Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwasikiliza baadhi ya wafugaji na wakulima wanaoishi katika hifadhi ya Wembele iliyopo kijiji cha Makomelo wilaya ya Igunga mkoani Tabora alipokwenda kusuluhisha mgogoro baina yao wakati wa ziara yake ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi na kukagua masijala za ardhi katika mkoa wa Tabora jana
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafugaji na wakulima wanaoishi katika kijiji cha Makomelo wilaya ya Igunga mkoani Tabora alipokwenda kusuluhisha mgogoro baina yao wakati wa ziara ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi na kukagua masijala za ardhi katika mkoa wa Tabora jana.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Igunga John Mwaipopo wakiwasili kijiji cha Makomelo wilaya ya Igunga mkoani Tabora alipokwenda kusuluhisha mgogoro kati ya wafugaji na wakulima wakati wa ziara yake ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi na kukagua masijala za ardhi katika mkoa wa Tabora jana (PICHA ZOTE NA HASSAN MABUYE WIZARA YA ARDHI)

…………………………………………………

Na Munir Shemweta, WANMM IGUNGA

Serikali imeagiza kaya 13 zilizopo eneo la wafugaji katika hifadhi ya Wembele kijiji cha Makomelo kitongoji cha Kitulo wilayani Igunga mkoani Tabora kuondoka katika eneo hilo kwenda eneo ililopangiwa la wakulima ili kuondoa mgogoro wa muda mrefu kati ya wafugaji na wakulima.

Kauli hiyo ya serikali inafuatia wakulima kuvamia eneo la wafugaji katika kijiji hicho na kuzuia wafugaji kulisha mifugo yao jambo lililokiuka makubaliano ya awali ya kila upande kubaki katika eneo lake kwa ajili ya shughuli zake.

Akizungumza na pande mbili za wafugaji na wakulima katika kijiji cha Makomelo akiwa katika ziara yake ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya pango la ardhi na kukagua Masijala ya Ardhi katika mkoa wa Tabora jana tarehe 24 Agosti 2019, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alisema serikali haiwezi kuendelea kuona watu wanapigana na kuuana wakati mipaka ya eneo hilo ilishawekwa.

Alisema, eneo linalogombaniwa na pande hizo mbili linajulikana kama eneo la hifadhi ya Wembele chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii lakini kwa busara serikali iliamua kutoa matumizi kwa ajili ya wakulima na wafugaji na kuweka mipaka lakini wakulima wameamua kukiuka utaratibu na kuvamia eneo la wafugaji kitu alichokieleza kuwa hakikubaliki.

‘’Waliokiuka utaratibu wa awali waondoke, ziko kaya 13 hatuwezi kuendelea na vifo katika haya, serikali ishaweka mipaka kinachotakiwa ni kuheshimu maamuzi’’ alisema Dkt Mabula

Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kinachotakiwa kwa pande mbili zinazogombana ni kuheshimu makubaliano hadi hapo Wizara ya Maliasili na Utalii itakalichukua eneo lake.

Aliwataka wafugaji na wakulima wasiendelee kufanya vurugu na kuheshimu makubaliano waliyokubaliana awali ambapo alimuagiza Mkuu wa wilaya ya Igunga mkoani Tabora John Mwaipopo kuhakikisha anasimamia zoezi la kuondoka kwa kaya 13 katika eneo la wakulima.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kitulo katika Kata ya Igunga Zephania Ndassa alimueleza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwa, eneo hilo limekuwa na mgogoro mkubwa kati ya wakulima na wafugaji pamoja na kuwepo makubaliano yaliyofikiwa mwaka 2004 wakati wa uongozi wa Mkuu wa mkoa wa Tabora wakati huo Marehemu Abbas Kandoro.

Kwa mujibu wa Ndassa pande zinazopingana zinatambua kabisa kama eneo hilo ni hifadhi ya Wembele tangu mwaka 2002 na wao wanalitumia eneo hilo wakifahamu pindi litakapohitajika litachukuliwa na Maliasili lakini mgogoro huo umekuwa ukuwasumbua.

Naye Mkazi wa kijiji cha Makomelo Christopher Shigela alimuomba Dkt Mabula kunusuru mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu hasa baada ya juhudi za wilaya na mkoa kugonga mwamba na kubainisha kuwa, pamoja na uwepo alama zilizoainisha maeneo ya wakulima na wafugaji lakini wakulima wameendelea kufanya uvamizi jambo lililozusha mgogoro uliosababisha watu kuumia na wengine kupoteza maisha.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...