*Asema ana matumaini makubwa dhidi yao, hivyo wachape kazi
*Awambia anajua watapigwa vita sana lakini watamngulize Mungu

Na Said Mwishehe,Michuzi TV

RAIS Dk.John Magufuli amemtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira pamoja na Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kikamilifu na kwa wakati.

Akizungumza baada ya Simbachawene na Bashe kula kiapo leo Julai 22 mwaka huu Ikulu jijini Dar es Salaam Rais Magufuli amewaambia kuwa wawe chachu ya kuhakikisha changamoto zilizopo zinapata ufumbuzi wa haraka.

Rais Magufuli wakati anamzungumzia Simbachawene amesema Wizara yake inahusika na masuala ya Muungano , hivyo akahakikishe anakuwa chachu ya kuuimarisha muungano na si kuwa chachu ya kuuvuruga.

Kuhusu eneo la mazingira Rais Magufuli amemwambia Waziri Simbachawene kuwa akahakikishe anaisimamia NEMC kuhakikisha vibali vinatoka kwa wakati, kwani kuna ucheleweshaji mkubwa wa vibali NEMC.

"Tunahitaji viwanda hivyo lazima vibali navyo vitoke kwa wakati na ikiwezekana viwanda viwe vinaanza halafu mambo ya vibali yanafuata baadae maana kumekuwa na tabia ya kucheleweshwa kwa vibali.

"Kwa hiyo nenda kasimamie hili , kaa na watalaamu wako kuhakikisha mnasimamia hili la vibali na mambo mengine muhimu.Pia hakikisha unasimamia na kutekeleza majukumu yako kwa wakati.

"Nakumbuka suala la katazo la mifuko ya plastiki nililizungumza kwa muda mrefu lakini hakulitekelewa hadi nilipoamua kutoa maagizo ya lazima ndipo likafanyika. Nenda kafanyie yale ambayo umeyaapa leo hii tena kwa wakati,"amesema Rais Magufuli wakat anatoa maelekezo kwa Simbachawene.

Wakati huo huo amesema kwenye eneo la mazingira kuna fedha nyingi zinaelekezwa huko lakini haziendani na uhalisia na kwamba kumekuwepo na miradi hewa akitoa mfano mradi wa upandaji mikoko Rufiji , hivyo amemtaka Simbachawene kwenda kusimamia vizuri eneo la mazingira.

Pia Rais Magufuli amesema siku za karibuni anajiandaa kufanya mazungumzo na wafugaji wote nchini ili kusikiliza changamoto zao,ili zipatiwe ufumbuzi.

Kuhusu Naibu Waziri Bashe,Rais Magufuli amesema kuwa amekuwa akimfuatilia bungeni na namna ambavyo amekuwa akichambua hoja na mijadaa inayohusu sekta ya kilimo.

"Nimekuwa nikikufuatilia sana unapozungumza bungeni, sasa yale uliyokuwa unayachambua nenda kayafanye kwa vitendo.Najua hutashindwa kutekeleza kwa vitendo.Pia natambua kuna changamoto nyingi katika eneo la kilimo na kutoa mfano kuwa Bodi ya sukari inafanya kazi nzuri sana lakini inapigwa vita sana.

"Nilikuwa nasubiri tu nione kama Waziri wa Kilimo ataivunja bodi lakini ana bahati hakufanya hivyo kwani angekiona cha mtema kuni.Lazima niseme ukweli, bodi inafanya kazi nzuri lakini kuna baadhi ya watu wanaipiga vita kwa maslahi yao binafsi,"amesema Rais Magufuli.

Amefafanua Wizara ya Kilimo ikisimamia vizuri italeta matumaini makubwa kwa wananchi huku akitumia nafasi hiyo anafahamu changamoto iliyopo katika zao la kahawa mkoani Kagera.

"Hata hivyo pamoja na Serikali kutoa maelekezo kuhusu bei ya kahawa, ninazo taarifa kuna wafanyabiashara wameanza kuwadaha wananchi, hao lazima washughulikiwe tena washughulikiwe kwa mkono mkubwa,"amesema.

Rais Magufuli amemtaka Bashe na Waziri wa Kilimo kushirikiana katika kutatua changamoto za sekta ya kilimo huku akitoa rai kuwa lazima wakulima wanufaike na kilimo chao kwa kulipwa fedha zao kwa wakati.

"Katika zao la pamba nako lazima Wizara hii isimame imara kuhakikisha wakulima wa zao hilo wanapata fedha zao kwa wakati .Lazima tuhakikishe wakulima wanyonge wanasimamiwa vema na ukweli uliopo sekta ya kilimo imebeba matumaini ya wananchi walio wengi.Hivyo nenda mkashirikiane kuisimamia vizuri,"amesema Rais Magufuli.

Pamoja na maelekezo ambayo ameyatoa kwa mawaziri hao, Rais Magufuli amesema anajua baada ya kuwaapisha kwenye nafasi hizo watapigwa vita sana lakini wakamtangulize Mungu ili kuyashinda majaribu."Najua mtapigwa vita sana lakini kafanyeni kazi tu."
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mh.Simba Chawene  pamoja na Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...