Na Said Mwishehe, Globu ya jamii

ALIYEKUA Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ametakiwa kuachana na mawazo ya kugombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu ujao wa Urais.

Kauli hiyo imetolewa na Kada wa CCM, Ally Mwinyi Simba jijini Dar es Salaam leo ambapo amemtaka Membe na wenzake kufuta wazo la kuwa Rais hadi hapo Rais Magufuli atakapostaafu.

" Tumeshasikia tetesi za wao kuwaza kuweka nia ya kugombea urais katika uchaguzi mkuu ujao wa 2020, Ndugu Membe na wengineo waendelee na shughuli zao nyingine watuachie Mwenyekiti na Rais wetu Magufuli amalizie kazi aliyoianza.

" Tena wakae wakijua wazi hili tutalisimamia kwa nguvu zetu zote kwa sababu tuna imani kubwa na Mwenyekiti na Rais wetu Dk John Magufuli," amesema Mwinyi Simba.

Amesema kwa kazi nzuri ambayo inafanywa na Rais Dk.John Magufuli na Watanzania kwa ujumla wanafunga mkono na kuahidi kumchagua kwenye uchaguzi mkuu mwakani na hivyo wanaoutaka urais kwa sasa hawana nafasi.

Amesema kazi nzuri inayofanywa na Rais Magufuli imekuwa chachu kubwa ya maendeleo na kwa sasa sote tunashuhudia utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo na hivyo lazima Rais apewe muhula wa pili aweze kumalizia kazi kubwa na nzuri anayoifanya kwa ajili ya nchi yetu.

Hata hivyo amefafanua kwa utamaduni na taratibu za CCM Rais anapochaguliwa huuchwa kwa vipindi vya mihula miwili kwa kila muhula kuwa na miaka mitano na ndio maana kuanzia Rais wa awamu ya pili na kuendelea wote wamehudumu kwa miaka 10 ,hivyo Rais Magufuli naye lazima aachwe aendelee kututumikia Watanzania.

Akizungumzia kauli iliyotolewa na Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe kuhusu kauli yake ya kusema wanajiandaa kuchukua Nchi, Mwinyi Simba alimtaka kiongozi huyo ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini kuhakikisha kwanza wanaongeza idadi ya wabunge wa upinzani kabla hawajafikiria kushinda Urais.

Amesema inashangaza kuona Zitto anapiga hesabu zza Urais ilihali wabunge wa upinzani hawafiki nusu ya wale wa Chama cha Mapinduzi.

" Zitto ni mwanasiasa ambaye hana heshima, katika mkutano wake na wandishi wa habari wa Juni 11 mwaka huu alikaririwa akisema kuwa yeye hawezi kusikiliza matamko ya kisiasa bali atasikiliza yale yanayotolewa na Taasisi.

" Lakini anasahau yeye mwenyewe ni mwanasiasa na ametoa matamko ya kisiasa. Zitto anapaswa kufahamu kuwa Watanzania wa Sasa wanafahamu kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya awamu ya tano chini ya Dk John Magufuli," amesema Mwinyi Simba.

Akizungumzia ongezeko la wigo wa walipa Kodi, Mwinyi alimpongeza Rais Magufuli kwa kuimarisha urafiki uliopo kati ya wafanyabiashara na Serikali.

Ametoa rai kwa Serikali kuangalia namna ya kuanzisha Ward Tax Officer (Afisa Kodi Kara) ambao kwa kuanza wanaweza kuwafanyia majaribio katika majiji ambayo kibiashara ukusanyaji wake wa kodi upo juu.

" Afisa Kodi Kata wanaweza kukusanya taarifa kwa usahihi juu ya biashara zilizopo katika kata husika, mikataba inayoingiwa na pia wataweza kutoa elimu juu ya ulipaji kodi na kutengeneza urafiki kati ya mlipaji kodi na watoza kodi," amesema Mwinyi Simba.

Aidha amempongeza Rais Magufuli kwa kuwapa kipaumbele wabunifu wawili wa umeme ambao wamekua wakitatua changamoto ya umeme katika sehemu ambazo wametoka.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...