Na Charles James,Michuzi TV

Naibu Waziri wa Maji Mhe Jumaa Aweso amesema Wizara yake itashirikiana na TAKUKURU ili kujiridhisha katika utekelezaji mradi wa Maji katika kijiji cha Masange Wilayani Kondoa mkoani Dodoma.

Naibu Waziri Aweso ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wa eneo hilo alipofanya ziara ya kukagua na kujionea mradi wa Maji kijiji cha Masange uliogharimu kiasi cha Sh.Milioni 433 baada ya kupewa majibu yasiyojitosheleza na Mkandarasi wa Mradi huo.

“Haiwezekani tukauziwa mbuzi kwenye gunia,lazima kukagua na kujionea,baada ya kupewa majibu ya kusuasua hivyo TAKUKURU tutashirikiana nao kubaini ubadhilifu,na mkandarasi asilipwe mpaka tufanye uchunguzi tujiridhishe''amesema Aweso

Hali hiyo imekuja baada ya Mkandarasi wa mradi huo wa Maji kampuni ya Best One kwa kushirikiana na wataalam wa sekta ya Maji wa halmashauri ya Wilaya ya Kondoa kutoa majibu yasiyoridhisha kuhusu matumizi ya fedha zilizotumika katika mradi huo .

Akijibu kero ya wananchi hao kuhusu Maji Mhe Aweso amepiga simu mbele ya wananchi kwa wataalamu wa Wizara kuulizia taratibu za upatikanaji wa Gari la kuchimba visima katika kijiji hicho ambapo ameahidi kuchimbwa visima viwili kwenye Kijiji hicho ndani ya kipindi cha muda mfupi.

Katika kujiridhisha na mradi huo Mhe Aweso alilazimika kupanda kwenye mlima ambao chanzo cha maji kinapatikana ambapo alikiri kuwepo kwa changamoto Na kuahidi kuzimaliza ili wananchi wa Masange waweze kupata maji na kwenda sawa na kauli mbiu ya kumtua mama ndoo.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kondoa vijijini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dokta.Ashatu Kijaji amesema yupo tayari kufanya kazi hata saa sita usiku na walichomwagiza wananchi wake ni kutatua kero ya Maji .

Dkt.Kijaji amesema kuwa wananchi wa Mtaa wa Masange wamesema adha kubwa inayowakabili ni maji hivyo ni vyema serikali ikafanya mchakato haraka kutatua kero hiyo.

Awali ,akisoma taarifa ya Mradi wa Maji wa Masange mbele ya Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso,Kaimu Meneja wa Wakala wa Maji vijijini[RUWASA]Wilaya ya Kondoa Mhandisi Falaura Seleman Kikusa amesema mradi wa Maji Masange ulianza tangu tarehe 15,Disemba,2014 na kuzinduliwa rasmi tarehe 13,Septemba ,2016 kupitia mbio za Mwenge wa Uhuru huku ukigharimu zaidi ya Tsh.Milioni 433 .

Aidha amebainisha kuwa muda wa utekelezaji wa Mradi huo kwa mujibu wa Mkataba ni kipindi cha miezi mine kuanzia tarehe 15,Disemba,2014,hadi 15,Machi,2015 hivyo kutokana na changamoto mbalimbali hususan kuchelewa kwa malipo ya madai ya mkandarasi,mradi uliongezewa muda wa utekelezaji na kukamilika rasmi mnamo tarehe 7,Juni,2018.

Mhandisi Kikusa ameendelea kufafanua kuwa upatikanaji wa Maji katika kijiji cha Masange haukidhi mahitaji halisi ya maji kwa wakazi wa kijiji hicho kwani huduma ya maji imekuwa ikipatikana kwa mgao kwa vitongoji kwa masaa manne hadi matano.

Amesema chanzo cha kuwepo kwa hali hiyo unatokana na changamoto kadhaa ikiwemo kuongezeka kwa wakazi pamoja na kukua kwa mji wa Masange ,Uwezo wa chanzo cha Maji [lita 119,577.6 kwa siku]kuwa mdogo ikilinganisha na mahitaji halisi ya Maji ya sasa [zaidi ya lita 141,560 kwa siku] na changamoto nyingine ni usimamizi usio mzuri kutoka kwa timu ya mhandisi.

Hata hivyo mkandarasi wa mradi hadi kufikia sasa alishalipwa kiasi cha sh.347,421,000 kati ya gharama 433,288,548 na zilizobaki kwa mujibu ya makubaliano ya mkataba ni Tsh.120,609,648.
Naibu Waziri wa Maji, Mhe Juma Aweso akiwa ameambatana na Wananchi wa Kijiji cha Masange wilayani Kondoa wakati akipandisha Mlima Masange ambao ndipo lilipo Tanki na Chanzo cha Maji kijijini hapo
 Naibu Waziri wa Maji, Mhe Jumaa Aweso akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Masange ilayani Kondoa alipofika kuzungumza nao na kutatua kero ya maji iliyokua ikiwakabili. 
 Mbunge wa Jimbo la Kondoa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe Ashantu Kijaji akieleza changamoto ya maji inayowakabili wananchi wake wa eneo la Masange, Kondoa mbele ya Naibu Waziri wa Maji, Mhe Jumaa Aweso.
 Naibu Waziri wa Maji, Mhe Jumaa Aweso akipanda juu ya Tanki la Maji ambalo linatumika kugawa maji kwa Wanaanchi wa Kijiji cha Masange wilayani Kondoa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...