Daktari wa macho wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila Geofrey Josephat akitumia kifaa maalum kumfanyia uchunguzi mtoto sehemu ya nyuma ya jicho ili kubaini kama ana tatizo. Hospitali ya Mloganzila imefanya zoezi la uchunguzi wa macho bure kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ikiwa ni maadhimisho ya wiki ya saratani ya jicho kwa watoto (Retinoblastoma). 
Mtaalam wa miwani Nestory Massawe akimpima uwezo wa kuona mbali mtoto Shamsa Mbegu.
Daktari Bingwa wa macho Suzan Mosenene (kulia) akimfanyia uchunguzi wa macho mtoto, huduma ya uchunguzi wa macho bure kwa watoto imefanyika Mei 16 hadi Mei 17, 2019.
Baadhi ya wazazi ambao wamewaleta watoto wao katika Hospitali ya Mloganzila kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa macho.





Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imefanya zoezi la uchunguzi wa macho bure kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ikiwa ni maadhimisho ya wiki ya saratani ya jicho kwa watoto (Retinoblastoma).

Katika zoezi hilo ambalo limefanyika Mei 16 hadi Mei 17, 2019 zaidi ya watoto 100 wamehudumiwa ambapo baadhi yao wamekutwa na matatizo ya uoni hafifu, mzio na kovu kwenye macho.

Daktari Bingwa wa macho kutoka Muhimbili Judith Mwende amesema ugonjwa wa saratani ya jicho kwa watoto ni hatari na husababisha upofu na kifo endapo usipotibiwa mapema na wakati mwingine hulazimu kuliondoa jicho ili kuokoa  maisha ya mtoto.

Akifafanua Dkt. Mwende amesema takwimu za miaka mitatu za kutibu na kufuatilia ugonjwa wa saratani ya jicho  kwa watoto katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) takribani asilimia 60-70 ya watoto hao huwa wako kwenye hatua mbaya za ugonjwa.

Hali hiyo husababisha asilimia 50-60 kupoteza maisha kwa sababu ya kuchelewa kufika kupata huduma inayostahili na kwa wakati.

Ametaja  sababu za kucheleweshwa hospitalini ni familia kutokufahamu dalili za  ugonjwa  na hatari zake, wahudumu wa afya ya msingi kuchelewesha rufaa kwa kutofahamu dalili za ugonjwa, familia kukosa nauli kufuata matibabu pindi wakipewa rufaa , familia kutafuta matibabu mbadala mpaka wakiona hatua za mwisho za ugonjwa na kukataa mapendekezo ya wataalam hasa kuliondoa jicho pale inapohitajika ili kunusuru maisha ya mtoto

Dalili za mwanzoni za saratani ya jicho kwa watoto ni weupe kwenye mboni ya jicho ambao unaonekana kirahisi kwenye giza au mtoto akipigwa picha na flush, kengeza, jicho kuvilia damu kuwa jekundu, kubadilika rangi au kuuma.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...