ya Tanzania.
Aidha amempongeza Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kufungua na kupaanua wigo wa elimu kwa Serikali kulipa gharama za wanafunzi hivyo kuwezesha watoto wote wa Tanzania kupata fursa kupata elimu.
Kwa upande wake, Mratibu wa mashindano hayo kutoka Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Sylivia Chinguwile amesema mashindano ya uandishi wa insha yamekuwa chachu kwa vijana kufanya utafiti, kujifunza na kufahamu vizuri mchakato na hatua mbalimbali za uimarishaji mahusiano kwa nchi wanachama.
"Mada zinazoshindaniwa huzingatia makubaliano ya wakuu wa nchi, baada ya hapo kila nchi wanachama huwajibika kutangaza na kubainisha vigezo vya ushiriki kama inavyoelekezwa na sekretarieti za jumuiya husika," ameeleza Sylivia.
Amesema, insha hizo huwasilishwa wizarani baada ya kuteuliwa insha bora katika ngazi ya shule na kusahihishwa na jopo la wataalam, ambapo insha bora za SADC hupelekwa Botswana, makao makuu ya SADC ili kushindanishwa na mataifa wanachama wa Jumuiya hiyo.
Kwa upande wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, insha tano bora hupelekwa Arusha makao makuu ya Jumuiya kwa ajili ya kushindanishwa na mataifa wanachama wa Jumuiya hiyo.
Naye, Mshindi wa insha za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Innocent Shirima ambaye pia ni mlemavu wa macho, amesema mashindano yamewapa fursa ya kujifunza masuala ya jumuiya hiyo.
Hata hivyo, ameomba waratibu wa mashindano hayo kuweka kipaumbele  matumizi ya lugha ya kiswahili katika uandishi wa insha ili kuangaza zaidi lugha ya Kiswahili nje ya mipaka ya Tanzania.
Washindi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Kitaifa ni Paschal Thomas kutoka Shule ya Sekondari Kibaha (Pwani), Lazarius Yamawasa kutoka Shule ya Sekondari Mzumbe (Morogoro),  Innocent Shirima kutoka Shule ya Sekondari Moshi (Kilimanjaro), Nasra Kondo kutoka Shule ya Sekondari Kifungilo (Tanga), Hanifa Gunter Harms kutoka Shule ya Sekondari Heritage (Pwani), Mwanaisha Mwalimba kutoka Shule ya Sekondari Kwemkabala (Tanga), Asha Pazi kutoka Shule ya Sekondari Kilangalanga Sekondari (Pwani), Jacquiline Kassian kutoka Shule ya Sekondari Harrison UWATA (Mbeya), Samweli Chale kutoka Mbagala Sekondari (Dar es Salaam) na Coloniel Jishosha kutoka Shule ya Sekondari Shinyanga (Shinyanga).
Washindi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika ni Sada Kimangale kutoka Shule ya Sekondari Kwemnabara  (Tanga), David Mkinga kutoka Shule ya Sekondari St. Augustine Tagaste (Dar es Salaam) na Alex Paul kutoka Shule ya Sekondari Longido (Arusha).
 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Ave Maria Semakafu akizungumza wakati wa hafla fupi ya kutoa zawadi kwa wanafunzi walioshinda mashindano hayo kwa mwaka 2018 leo jijini Dodoma.
 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Ave Maria Semakafu akizungumza wakati wa hafla fupi ya kutoa zawadi kwa wanafunzi walioshinda mashindano hayo kwa mwaka 2018 leo jijini Dodoma.
 Mratibu wa Mashindano ya Insha kwa wanafunzi wa Shule za Sekondari toka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Bi.Sylivia Chinguwile akizungumza wakati wa hafla fupi ya kutoa zawadi kwa wanafunzi walioshinda mashindano hayo kwa mwaka 2018 leo jijini Dodoma. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Ave Maria Semakafu na kushoto ni Kaimu Kamishna wa Elimu Tanzania.

 Kaimu Mkurugenzi wa Miundombinu na Huduma za Jamii toka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Eliabi Chodata akielezea namna ushiriki wa mashindano hayo kwa upande wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakati wa hafla fupi ya kutoa zawadi kwa wanafunzi walioshinda mashindano hayo kwa mwaka 2018 leo jijini Dodoma.
 Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Moshi ya Watu wenye mahitaji maalum, Innocent Shirima  Akitoa neon la shukrani kwa niaba ya wenzake wakati wa hafla fupi ya kutoa zawadi kwa wanafunzi walioshinda mashindano hayo kwa mwaka 2018 leo jijini Dodoma.
 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Ave Maria Semakafu akimkabidhi Cheti cha Pongezi Mshindi wa Mashindano ya Insha kwa Wanafunzi wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Sada  Kimangale kutoka Shule ya Sekondari Kwemkabara ya wilayani Muheza mkoani Tanga leo wakati wa hafla ya kuwapa zawadi washindi wa mashindano hayo kwa mwaka 2018 leo jijini Dodoma.Kulia ni Mzazi wa mwanafunzi huyo.
 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Ave Maria Semakafu akimkabidhi Cheti cha Pongezi na fedha taslimu shilingi Laki Tano Mshindi wa Mashindano ya Insha kwa Wanafunzi wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Innocent Shirima kutoka Shule ya Sekondari Moshi ya Watu wenye mahitaji Maalum. Kulia ni Mkuu wa Shule hiyo hiyo  leo wakati wa hafla ya kuwapa zawadi washindi wa mashindano hayo kwa mwaka 2018 leo jijini Dodoma.
 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Ave Maria Semakafu akimkabidhi zawadi ya fedha Dola za Kimarekani 500 Mshindi wa Mashindano ya Insha kwa Wanafunzi wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Sada  Kimangale kutoka Shule ya Sekondari Kwemkabara ya wilayani Muheza mkoani Tanga leo wakati wa hafla ya kuwapa zawadi washindi wa mashindano hayo kwa mwaka 2018 leo jijini Dodoma.Kulia ni Mzazi wa mwanafunzi huyo.Kushoto ni Bibi. Agnesi Kayola Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda toka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Ave Maria Semakafu akimkabidhi Cheti cha Pongezi Mshiriki wa Mashindano ya Insha kwa Wanafunzi wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), na Jumuiya ya Afrika Mashariki, Hanifa Harms kutoka Shule ya Sekondari Heritage ya Kibaha Pwani wakati wa hafla ya kuwapa zawadi washindi wa mashindano hayo kwa mwaka 2018 leo jijini Dodoma.Kulia ni Mzazi wa mwanafunzi huyo. Bi. Shamim Yunga.
 Baadhi ya wanafunzi walioshinda Mashindano ya Insha kwa Wanafunzi wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki wakifuatilia zoezi la utoaji zawadi wakati wa hafla fupi ya kuwapa zawadi washindi wa mashindano hayo kwa mwaka 2018 leo jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Ave Maria Semakafu akiwa katika picha ya pamoja na Washindi wa Mashindano ya Insha kwa Wanafunzi wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na wazazi wao mara baada ya kumaliza hafla fupi ya kuwapa zawadi washindi wa mashindano hayo kwa mwaka 2018 leo jijini Dodoma. (Picha na Idara ya Habari –MAELEZO).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...