Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed akizungumza na ujumbe kutoka Mji wa Xuzhou Nchini China uliokuja kufanya tathmini ya Madaktari wa nchi hiyo wanaokuja kufanya kazi Zanzibar Ofisini kwake Mnazimmoja Mjini Zanzibar. 
Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed akiagana na Kiongozi wa ujumbe kutoka Mji Xuzhou Nchini China Zhou Guangchum baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliofanyika Ofisini kwake. Picha na Makame Mshenga. 

 

Na Ramadhani Ali – Maelezo Zanzibar 

Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed ameiomba Jamhuri ya Watu wa China kurejesha utaratibu wa madaktari wa nchi hiyo wanaokuja kufanyakazi Zanzibar kukaa miaka miwili badala ya mwaka mmoja wa sasa. 

Alisema tokea kuanzisha uhusiano wa madaktari wa China kuja Zanzibar mwaka 1965 walikuwa wakikaa kipindi cha miaka miwili lakini utaratibu huo ulibadilika miaka ya hivi karibuni na hivi sasa wanakaa mwaka mmoja. 

Waziri wa Afya alitoa ombi hilo alipokutana na Ujumbe wa wataalamu wa afya kutoka Mji wa Xuzhou ambao upo nchini kufanya tathmini ya Madaktari wanaokuja kufanyakazi Zanzibar katika hospitali ya Abdlala Mzee Mkoani na Mnazimmoja. 

Aliueleza ujumbe huo kwamba utaratibu wa zamani wa timu za madaktari wa China kukaa miaka miwili ulikuwa unatoa fursa nzuri kwa madaktari wa Zanzibar kujenga uzoefu na kujifunza mambo mengi ya kitaalamu kutoka kwao. 

Alisema madaktari wa Zanzibar wanapopata uzoefu kwa vitendo kutoka kwa madaktari wa China inawasaidia kufanya vizuri wanapopata nafasi ya masomo ya juu nje ya nchi. 

Waziri Hamad aliushauri ujumbe huo kuwaelekeza madaktari wa China waliopo Zanzibar kuwapa mafunzo madaktari wa Hospitali ya Abdalla Mzee ya kutumia mashine mpya zilizowekwa katika hospitali hiyo na kuitafsiri teknolojia iliyotumika ili baada ya kuondoka waweze kuzitumia. 

Aidha Waziri wa Afya aliwahimiza madaktari wazalendo kuwa tayari kujifunza utaalamu kutoka madaktari wa China ambao wamekuwa wakifanya matibabu ya kitaalamu na kuwashirikisha. 

Kiongozi wa ujumbe huo Zhou Guangchum alimuhakikishia Waziri wa Afya kwamba nchi yake itaendelea kuisaidia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuongeza msaada wake hasa katika sekta ya afya. 

Aliahidi kuwa atalifikisha nchini kwake ombi la kurejesha utaratibu wa zamani wa madaktari wanaokuja Zanzibar kukaa kwa kipindi cha miaka miwili ili waweze kutoa mchango mkubwa zaidi kwa ndugu zao.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...